Mechi za maajabu kwa maafande wa JKT Tanzania
Muktasari:
- Licha ya JKT Tanzania kutokuwa na wachezaji wa kigeni kama timu nyingine za Ligi Kuu Bara, imeonyesha ushindani kwa kutegemea wazawa pekee tu kikosini, ambao hadi sasa wamekuwa na mchango mkubwa wa kukisaidia kikosi hicho cha maafande.
UNAPOZUNGUMZIA miongoni mwa timu shindani Ligi Kuu Bara hutoacha kulitaja jina la maafande wa JKT Tanzania kutokana na ushindani inaoendelea kuuonyesha hadi sasa, huku nyuma ya mafanikio hayo makubwa yakiongozwa na kocha mzawa, Ahmad Ally.
Licha ya JKT Tanzania kutokuwa na wachezaji wa kigeni kama timu nyingine za Ligi Kuu Bara, imeonyesha ushindani kwa kutegemea wazawa pekee tu kikosini, ambao hadi sasa wamekuwa na mchango mkubwa wa kukisaidia kikosi hicho cha maafande.
Timu hiyo licha ya msimu huu kubakisha mechi tano za Ligi Kuu Bara, imevunja rekodi ya kukusanya pointi nyingi zaidi tofauti na msimu uliopita wa 2024-2025, huku kwa sasa ikipambania nafasi nne za juu ili kucheza michuano ya kimataifa.
Msimu wa 2024-2025, JKT ilimaliza Ligi Kuu ikiwa nafasi ya sita na pointi 36, baada ya kushinda mechi nane, sare 12 na kupoteza 10, huku safu ya ushambuliaji ya kikosi hicho ikifunga mabao 27 na kuruhusu pia nyavu zake kutikiswa mara 27.
Kwa msimu huu wa 2025-2026, timu hiyo imecheza mechi 25 za Ligi Kuu na kati ya hizo imeshinda tisa, ikitoka sare 11 na kupoteza mitano, ikishika nafasi ya tano na pointi 38 zaidi ya msimu wa 2024-2025, ikifunga mabao 27 na kuruhusu 26.
Licha ya JKT kuvunja rekodi ya kukusanya pointi nyingi msimu huu tofauti na za msimu uliopita, timu hiyo ina mechi ilizoepuka kichapo na kuambulia ushindi au sare baada ya wapinzani kuongoza kufunga bao kama Mwanaspoti linavyozielezea.
Mashujaa FC 1-1 JKT TZ
Timu hizi zilizopanda zote Ligi Kuu Bara msimu wa 2022-2023, zikitokea Championship, msimu huu wa 2025-2026, zilikutana katika mechi ya kwanza kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika, mjini, Kigoma na kutoka sare ya bao 1-1.
Katika mechi hiyo ya maafande iliyopigwa Septemba 18, 2025, Mashujaa ilitangulia kupata bao dakika ya 78, lililofungwa na Mundhir Vuai kisha Paul Peter akaisawazishia dakika ya 86 na JKT kuepuka kichapo ugenini na kuambulia pointi moja.
Coastal Union 1-2 JKT TZ
Hii ni mechi nyingine iliyoshuhudia JKT ikiondoka na pointi tatu muhimu, baada ya wenyeji, Coastal Union kufunga bao la mapema dakika ya 22, lililofungwa na nyota wa timu hiyo, Athumani Masumbuko 'Makambo' kwenye Uwanja wa Mkwakwani Tanga.
Katika mechi hiyo iliyopigwa Septemba 22, 2025, licha ya Coastal Union kupata bao hilo, JKT Tanzania ilijibu mapigo na kusawazisha dakika ya 35, lililofungwa na Salehe Karabaka kisha Mohamed Bakari akaifungia la pili na la ushindi dakika ya 66.
JKT TZ 1-1 Azam FC
Miongoni mwa mechi zilikuwa bora msimu huu, hutoacha kuitaja ya JKT Tanzania dhidi ya Azam FC iliyopigwa Oktoba 1, 2025, kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, Mbweni, jijini, Dar es Salaam, kutokana na ushindani ulioonekana tangu mwanzo.
Katika mechi hiyo, Azam FC ilipata bao la dakika ya 42, lililofungwa na nyota wa kikosi hicho, Feisal Salum 'Fei Toto', ila wakati ikiamini inaondoka na pointi tatu, Paul Peter aliyewahi kucheza timu hiyo aliisawazishia JKT dakika ya 90+2.
Paul Peter aliyewahi kuanzia timu ya vijana ya Azam chini ya miaka 20, hadi kupandishwa kuchezea ya wakubwa, amekuwa ni muhimili mkubwa kwa kikosi hicho cha maafande msimu huu, akishirikiana na nyota, Valentino Mashaka na Salehe Karabaka.
Mshambuliaji huyo aliyepandishwa kuichezea Azam na aliyekuwa kocha wa kikosi hicho, Mromania Aristica Cioaba amechezea pia timu mbalimbali zikiwemo za Mugabe FC, KMC FC, maafande wa Tanzania Prisons na msimu uliopita alikuwa Dodoma Jiji.
