Mchepuko katikati ya ugomvi wa Nas na Jay Z

Muktasari:

  • Awali, Jay Z alikuwa shabiki mkubwa wa Nas baada ya kutoa albamu yake ya kwanza, Illmatic (1994) ila harakati za kuwania ufalme wa New York katika rap zikawafanya kuwa mahasimu wasiochaguliana maneno. 

BAADA ya kufariki kwa Tupac na The Notorious B.I.G, vita vingine vya maneno vilivyoshuhudiwa katika ulimwengu wa Hip Hop ni kati ya Nas Escobar (50), na Jay Z (54), ingawa ugomvi wao haukufika hatua mbaya kama wenzao.

Awali, Jay Z alikuwa shabiki mkubwa wa Nas baada ya kutoa albamu yake ya kwanza, Illmatic (1994) ila harakati za kuwania ufalme wa New York katika rap zikawafanya kuwa mahasimu wasiochaguliana maneno. 

Katikati ya ugomvi wa Nas na Jay Z ulikuwepo mchepuko, naye ni Foxy Brown ambaye ni msanii wa pili wa kike wa Hip Hop duniani kwa albamu yake kushika namba moja chati ya Billboard 200.

Ugomvi kati yao ulianza baada ya Nas na wenzake kukubali kushiriki katika albamu ya kwanza ya Jay Z, Reasonable Doubt (1996), kisha lebo ya Jay Z, Roc-A-Fella Records italisaini kundi lao la The Firm.

Lakini Nas na wenzake walipiga chini kimya kimya makubaliano hayo na kwenda kusaini Aftermath Entertainment ya Dr. Dre na kutoa albamu yao ya pekee, The Firm (1997) iliyokamata nafasi za juu katika chati ya Billboard 200.

Hatua hiyo ilichochea uhasama na matusi, walishambuliana katika nyimbo zao na mahojiano mbalimbali. Baadhi ya wasanii wa New York kama Jadakiss, DMX pamoja na Nas walimshambulia Jay Z ambaye aliamua kujibu.

Jay Z alimchana Nas kupitia wimbo ‘Takeover’ kutoka katika albamu yake ya sita, The Blueprint (2001), wimbo huo uliotengenezwa na Kanye West uliponda kipaji cha Nas na kusema nyimbo zake zinafaa kutupwa na kuhoji heshima ya mtaa aliyopewa.

“Kila mmoja anataka kuheshimiwa hata kama sisi sio marafiki lakini tunatakiwa kuheshimiana, na nilihisi nilikuwa nikikosewa heshima nao, kwa hiyo nilitaka kuwaonyesha,” alisema Jay Z.

Haikuchukua muda Nas akajibu kupitia wimbo wake, Ether (2001) ambapo alimchana Jay Z kwa madai kuwa anaogopa wanawake kutokana na kunyanyaswa akiwa mdogo au alikuwa na tabia ambazo sio za kiume.

Hatua hiyo iliwasha moto kwa Jay Z ambaye alijibu hilo kwa freestyle ya wimbo ‘Supa Ugly’ uliokuja kuwekwa katika albamu yake ya live, Unplugged (2001), humo Jay Z alidai kuwa alikuwa na uhusiano na mzazi mwenzie na Nas!

Mei mwaka huu mwanzilishi mwenza wa Roc-A-Fella, Kareem ‘Biggs’ Burke akiongea na podcast ya Moguls In The Making, alisema wimbo huo wa Jay Z ulikuwa na maneno makali sana na hakuupenda kabisa.

Hatimaye ugomvi wa wawili hao ulikuja kumalizika na kufikia Aprili 2013, Nas na Jay Z wakapanda jukwaani pamoja katika tamasha la Coachella na kutumbiza nyimbo mbili ambazo ni Dead Presidents (1996) na Where I’m From (1997).

Ikumbukwe ugomvi wa Nas na Jay Z uligonga vichwa vya habari baada ya kumalizika ule wa wababe wawili wa East Coast na West Coast, Tupac na Notorious B.I.G kufuatia vifo vyao kati ya mwaka 1996 na 1997.

Tupac mzaliwa wa New York aliwakilisha East Coast baada ya kusaini Death Row Records yenye makao Los Angeles, mara nyingi alirushiana maneno na wenyeji wa New York, B.I.G na Diddy kutoka West Coast akiwakilisha Bad Boy Records ya New York.

Sasa mwaka 1996 baada ya Foxy Brown kusaini Def Jam Recordings, alikuwa na ukaribu na Jay Z ambaye alisikika katika wimbo yake ‘I’ll Be’ kutoka katika albamu yake ya kwanza, I’ll Na Na (1996) ambayo ilishirikisha wakali wengine kama Ll Cool J, Case na kadhalika.

Ukaribu wa Foxy Brown na Jay Z ukaibuwa tetesi kuwa wawili hao ni wapenzi, kipindi hicho bado Jay Z alikuwa hajakutana na Beyonce Knowles aliyekuwa akitamba na kundi la Destiny’s Child lililoanzishwa 1990.

Wakati huo Foxy Brown alikuwa mwanachama wa kundi kubwa la Hip Hop, The Firm akiwa na Nas, AZ na Cormega, hivyo Foxy pia alikuwa na ukaribu na Nas ambaye walishirikiana katika albamu ya kwanza ya kundi lao, The Firm (1997).

“Ni mengi watu hawajui, ilikuwa ni kama kuwa na mume na mchepuko na wote walikuwa wanafahamiana,” alisema Foxy Brown mwaka 2013 katika mahojiano na Shade 45 Radio pindi alipoulizwa kuhusu kuwa na uhusiano na Nas na Jay Z. 

Hata hivyo, Jay Z kupitia wimbo wake ‘Picasso Baby’ kutoka katika albamu yake ya 12, Magna Carta Holy Grail (2013) anakanusha madai ya kuwa na uhusiano na Foxy Brown ikiwa ni miaka 17 tangu hilo kuchukua nafasi.

Katika mahojiano yake na kipindi cha RapFix Live cha MTV mwaka 2013, Foxy Brown alishangazwa na kitendo cha Jay Z kuamua kujibu tetesi hizo baada ya miaka 17.

“Tunajua jinsi gani hii biashara inavyoenda, tunakaa nyuma na kuzicheka tetesi hizo, nadhani alianza kuhisi msukumo wa kufanya hivyo kwa sababu watu walianza kutaja umri wangu, miaka 16 wakati ule,” alisema Fox Brown.