Mastaa waliozibeba timu Ligi Kuu Bara
Muktasari:
- Wachezaji hao wamekuwa nguzo muhimu kwa timu zao kupitia idadi kubwa ya mechi walizocheza, mabao waliyofunga, uwezo wa kuzuia mabao kwa mabeki na makipa pamoja na mchango wao wa moja kwa moja katika mafanikio ya timu.
WAKATI Ligi Kuu Bara ikielekea ukingoni huku kila timu ikiendelea na hesabu zake za kuhakikisha inamaliza salama msimu wa 2025/26, wapo wachezaji ambao wameonyesha kiwango cha juu, ubora wa kipekee na kuwa tegemeo kubwa katika vikosi vyao kutokana na mchango mkubwa walioutoa ndani ya uwanja.
Wachezaji hao wamekuwa nguzo muhimu kwa timu zao kupitia idadi kubwa ya mechi walizocheza, mabao waliyofunga, uwezo wa kuzuia mabao kwa mabeki na makipa pamoja na mchango wao wa moja kwa moja katika mafanikio ya timu.
Kwa sasa zimebaki mechi tano pekee kumalizika kwa msimu huu wa Ligi Kuu, ambapo Yanga inaendelea kusaka rekodi ya kutwaa ubingwa kwa msimu wa tano mfululizo huku Simba ikipambana kuvunja ukame wa mataji baada ya kukosa ubingwa kwa misimu minne mfululizo.
Yanga inaongoza msimamo wa ligi ikiwa na pointi 60, ikifuatiwa na Simba yenye pointi 58, Azam FC ikiwa nafasi ya tatu kwa pointi 52, Singida Black Stars ikijikusanyia pointi 41 huku JKT Tanzania ikiwa na pointi 38 na TRA United ikikamilisha orodha ya timu sita bora kwa pointi 37.
Upande wa mkiani mwa msimamo, KMC ndiyo inayoburuza mkia ikiwa na pointi tisa, Tanzania Prisons ikifuata kwa pointi 20, Mbeya City ikiwa na pointi 22, Namungo pointi 25 huku Mtibwa Sugar na Mashujaa zikiwa zimejikusanyia pointi 27 kila moja, hali inayofanya vita ya kusalia Ligi Kuu kuwa kali na yenye ushindani mkubwa. Pamoja na ushindani huo mkubwa unaoshuhudiwa msimu huu, wapo mastaa ambao wameendelea kung’ara katika timu zao kutokana na mchango wao binafsi, uwezo wao wa kiufundi na namna walivyozibeba timu zao katika nyakati muhimu, huku wakijitengenezea mazingira mazuri kuelekea dirisha lijalo la usajili.
Yona Amos (Pamba Jiji)
Tangu alipokuwa akikipiga katika kikosi cha Tanzania Prisons misimu miwili iliyopita, kipa Yona Amos ameendelea kuonyesha kiwango bora kilichozifanya timu mbalimbali, zikiwamo zile kubwa nchini, kuendelea kuvutiwa na huduma yake.
Kipa huyo wa kimataifa amekuwa na mwendelezo mzuri wa kiwango chake kwani hadi sasa ndiye kinara wa kuokoa hatari nyingi zaidi langoni baada ya kufanya hivyo mara 38 huku akifanikiwa kutoruhusu nyavu zake kutikiswa katika mechi saba.
Kutokana na uimara wake na mchango wake mkubwa ndani ya kikosi cha Pamba Jiji, ameisaidia timu hiyo kupata matokeo mazuri na kujikuta ikishika nafasi ya saba ikiwa na pointi 33 huku ikibaki na matumaini ya kumaliza msimu ndani ya nafasi nne za juu.
Mbali na Amos, mshambuliaji kutoka Kenya, Methew Tegisi, ni miongoni mwa nyota walioonyesha mchango mkubwa katika kikosi hicho baada ya kufunga mabao saba katika msimu wake wa kwanza kucheza soka la kulipwa nchini Tanzania.
