Mechi 5 zitakavyoamua vita ya Arsenal, Man City, Liverpool England
Muktasari:
- Miamba hiyo inayonolewa na Mikel Arteta ilishinda 1-0 uwanjani Emirates dhidi ya Crystal Palace, matokeo ambayo yalikuwa matamu kwao baada ya wapinzani wao kwenye mbio za ubingwa huo, Manchester City kuchapwa ugenini Villa Park mbele ya Aston Villa.
LONDON, ENGLAND: WIKIENDI ilikuwa tamu kwa Arsenal ilipofufua matumaini yao ya kunyakua taji la Ligi Kuu England kwa mara ya kwanza tangu 2004.
Miamba hiyo inayonolewa na Mikel Arteta ilishinda 1-0 uwanjani Emirates dhidi ya Crystal Palace, matokeo ambayo yalikuwa matamu kwao baada ya wapinzani wao kwenye mbio za ubingwa huo, Manchester City kuchapwa ugenini Villa Park mbele ya Aston Villa.
Eberechi Eze aliifungia bao pekee Arsenal na kuibwaga timu yake ya zamani. Mechi hiyo ilishuhudiwa pia Arsenal ikicheza bila ya kuruhusu bao kwenye nyavu zao, ambapo hadi sasa imefungwa mabao matatu tu, ikijibainisha kama moja ya timu zenye beki imara kwenye Ligi Kuu England.
Man City ya straika Erling Haaland ilichapwa 1-0 na Aston Villa, shukrani kwa bao la Matty Cash, wakati mabingwa watetezi Liverpool, nao walikumbana na kipigo kutoka kwa Brentford.
Arsenal na Man City zilishuka uwanjani Jumapili zikitambua wazi umuhimu wa kutumia fursa ya kuweka pengo la pointi baada ya Liverpool kuchapwa 3-2 na Brentford.
Kutokana na hilo, mechi tano zijazo kwa kila timu zitakuwa muhimu katika vita hiyo ya kusaka ubingwa kati ya sasa hadi kufikia kipindi cha sikukuu za mwisho wa mwaka.
Hali itakavyokuwa kwa mechi zijazo baina ya Arsenal, Man City na Liverpool katika mchakamchaka wa kuwania ubingwa wa Ligi Kuu England.
Arsenal
-Burnley (ugenini)
-Sunderland (ugenini)
-Tottenham (nyumbani)
-Chelsea (ugenini)
-Brentford (nyumbani)
Arsenal itaanza Novemba kwa mechi mbili za ugenini dhidi ya timu zilizopanda daraja. Hata hivyo, mechi hizo hazitakuwa mchekea kwao maana Sunderland ipo kwenye kiwango kizuri sana.
Kisha Arsenal itakuwa na kipute cha North London derby, japo imekuwa na rekodi nzuri kwenye mechi zake dhidi ya Tottenham Hotspur. Baada ya hapo itakabiliana na Chelsea ugenini, mechi ambayo inatazamiwa kuwa na upinzani mkali kwelikweli kabla ya kumaliza na Brentford.
Ukiweka kando mechi hizo za Ligi Kuu England, Arsenal itakuwa bize kwenye michuano mingine, Kombe la Ligi na Ligi ya Mabingwa Ulaya. Itakutana na Bayern Munich katikati ya mchezo wa Spurs na Chelsea.
Man City
-Bournemouth (nyumbani)
-Liverpool (nyumbani)
-Newcastle (ugenini)
-Leeds United (nyumbani)
-Fulham (ugenini)
Man City mechi zao mbili zijazo kwenye Ligi Kuu England itacheza dhidi ya timu zinazowania nafasi kwenye Top Four, ambapo Bournemouth inayoshika nafasi ya pili itakuwa na shughuli pevu ya kuwakabili vijana hao wa Pep Guardiola.
Kisha itachuana na Liverpool katika mechi inayotarajiwa kuwa na upinzani mkali. Mechi ya ugenini dhidi ya Newcastle United mara zote imekuwa ngumu na baada ya hapo, itakipiga na Leeds United nyumbani na Fulham ugenini. Ratiba hiyo inaonekana kuwa ngumu kwelikweli kwa Man City kutokana na mwenendo wao.
Man City inakabiliwa pia na mechi za michuano mingine, ambapo huko kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya, itakuwa na kibarua cha kuzikabili Borussia Dortmund na Bayer Leverkusen na hivyo kumfanya kocha Guardiola kukuna kichwa kutafuta namna ya kutoboa.
Liverpool
-Aston Villa (nyumbani)
-Man City (ugenini)
-Nottingham Forest (nyumbani)
-West Ham (ugenini)
-Sunderland (nyumbani)
Mambo yataendelea kuwa magumu Liverpool kabla ya kuwa mepesi. Mechi ijayo, Liverpool mechi ijayo itakabiliana na Aston Villa, ambayo imeshinda mechi nne zilizopita za ligi, wakati Man City itahitaji kupata ushindi kabla ya kwenda mapumziko ya ligi kupisha mechi za kimataifa.
Liverpool ya kocha Arne Slot baada ya mechi hizo mbili, itakabiliana na Nottingham Forest na kisha West Ham United, ambazo kwenye katarasi zinaonekana kuwa nyepesi zitakazoipa Liverpool ahueni kiasi.
Lakini, shida ni kwamba Liverpool inakabiliwa na mechi za michuano mingine, ikiwamo ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, ambapo itaavana Real Madrid na PSV Eindhoven, ambazo zipo kwenye kiwango matata sana kwa siku za karibuni.