Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mbao ina dili zake za kijanja nyie!

ITAKAPOSHUKA uwanjani Kirumba kesho Jumatano kuvaana na Allianze FC katika ‘Debi’ jipya la Mwanza, Mbao FC pia itakuwa inauanza msimu wa tatu mfululizo kwao kushiriki Ligi Kuu Bara huku kwa wenzao ikiwa ndio mara ya kwanza.

Pamoja na kuzichachafya klabu kongwe za Simba na Yanga, lakini hiyo misimu miwili ya awali Mbao ilipitia changamoto nyingi ikiwamo kupigania kutoshuka daraja, lakini sasa inasema imeshapata uzoefu. Mbao ilipanda msimu wa 2016/17 kutoka Kundi C la Ligi Daraja la Kwanza baada ya Geita Gold Sport kushushwa kwa tuhuma za kupanga matokeo.

Kwa misimu miwili ya kwanza, ilifundishwa na Mrundi Ettiene Ndayiragije aliyeipandisha. Safari hii ipo chini ya beki wa zamani wa Simba, Amri Said ‘Jap Stam’, aliyempokea Fulgence Novatus aliyepambana kuinusuru isishuke baada ya kuachwa na Ndayiragije ambaye sasa yupo KMC. Mwanaspoti limezungumza Stam aliyepangiwa nyumba maeneo ya Kapripointi wanakoishi vigogo wenye pesa zao na ndipo ilipo pia Ikulu ndogo ya Rais John Magufuli na kocha huyo ameweka wazi mambo kadhaa.

AGOMEA KUSHUKA

Huenda sasa Mbao imepata mwarobaini wa lile balaa la kunusurika kushuka daraja. Kocha Stam kawaambia wachezaji wake hana msamiati wa neno kushindwa, anasema anachotaka ni ushindi tu kama si hivyo basi sare. Sasa hapo presha ya kushuka daraja itakujaje?

“Nimekuja Mbao kufanya kazi na kazi yangu ni kuipa timu matokeo mazuri. Hii ni kuanzia mechi namba moja, hatupaswi kusubiri dakika za mwishoni. Biashara asubuhi,” anasema.

Anaamini ushirikiano, kujituma na kujitambua kwa pande zote nne; benchi la ufundi, wachezaji, viongozi na mashabiki, ndiyo njia pekee ya mafanikio klabuni.

USAJILI

Stam mwenye Leseni Daraja B ya ukocha ya Shirikisho la Soka la Afrika (CAF), ameridhishwa na usajili walioufanya akisema umezingatia mapendekezo yake.

“Bahati nzuri nimelisimamia hilo na wachezaji wote wapo wakisubiri ligi. Tumeshafanya mazoezi na timu ipo vizuri,” anasema.

UBINGWA

“Ubingwa? Sijui tutaona itakavyokuwa kama tutapata bahati hiyo, lakini lengo letu ni kushinda mechi nyingi kadiri itakavyowezekana kama si zote, hilo la ubingwa litakuja lenyewe huko mbele,” anasema. Anasema anajua watacheza ligi kuu na pia Kombe la FA na kote anataka timu ishinde mechi zake kwanza halafu mengine yafuate.

“Sitaki kuzungumzia ubingwa sasa, nataka kikosi kiwe cha ushindani na hayo mengine tutayajua baadaye,” aliongeza Stam aliyetumia mechi kadhaa za kirafiki kukipima kikosi chake.

Katika baadhi ya mechi hizo, walizishinda Biashara United (1-0), Kagera Sugar (2-0), Kahama Combine (3-1) na Masumbwe Warriors (1-0).

NI MBAO MPYA

Mbao imeondokewa na nyota kadhaa walioisaidia misimu miwili iliyopita licha ya Stam alikuwa anawahitaji. Nyota hao ni Yusuph Ndikumana na James Msuva (wameenda KMC), Habib Kiyombo na Boniface Maganga (wametua Singida United) na kipa Metacha Mnata aliyesajiliwa Prisons.

“Ndio maana nipo hapa. Mimi ni kocha, nimeandaa wengine na hii ni Mbao mpya, inakuja kivingine, kiushindani zaidi.”

HANA HOFU NA DEBI

Achana na debi la zile timu za Kariakoo; Simba na Yanga au lile la hapa Mwanza la zamani, Pamba na Toto. Jiji la Mwanza sasa lina debi la zama hizi za 4G, Mbao vs Alliance iliyopanda daraja.

Stam anasema anawafahamu wapinzani wao kwa jinsi walivyojipanga kuikamata Mwanza, lakini kaapa lazima Mbao ishinde.

KIKOSI

Kikosi chake ni Hashim Mussa, Bruno Thomas, Kelvin Igendelezi, Mussa Mussa, Vicent Philipo, Andrew James, David Mwasa, Amos Charles, Hamim Abdul, Aboubakari Mfaume, Hassan Khamis, Peter Mwangosi, Rolland Msonjo, Yusuph Amos na Sylvestre Chitembe.

Wengine ni Ibrahim Njohole, Ally Mussa, Hussein Kasanga, Ismail Ally, Abdulkarim Segeja, Emmanuel Mtumbuka, Alawi Janja, Aman Malunde, Hajji Mussa, Pastory Athanas, Rajesh Kotecha, Evaligestus Mujwahuki, Helbert Lukindo, Raphael Siame, Ndaki Robert, Rayson Okelo, Said Khamis na Hassan Jafari.