Clatous Chama (Simba)
Kiungo mshambuliaji huyu kutoka Zambia hajawahi kuwachosha mashabiki wa soka kumtazama akiwa na mpira miguuni. Kipaji chake cha hali ya juu, ubunifu wake na uwezo wa kuamua matokeo ya mechi vimemfanya kuwa mmoja wa wachezaji wanaopendwa zaidi katika Ligi Kuu.
Tangu alipotua Simba, Chama amefanya mambo makubwa ikiwamo kusaidia timu hiyo kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu na kufika hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika. Msimu huu ameendelea kuwa muhimu katika kikosi hicho baada ya kufunga mabao nane, likiwamo bao lililozua gumzo kubwa mitandaoni dhidi ya watani wao wa jadi, Yanga. Mbali na Chama, Simba pia imekuwa ikinufaika na mchango wa Seleman Mwalimu ambaye ameleta utulivu katika safu ya ushambuliaji pamoja na Libase Gueye aliyefunga mabao sita. Aidha, mchango wa Elie Mpanzu umeendelea kuonekana katika maeneo mbalimbali ya uwanja kutokana na uwezo wake wa kufanya kazi kubwa kwa ajili ya timu.
Baraka Maranyingi (Mbeya City)
Licha ya Mbeya City kutokuwa na msimu mzuri kwa ujumla kutokana na matokeo yasiyoridhisha, jina la Baraka Maranyingi haliwezi kuachwa linapozungumziwa kikosi hicho.
Kiungo huyo amekuwa miongoni mwa wachezaji walioibeba timu hiyo mabegani kutokana na kujituma kwake na mchango mkubwa alioutoa. Maranyingi ndiye mchezaji aliyecheza mechi nyingi zaidi katika kikosi hicho, akihusika katika michezo 23 kati ya 25 iliyochezwa hadi sasa na kukosa mechi mbili pekee.
Katika michezo hiyo amefunga mabao mawili na kutoa pasi nne za mabao, takwimu zinazoonyesha namna alivyokuwa muhimu kwa timu. Sambamba na yeye, mshambuliaji Eliud Ambokile amekuwa sehemu ya nyota waliotoa mchango mkubwa baada ya kuongoza orodha ya wafungaji wa Mbeya City kwa mabao matano.
Kwa sasa timu hiyo inapambana kwa nguvu zote kuhakikisha inasalia Ligi Kuu baada ya kurejea msimu huu kutoka daraja la chini, huku dakika 450 zilizobaki zikitarajiwa kuamua hatma yao.
Maabad Maulid (Coastal Union)
Mshambuliaji huyu kutoka Zanzibar ameendelea kuthibitisha ubora wake tangu alipojiunga na Coastal Union misimu minne iliyopita. Kwa muda wote huo amekuwa akionyesha uwezo mkubwa wa kufunga mabao, kasi ya juu pamoja na mchango mkubwa kwa timu nzima.
Hadi sasa Maabad ndiye kinara wa mabao ndani ya kikosi hicho akiwa amefunga mabao sita na kutoa asisti nne huku akiendelea kujiimarisha kama mmoja wa wafungaji bora wa muda wote wa Coastal Union. Ikumbukwe kuwa alijiunga na timu hiyo akitokea KVZ ya Zanzibar baada ya kuwa mfungaji bora wa msimu wa 2021/22 kwa mabao 19.
Kiwango chake bora kimeendelea kuvutia macho ya timu mbalimbali zinazotamani kupata saini yake. Mbali na Maabad, winga Bakari Msimu naye ameonyesha kiwango kizuri kutokana na uwezo wake wa kutengeneza nafasi na kusaidia timu kufika fainali ya Kombe la Shirikisho la Tanzania (FA).
Feisal Salum (Azam FC)
Kiungo huyu wa kimataifa wa Tanzania ameendelea kuonyesha ubora uleule aliouonyesha akiwa Yanga. Tangu ajiunge na Azam FC amekuwa mhimili mkubwa wa mafanikio ya timu hiyo huku akiendelea kujiweka katika nafasi nzuri ya kuwa mmoja wa wachezaji bora wa msimu.
