Mastaa waliorejea Bara na kuchemka
KIWANGO walichokionyesha baadhi ya mastaa wa Ligi Kuu Bara, kiliwapa dili za kucheza nje ya nchi, lakini baada ya kurejea tena Bongo, hawajaweza kucheza kwa mafanikio kama mwanzo.
Clatous Chama wa Simba, hawezi kuingia katika orodha hii kwani ameendelea kufanya makubwa hivi sasa katika moto ule ule aliokuwa nao alipoondoka kwenda RS Berkane ya Morocco, ilimchukua muda mchache kurejea kwenye makali yake na akawa msaada kwa timu yake akamaliza na asisti 15 na mabao manne msimu uliopita wa 2022-23.
Mwisho wa msimu wa 2021/22 ambao ndio aliondoka kwenda kujiunga na Berkane, Chama alikuwa kinara wa asisti 15 na alifunga mabao manane kwenye Ligi Kuu.
Lakini Chama ni kati ya nyota wa kipekee waliorudi na makali yale yale. Mwanaspoti, linakuchambulia mastaa ambao baada ya kurejea kutoka nje, hawakuweza kufanya vizuri, kama ilivyotarajiwa.
HERITIER MAKAMBO
Wakati anaondoka Yanga 2019/20 kwenda kujiunga na Horoya ya Guinea alikuwa amefunga mabao 17, hilo lilifanya mashabiki wawe wanakumbuka huduma yake, lakini aliporejea 2021/22 hakuwa kwenye kiwango kilichotarajiwa akaonyeshwa mlango wa kutokea na sasa anacheza klabu ya Al Murooj ya Libya.
THOMAS ULIMWENGU - SINGIDA
Mshambuliaji Thomas Ulimwengu, aliporejea kucheza soka la Tanzania, alitarajiwa kutisha kutokana na uzoefu wake wa kuzichezea timu za nje ikiwamo TP Mazembe. Hata hivyo, mambo yamekuwa sivyo ndivyo na hajawa mchezaji wa kutegemewa katika kikosi cha kwanza cha Singida Fountain Gate.
Alikopita Ulimwengu ni Tanzania Soccer Academy (2008), Moro United (2009/10 kwa mkopo), Athletic FC (2010/2011), TP Mazembe (2011-2016), AFC Eskilstuna (2017), Sloboda Tuzla (2017/18), Al-Hilal Club (2018), JS Saoura (2019), TP Mazembe (2020-2023) na sasa Singida Fountain Gate.
LUIS MIQUISSONE - SIMBA
Msimu wake wa kwanza kuichezea Simba (2020/21), akitokea UD Songo, alifanya vizuri na alimaliza na mabao 10 na asisti 9 na kilichoishawishi Al Ahly ya Misri kumnunua ni baada ya kuwafunga bonge la bao katika mechi ya CAF kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa.
Aliporejea kwa mara ya pili Simba (2023/24) akitokea Abha (kwa mkopo), hajawa kwenye kiwango kizuri, tofauti na matarajio ya mashabiki na hajawa mchezaji tegemeo kikosini.
SHABAN CHILUNDA - KMC
Kiwango alichokuwa amerejea nacho Shaban Chilunda, Azam FC kwa mara ya pili, akitokea klabu ya Tenerife ya Hispania alikoenda kwa mkopo msimu wa 2018/19 na kupita Izarra (2019, kwa mkopo) na Moghreb Tetouan, hakikuwa cha ushindani.
Simba baada ya kumsajili msimu huu, alishindwa kuonyesha ushindani, ikamtoa kwa mkopo dirisha dogo kwenda KMC.
YAHYA ZAYD - AZAM FC
Wakati anaondoka Azam FC 2018, kwenda kujiunga na Ismaily SC ya Misri, alikuwa na kiwango cha juu, baada ya kurejea kwenye kikosi hicho, kiwango chake hakijawa cha ushindani kama mwanzo, ingawa anapata nafasi ya kucheza.
TUISILA KISINDA - RS BERKANE
Winga wa zamani wa Yanga, wakati anajiunga na timu hiyo akitokea As Vita kiwango chake kilikuwa cha juu, kilichoishawishi RS Berkane ya Morocco kumnunua, baada ya kurejea Jangwani kwa mkopo 2023 hakuwa na kiwango cha kutisha hadi anaondoka.
ELIUD AMBOKILE - MBEYA CITY
2018/19 akiwa na Mbeya City, alimaliza akiwa na mabao 10 kwenye Ligi Kuu, kisha akaenda kujiunga na TP Mazembe ambako hakuwa anapata nafasi ya kucheza, ikamlazimu kuvunja mkataba kisha akajiunga na Nkana ya Zambia, nako hakucheza kwa ushindani.
Akarejea tena Mbeya City hadi akashuka nayo daraja na bado anaitumikia ikiwa Championship na alikuwa na haya ya kusema: “Baada ya kurejea Mbeya City, ikiwa Ligi Kuu nilipata majeraha, yaliyosababisha nisiwe nacheza mara kwa mara, ila najipanga nitarejea kwenye mstari.”
RAMADHAN SING’ANO - HURU
Tangu alipoondoka Azam na kwenda kujiunga na TP Mazembe mwaka 2020, hakuwa na nafasi kikosini, kisha akaondoka na kwenda Nkana na aliporejea Tanzania, hajaonekana tena uwanjani, lakini anafanya shughuli za kituo chake cha soka.
“Kwa sasa nina kituo cha soka, ila ipo siku nitarejea uwanjani, nilijipa muda wa kuweka sawa vitu vingine kwanza,” anasema.
HASSAN KESSY - NKANA
Baada ya kucheza kwa kiwango kikubwa Simba na Yanga, kisha 2020 akaenda kujiunga na Nkana ambako nako alionyesha kiwango cha juu. Kilichomfanya arejee nchini ni baada ya mlipuko wa ugonjwa wa Covid -19.
Akajiunga na Mtibwa (2021), KMC (2022) na sasa anacheza Dodoma Jiji, lakini kiwango chake ni cha kawaida siyo kama mwanzo ambapo alikuwa tishio.
WENGINE
Kipa David Kisu baada ya kutoka Gor Mahia ya Kenya na kujiunga na Azam kiwango chake kilishuka na sasa anaichezea Biashara United ya Championship. Pia beki Juma Abdul baada ya kuondoka Yanga na kwenda Indeni FC ya Zambia 2021, akarejea Singida FG ikiwa Championship, lakini haku-ng’aa.