Nyota huyo alijiunga na JKT, Julai 9, 2025, akitokea Dodoma Jiji, baada ya msimu wa 2024-2025, kufunga mabao manane ya Ligi Kuu, akiwa nafasi ya pili kwa wachezaji wazawa waliofunga mabao mengi, nyuma ya Clement Mzize wa Yanga aliyefunga 14.
Msimu huu wa 2025-2026, tayari Paul Peter ameifungia JKT mabao manane ya Ligi Kuu Bara akiongoza kwa timu hiyo, huku pia katika Kombe la CRDB akiwa pia ndiye kinara akiwa ameshafunga matano, sawa na mshambuliaji wa Dodoma Jiji, Yassin Mgaza.
JKT TZ 1-1 Namungo FC
Hii ni mechi nyingine iliyoiokoa JKT Tanzania na kichapo nyumbani kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, Mbweni, baada ya Namungo FC kupata bao la dakika ya 39, kupitia Ali Salehe Machupa kisha, Salehe Karabaka akaisawazishia dakika ya 90.
Katika mechi hiyo iliyopigwa Oktoba 19, 2025, Karabaka anayecheza JKT Tanzania kwa mkopo akitokea Simba, alilifunga bao hilo na kuyeyusha ndoto za Namungo FC aliyowahi kuichezea msimu wa 2024-2025, za kuondoka na pointi tatu muhimu ugenini.
Karabaka aliyeichezea Namungo FC msimu wa 2024-2025, kwa mkopo akitokea pia Simba, aliifungia timu hiyo mabao mawili ya Ligi Kuu Bara, ingawa hadi sasa akiwa na JKT ameshaifungia mabao manane sawa na mshambuliaji nyota mwenzake, Paul Peter.
Mbeya City 2-2 JKT TZ
Katika mechi hii iliyopigwa kwenye Uwanja wa KMC Complex, Mwenge, jijini, Dar es Salaam, Oktoba 24, 2025, ilikuwa ni ya piga nikupige kati ya miamba hiyo na Mbeya City ilitangulia kupata bao kupitia kwa Hamad Majimengi dakika ya 14.
Hata hivyo, JKT ilisawazisha dakika ya 62, kupitia kwa Paul Peter kisha, Vitalis Mayanga akaiandikia Mbeya City bao la pili dakika ya 74, huku mwokozi wa kikosi cha maafande akiwa ni Salehe Karabaka aliyeiokoa na kichapo dakika ya 90+4.
Namungo FC 2-2 JKT TZ
Wakati Namungo FC 'Wauaji wa Kusini', ikiamini inaondoka na pointi tatu muhimu, ghafla ilijikuta ikiangukia pua dakika za mwishoni na kulazimishwa sare ya kufungana mabao 2-2, dhidi ya kikosi cha maafande wa JKT Tanzania, Aprili 4, 2026.
Katika mechi hiyo, Namungo ilitangulia kupata mabao hayo mawili yakifungwa na Jacob Masawe dakika ya 25 na Herbert Lukindo dakika ya 63, kisha JKT kusawazisha yote yakifungwa na Salehe Karabaka dakika ya 66 na Valentino Mashaka dakika ya 90+2.
JKT TZ 2-2 Fountain Gate
Miongoni mwa mechi zilizokuwa na mvuto zaidi msimu huu, hutoacha kuitaja ya JKT Tanzania dhidi ya Fountain Gate iliyopigwa Mei 21, 2026, kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, Mbweni na kuisha kwa sare ya mabao 2-2.
Katika mechi hiyo, ukiachana na Fountain Gate kutangulia kufunga mabao yote mawili na JKT Tanzania kuyasawazisha, jambo lililoteka hisia za mashabiki wengi wa soka hapa nchini ni bao lililofungwa na nyota wa kikosi hicho, Paul Peter.
Bao hilo lilikuwa ni la pili la kuchomoa kwa JKT Tanzania alilofunga dakika ya 86 kwa staili ya tiki-taka na kuteka hisia za mashabiki wa soka, huku likitabiriwa huenda likaingia katika tuzo za kuwania bao bora la msimu huu.
Mechi hiyo ya Mei 21, 2026, Fountain Gate ilianza kupata mabao hayo mawili kupitia kwa Juma Issa Abushiri dakika ya 3 na Ismail Aziz Kader dakika ya 45, huku yale ya JKT yakifungwa na Salehe Karabaka dakika ya 54 na Paul Peter dakika ya 86.
Mjadala wa bao bora la msimu huu, ulikuwa kwa kiungo mshambuliaji wa Simba, Clatous Chama alilolifunga katika mechi ya 'Kariakoo Derby', dhidi ya Yanga, iliyopigwa pia kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, Mei 3, 2026.
Katika mechi hiyo ya Mei 3, 2026, Chama alilifunga bao hilo kwa staili pia ya tiki-taka dakika ya 10, baada ya Libasse Gueye kuifungia Simba dakika ya 2, kisha, Prince Dube dakika ya 17 na Bakari Mwamnyeto dakika ya 50, wakaifungia Yanga.
Katika mechi hizo saba ambazo zimeiepusha JKT Tanzania na kichapo, imeshinda moja tu na kutoka sare sita na ni sawa na kukusanya jumla ya pointi tisa kati ya 21, ilizopaswa kuzipata msimu huu katika Ligi Kuu Bara ikiwa ingeshinda yote.