MASTAA WALIOISHIA 'VYUMBANI' KWA MKAPA

Muktasari:

MOTO utawaka pale kwa Mkapa, wakati Simba ikiikaribisha Yanga kwenye mchezo wa Ligi Kuu Bara huku wakiwa na kumbukumbu ya sare ya bao 1-1 katika mchezo uliopita.

MOTO utawaka pale kwa Mkapa, wakati Simba ikiikaribisha Yanga kwenye mchezo wa Ligi Kuu Bara huku wakiwa na kumbukumbu ya sare ya bao 1-1 katika mchezo uliopita.

Huko mtaani tambo kibao kila mmoja akisifu kikosi chake huku wale wa Msimbazi wakidai kama kocha wa Yanga, Nasreddine Nabil atampanga beki, Abdallah Shaibu ‘Ninja’ eti ajiandae kula kadi nyekundu.Vipi kuhusu Thadeo Lwanga tungoje dakika 90.

Pamoja na tambo hizo za kila mmoja kuegemea upande wake, Mwanaspoti halipo nyuma kukuletea mambo kadhaa kuelekea derby hii na hawa hapa ni baadhi ya mastaa waliokula umeme katika derby za hivi karibuni.


HASSAN KESSY -2018

Huyu ndiye mchezaji wa mwisho kula umeme kwenye derby hiyo ya Jumapili ya Aprili 29 dakika ya 48 wakati mchezaji huyo alipotolewa nje kwa kadi nyekundu baada ya kumchezea madhambi beki wa Simba, Asante Kwasi.

Mwamuzi katika mchezo huo alikuwa, Emmanuel Mwandembwa na wakati akionyeshwa kadi hiyo, tayari alikuwa na kadi ya njano, katika pambano hilo Simba ikishinda bao 1-0 lililofungwa na Erasto Nyoni kwa kichwa dakika ya 37, baada ya adhabu iliyopigwa na Shiza Kichuya.

Kessy aliwahi kukipiga Simba kabla ya kutimkia Yanga na baadaye kwenda Zambia, kujiuunga na Nkana na sasa anaitumikia Mtibwa Sugar.


BOKUNGU -2017

Ulikuwa mchezo wa Februar 25, 2017 wakati beki wa Simba, Besala Bokungu akionyeshwa kadi nyekundu na mwamuzi wa mchezo huo, Mathew Akrama kutoka Mwanza.

Beki huyo alipewa kadi nyekundu dakika ya 54, kwa kumfanyia madhambi, Obrey Chirwa aliyekuwa anaelekea langoni huku Yanga ikiwa mbele bao 1-0, lililofungwa na Simon Msuva dakika ya 5 kwa mkwaju wa penati baada ya Chirwa kufanyiwa madhambi na Novatus Lufunga,

Licha ya Simba kucheza pungufu kwenye mchezo huo lakini iliondoka na ushindi wa mabao 2-1 yaliyowekwa nyavuni na Laudit Mavugo na Kichuya.


MKUDE - 2016

Moja ya mchezo ambao hautasahaurika kwa wapenzi wa soka nchini ni hili pambano la watani wa jadi la Oktoba Mosi, 2016 baada ya Jonas Mkude kumalizia mchezo huo akiwa chumba cha kubadilishia nguo kwa kuonyeshwa kadi nyekundu.

Mkude alionyeshwa kadi hiyo kwa kuonekana kuwa kinara wa fujo baina ya wachezaji wa Simba waliokuwa wakipinga bao lililofungwa na Amis Tambwe kwa mwamuzi wa mchezo, Martin Saanya lakini Kamati ya Masaa 72 baada ya uchunguzi ilimfutia adhabu hiyo.

Mchezo huo ulimalizika kwa sare ya 1-1 lile la Tambwe dakika ya 26 pamoja na lile la Kichuya dakika ya tatu kabla ya kipyenga cha mwisho kwa kona iliyozama langoni moja kwa moja na kumwacha kipa wa Yanga Ally Mustafa ‘Barthez’ kichwa chini.

Baada ya mchezo huo Kamati ya Bodi ya Ligi iliipiga faini Simba faini ya Sh 5 Milioni kutokana na uharibifu uliojitokeza katika mchezo huo kwa mashabiki wanaoaminiwa kuwa wa Simba kung’oa viti uwanjani.

Saanya, pamoja na wasaidizi wake Samwel Mpenzu na Ferdinand Chacha nao wakikumbana na rungu, huku Afisa Habari wa Simba, Haji Manara akipigwa faini ya Sh 100,000.


BANDA - 2016

Beki Abdi Banda alikuwa matata tangu akiwa Msimbazi, lakini utata wake ulizaa hasara katika pambano la watani wa jadi lililopigwa Februari 20, 2016 na Yanga kuondoka kifua mbele kwa mabao 2-0.

Banda alitumia dakika 23 uwanjani kabla ya mambo kuanza kumwendea kombo alipoonyeshwa kadi ya njano kwa kumchezea sivyo mshambiliaji wa Yanga, Donald Ngoma, na dakika mbili baadaye alirudia makosa na mwamuzi wa mchezo huo, Jonesia Rukyaa kumzawadia kadi nyekundu.

Mabao ya Yanga katika mchezo huo yalifungwa na Ngoma dakika ya 39 pamoja na Tambwe aliyegonga msumari wa mwisho kwenye jeneza la Simba.