Mastaa wanaoishi kwa wasiwasi Simba, Yanga, Azam

WAPO baadhi ya mastaa wa Simba, Yanga na Azam FC wanaoishi maisha ya wasiwasi, kutokana na kutokuwa na uhakika wa namba kwenye vikosi vyao na bado hawajaeleweka kwa mashabiki ambao walitarajia kuona vitu vikubwa kutoka kwao.

Siyo wachezaji wabaya, ila kuna wakati msimu unaweza kumkataa mchezaji na akitimkia sehemu nyingine anaweza akaonyesha kiwango kikubwa.

Hilo aliwahi kulizungumzia Kocha wa Kagera Sugar, Francis Baraza akisema kuna wakati mchezaji akipewa nafasi na akashindwa kuonyesha anapaswa kutolewa kwa mkopo ili kuangalia makocha wengine wanamtumiaje.

“Hadi mchezaji anasajiliwa kwenye timu ni muhimu, lakini binadamu yapo mengi wanayoweza kuyapitia, kama kocha lazima ukae naye chini umpe nafasi ya kucheza mara nyingi ikishindikana unamtoa kwa mkopo ambako lazima umfuatilie anavyotumiwa na kocha mwenzako, ukiona kafanikiwa basi unamrejesha,” anasema.

Mtazamo huo unaaminiwa pia na kocha Msaidizi wa Ihefu, Zuber Katwila anayesema hakuna mchezaji mbaya duniani isipokuwa kila kocha ana jicho lake la kiufundi la namna ya kumtumia.

Kutokana na hilo, Mwanaspoti linakuchambulia mastaa ambao awali walikuwa na viwango vya juu, Simba, Yanga na Azam FC ila kwa sasa wanajikuta hawana uhakika wa namba, wakati mwingine hata wanapopewa dakika chache wanashindwa kutoa kilichotarajiwa.

Endapo kama wataendelea na viwango wanavyoonyesha sasa hadi utakapofunguliwa usajili wa dirisha dogo, nafasi ya kuondoka kwao ndani ya vikosi hivyo ni kubwa kuliko kusalia, jambo ambalo wengi linawapa wasiwasi.


HERITIER MAKAMBO-YANGA

Hakuna namna Kocha Nasreddine Nabi, anaweza akamuweka benchi Fiston Mayele aliye na mabao matatu ya Ligi Kuu na saba ya Ligi ya Mabingwa Afrika, wakati huohuo Makambo bado hajaanza kucheka na nyavu licha ya kupewa nafasi ya kucheza.

Mwaka 2021 wakati anarejeshwa Yanga akitokea Horoya ambako ilimuuza 2019, mashabiki walitarajia kuona maajabu yake, lakini mambo yanaonekana kwenda sivyo ndivyo, jambo lililosababisha kuwepo na fununu za kuachwa kuanzia usajili wa dirisha kubwa hadi sasa, hali inayosababisha wasiwasi kwa staa huyo.


JESUS MOLOKO-YANGA

Licha ya kuanza vizuri msimu huu, bado anaendelea kutazamwa kama atakuwa na mwendelezo wa kiwango chake, vinginevyo anaweza akatoa nafasi ya kurejeshwa Yacouba Sogne ambaye sababu iliyofanya atemwe ni kusumbuliwa kwa majeraha kwa muda mrefu, jamaa kapona na anapiga tizi hatari. Mbali na Yacouba pia yupo Tuisila Kisinda alirejea kwenye kikosi hicho msimu huu akitokea RS Berkane ya Morocco ambaye naye anazidi kuongeza ushindani wa nafasi baina ya nyota hao.


MOHAMED QUATTARA-SIMBA

Anahitaji kuonyesha ufundi wa ziada ili kuvunja pacha iliyokuwepo kati ya Henock Inonga na Joash Onyango, huku Kennedy Juma akiwa anacheza mara moja moja sana, vinginevyo Onyango akirejesha makali yake, maisha yake yanaweza yakawa mafupi ndani ya timu hiyo.


DEJAN GEORGIJEVIC-SIMBA

Straika huyu raia wa Serbia tayari ameshajitoa mwenyewe Simba baada ya kudai klabu imekiuka mkataba.

Hata hivyo, suala lake bado halijamalizwana na anahesabika ni mchezaj wa Simba.

Dejan mwenye bao moja la Ligi Kuu Bara alikuwa na kazi ya kufunga ili kuwapa raha mashabiki, vinginevyo angekuwa kwenye wakati mgumu mbele ya Moses Phiri ambaye ana upepo wa kufunga ambapo anamiliki mabao manne ya Ligi Kuu na matatu ya Ligi ya Mabingwa Afrika.


NELSON OKWA-SIMBA

Jicho la kiufundi la aliyekuwa Kocha wa Simba, Zoran Maki liliona umuhimu wa Okwa kutumika kwenye kikosi chake, baada ya Juma Mgunda kufanya majukumu hayo kwa muda wakisaka kocha mpya, amemuona Augustine Okra anafaa kutumika mara kwa mara kikosini, mastaa hao ambao wanacheza kwa mara ya kwanza Ligi Kuu bado wanahitaji kuonyesha ufundi ili kuendelea kuaminika.


CLEOPHANCE MKANDALA-AZAM FC

Azam FC, ilimsajili kiungo Cleophance Mkandala kutoka Dodoma Jiji kutokana na uwezo wake, ila asipokaza kamba katika nafasi yake kuna viungo wengi akiwemo Mnigeria, Isah Ndala aliyetokea Rivers United na tayari ameonyesha kiwango cha juu.


EDWARD MANYAMA-AZAM FC

Tangu msimu uliopita alisajiliwa akitokea Ruvu Shooting, amekuwa na nafasi finyu ya kucheza na ana wasiwasi wa muda wowote anaweza akawa siyo sehemu ya kikosi hicho kutokana na Bruce Kangwa kuendelea kuonyesha ubora.


IBRAHIM AJIBU-AZAM FC

Wakati anaondoka Simba, ilionekana ameshindwa kuendana na presha na kasi ya wachezaji ambao walikuwa wanacheza nafasi yake, huku wengi waliamini angefanikiwa sana, lakini bado hajaonyesha kile alichotarajiwa hali ambayo inazidi kutia wasiwasi kwa nyota huyo aliyewahi kuzichezea Simba na Yanga.


ISMAIL AZIZ-AZAM FC

Msimu huu, hana nafasi kwenye kikosi cha kwanza cha Azam, licha ya kupata nafasi ya kwa msimu uliopita alishindwa kuonyesha kiwango bora.

Mambo yamezidi kuwa magumu zaidi kwake kwani hajaanza hata mechi moja ya ligi na mechi pekee aliyoonekana kuanza kwenye kikosi cha kwanza kwa msimu huu ni ile ya kirafiki dhidi ya Taifa Jang’ombe.

Naye ana kazi kubwa ya kufanya ili kubakia kwenye kikosi kuelekea dirisha dogo la Tanzania.