Hadi sasa Feisal Salum ‘Fei Toto’ ndiye kinara wa mabao katika Ligi Kuu akiwa amefunga mabao 14 na kutoa asisti nane. Takwimu hizo zimeisaidia Azam FC kubaki katika nafasi ya tatu ya msimamo huku zikiendelea kumfanya kuwa miongoni mwa wachezaji wanaotamaniwa zaidi nchini. Taarifa mbalimbali zimekuwa zikihusisha jina lake na uwezekano wa kurejea Yanga, ingawa hakuna taarifa rasmi zilizotolewa. Mbali na Fei Toto, mshambuliaji Idd Nado ameendelea kuwa muhimu katika kikosi hicho baada ya kufunga mabao nane na kuwa chaguo la mara kwa mara la makocha wote waliopitia Azam FC kutokana na uwezo wake mkubwa.
Djigui Diarra (Yanga)
Miongoni mwa wachezaji wanaopendwa zaidi na mashabiki wa Yanga ni kipa Djigui Diarra wa Mali ambaye kwa kiasi kikubwa amekuwa nguzo muhimu ya mafanikio ya timu hiyo. Tangu alipojiunga na Yanga misimu mitano iliyopita, ameonyesha kiwango cha hali ya juu na kuwa sehemu ya mafanikio makubwa ya timu hiyo. Mbali na kusaidia Yanga kutwaa mataji ya ndani kwa misimu minne mfululizo, Diarra pia amekuwa sehemu ya safari ya kihistoria ya timu hiyo kufika fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika na hatua za juu za michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Kwa mujibu wa takwimu za msimu huu, Diarra ndiye kinara wa mechi nyingi za kutoruhusu bao akiwa na ‘clean sheet’ 13, akifuatiwa na Mahamadou Camara wa Simba mwenye 12 na Aishi Manula mwenye 11 huku Jean Noel wa TRA United akiwa na 10. Mbali na Diarra, beki Ibrahim Abdullah ‘Bacca’ amekuwa na ubora katika safu ya ulinzi ya Yanga na kuvutia timu mbalimbali za ndani na nje ya nchi. Vilevile, kiungo mshambuliaji Allan Okello ameanza maisha kwa kasi kubwa baada ya kufunga mabao 11.
Ramadhan Salum ‘Chobwedo’ (TRA United)
Ingawa siyo kinara wa mabao wala asisti ndani ya kikosi cha TRA United, Ramadhan Salum ‘Chobwedo’ amekuwa mmoja wa wachezaji wenye mchango mkubwa zaidi kutokana na uwezo wake wa kutengeneza nafasi, kupiga chenga na kuwasumbua mabeki wa timu pinzani.
Nyota huyo aliyewahi kucheza KenGold ameendelea kuwa kivutio kikubwa katika Ligi Kuu kutokana na mtindo wake wa uchezaji unaowavutia mashabiki wengi. Hadi sasa amefunga mabao manne na kutoa asisti nne, takwimu zinazodhihirisha mchango wake katika mafanikio ya timu hiyo.
Kutokana na kiwango chake kizuri, Chobwedo amekuwa akitajwa kuwindwa na Simba kwa ajili ya msimu ujao, ingawa hakuna upande ambao umeweka wazi taarifa rasmi kuhusu suala hilo.
Ismail Aziz (Fountain Gate)
Mshambuliaji Ismail Aziz ameibuka kuwa mmoja wa wachezaji muhimu zaidi katika kikosi cha Fountain Gate kutokana na moyo wake wa kujituma, upambanaji na uwezo wa kuiongoza timu katika nyakati ngumu. Mchango wake umeisaidia Fountain Gate kuondoka katika maeneo hatarishi ya msimamo na kurejesha matumaini ya kubaki salama ndani ya Ligi Kuu.
Hadi sasa straika huyo amefunga mabao manne na kuhusika katika mabao mengine matatu huku akionyesha kiwango kizuri na ushirikiano mkubwa na wachezaji wenzake akiwamo Juma Abushir na Henry David.
Kupitia juhudi zake binafsi na mchango wake wa moja kwa moja katika ushindi wa timu, Ismail Aziz ameendelea kujijengea jina kama mmoja wa nyota wanaostahili kuangaliwa kwa karibu katika hatua za mwisho za msimu huu wa Ligi Kuu Bara.