MATEI: Mwamba Prisons aliyeinusuru isishuke

Muktasari:
- Katika mahojiano baina yake na Mwanaspoti Matei anasema kipindi anachezea timu iliwahi kushuka daraja kabisa na pia kuna msimu iliponea chupuchupu kucheza Ligi ya Championship kipindi hicho ikiitwa Daraja la Kwanza.
JAPOKUWA katibu wa Tanzania Prisons, John Matei hakuanza kufanya majukumu hayo mwanzoni mwa msimu huu 2024/25, mchango wake umekuwa mkubwa kwa wachezaji kutokana na uzoefu wake wa kukichezea kikosi hicho miaka ya nyuma.
Katika mahojiano baina yake na Mwanaspoti Matei anasema kipindi anachezea timu iliwahi kushuka daraja kabisa na pia kuna msimu iliponea chupuchupu kucheza Ligi ya Championship kipindi hicho ikiitwa Daraja la Kwanza.
“Nimekuwa nikitumia mfano huo kuwapa moyo wachezaji kuendelea kupambana, angalau tupo nafasi ambayo inatupa nguvu ya kusalia Ligi Kuu ingawa bado kazi ni ngumu,” anasema.
CHANGAMOTO YA MSIMU HUU
Miongoni mwa vitu vilivyochangia kwa Prisons kufanya vibaya anavitaja ni wachezaji waandamizi wengi walikuwa majeruhi kama Samson Mbangula, Nurdin Chona, Jeremiah Juma na wengine.
“Hilo limetupa picha ya msimu ujao kusajili wachezaji ambao wataendana na falsafa ya timu yetu, ingawa soka linabadilika lile pira gwaride linapotea, ila tutazingatia vitu muhimu zaidi ambavyo vitairejesha ile Tanzania Prisons ngumu kufungika,” anasema.
Anasema kitendo cha kuipambania timu isishuke daraja siyo kigeni kwake imewahi kutokea wakati anacheza msimu wa 2014/15: “Nakumbuka zilibakia mechi nane, timu ilikuwa pabaya. Katika hizo tukashinda tano, sare mbili ikashuka Ruvu Shooting baada ya kufungwa na Stand United, kocha wetu alikuwa Mbwana Makata.”
Anaongeza: “Mchango wangu kama katibu na mchezaji wa zamani wa timu niliutumia uzoefu wa nyakati nilizowahi kuzipitia ili kuwapa moyo wachezaji wa kupambana kwa ajili ya timu na kuheshimisha ama kulinda CV zao.”
Katibu huyo wakati anacheza alijiunga na Prisons msimu wa 2008/2009, anasema kama kuna tukio analikumbuka la kuumiza katika soka ni 2009/10 timu ilishuka. “Maumivu yake hayasimuliki lakini haikutukatisha tamaa tukapanda tena 2011/12, ndiyo maana nilikuwa nasema na wachezaji kwamba ili mladi mbele yao kuna nafasi basi wanapaswa kupambana hadi tone la mwisho.”
Anasema wakati anajiunga na timu hiyo ilikuwa bora na kocha alikuwa James Nestory ambaye ni askari Magereza ilikuwa na wachezaji baadhi yao kama Oswald Morris, Yona Ndabila, Fred Chudu, Silvester Kamtande, Ismail Suleiman, Misango Magai, Mbega Daffah.
“Ambao nilisajiliwa nao ni Lugano Mwangama, Laurean Mpalile, Nelson Kimati, Sudi Ahadi na wengine wengi, hivyo tukawa tunapata uzoefu kutoka kwa wachezaji ambao tumewakuta ndani ya timu, tulihamasika kuwa wazalendo na kucheza hilo pira gwaride kwa kufanya mazoezi ya pumzi na fiziki,” anasema.
Anasema kupitia soka alifanikiwa kupata ajira ya askari Magereza, kitu ambacho ni kikubwa katika maisha yake na pia alifanikiwa kusafiri nchi mbili Libya na Sudan.
“Cheo changu kwa sasa ni mkaguzi msaidizi wa Jeshi la Magereza (Assistant Inspector of Prisons) kimtaani ni nyota moja,”anasema.
YANGA ILIWAHI KUMTAKA
“Nakumbuka wakati Yanga wanamhitaji kipa Nelson Kimati walinihitaji na mimi, lakini viongozi wa Prisons hawakuniruhusu kuondoka,” amesema Matei ambaye mechi yake ya kwanza ya Ligi Kuu alicheza dhidi ya Yanga Uwanja wa Uhuru kwa kiwango cha kuvutia, kilichoifanya timu pinzani kutamani huduma yake.
KUPANDA KWA MBEYA CITY
Matei anatoa pongezi kwa Mbeya City kurejea tena Ligi Kuu Bara akiamini kwamba italeta ushindani mkubwa baina yao na kuwapa burudani mashabiki wa mkoa huo.
“Mkoa sasa utachangamka, dabi itakuwa nzuri zaidi maana ushindani wa Ligi Kuu umeongezeka tofauti na misimu iliyopita,” anasema katibu huyo anayekumbuka mechi ya dabi waliyoifunga City bao 1-0 mfungaji alikuwa Lugano Mwangama kwa penalti iliyosababishwa na Juma Nyosso, hivyo wakanusurika kushuka.
KIKOSI BORA
Anataja kikosi chake bora kipindi anacheza ni Juma Kaseja, Sudi Ahadi, Laurean Mpalile, George Owino, Kelvin Yondani, Athuman Chuji, Fredy Chudu, Mwinyi Kazimoto, Felix Sunzu, Haruna Moshi na Kigi Makasi.
“Kwangu mimi hao jamaa walikuwa ni hatari na vipaji vya juu ingawa wapo wengi ninaowakubali kwa sasa kama Najim Mussa, Geofrey Julias kutoka Namungo,kiungo wa Kagera Sugar Geofrey Manyasi na wachezaji wote wa Prisons wamefanya kazi kubwa ya kuipambania timu bila kusahau John Bocco kacheza kwa kiwango cha juu kwa muda mrefu,” anasema Matei ambaye anasema ndani ya kikosi chao kuna nyota wa kigeni kama Amade Momade kutoka Msumbiji na msimu uliyopita walikuwa na oshua Nyantini kutoka Kenya.
Anasema msimu wake bora ni wa 2009/10 aliyofunga mabao matano japokuwa timu ilikuwa inapambana kujikwamua na kushuka daraja: “Mpira wa miguu ni ajira ninawashauri wachezaji kuuheshimu ili kubadilisha maisha yao, wakifanya kwa dhati watafanikiwa”.