Mapinduzi Cup, ile vita imerudi

New Content Item (1)
New Content Item (1)

Muktasari:

  • BAADA ya siku 116 tangu kuanza kwa msimu mpya wa 2022-2023 wa Ligi Kuu Bara na mechi 120 kupigwa kwa sasa macho na masikio ya mashabiki wa soka yanahamia visiwani Zanzibar.

BAADA ya siku 116 tangu kuanza kwa msimu mpya wa 2022-2023 wa Ligi Kuu Bara na mechi 120 kupigwa kwa sasa macho na masikio ya mashabiki wa soka yanahamia visiwani Zanzibar.

Ndio, ule msimu wa michuano ya Kombe la Mapinduzi umewadia kwa timu kutoka Bara na Zanzibar kuchuana kuwania ubingwa wa msimu wa 2023.

Michuano hiyo itaanza mwishoni mwa Desemba hadi Januari 13. Huu ni msimu wa 17 tangu kuasisiwa tangu mwaka 2007, safari hii nani atabeba taji baada ya msimu uliopita Simba kubeba taji ikiipokea Yanga.

Kombe la Mapinduzi lina historia ndefu, licha ya kuchukuliwa kama ya michuano ya kisiasa zaidi, lakini ukweli ni moja ya michuano iliyojipatia umaarufu na ambayo imekuwa ikiwapa burudani wakazi wa visiwani wenye wazimu wa soka.

Mwanaspoti linakuainishia rekodi za michuano hiyo ambayo awali ilishirikisha timu za visiwani miaka ya 2000 kabla ya kubadilishwa 2007 na kuchezwa katika mfumo wa sasa, japo ule utamaduni wa kuzialika timu kutoka nje ya Tanzania uliachwa takribani misimu mitatu iliyopita.


KAZI IPO

Ushiriki wa timu tano za Bara, moja kutoka Burundi na nne za Zanzibar kunafanya michuano ya mwaka huu kuwa mitamu na mikali zaidi. Ongezeko la Singida Big Stars limeongeza ushindani kwani kwa misimu karibu yote timu za Simba, Yanga, Azam na wakati mwingine Mtibwa na Namungo ndizo zimekuwa zikishiriki michuano hiyo na zimekuwa zikifanya kweli kwa kurejea na ubingwa kila mwaka.

Rekodi zinaonyesha katika fainali 16 za michuano hiyo timu za Bara zimegawana jumla ya mataji 13, huku ni mara moja kwa timu za visiwani kunyakua ubingwa huo, misimu miwili ubingwa huo ukibebwa na timu za nje.

URA na KCCA zote za Uganda kwa misimu miwili tofauti zilitwaa ubingwa huo, huku Miembeni ikiwa ndio timu pekee kwa timu za Zanzibar kutwaa taji hilo.

Januari 2020 Mtibwa ilibeba ndoo kwa kuing’oa Yanga hatua ya nusu fainali kisha kuinyuka Simba katika fainali ya kibabe kwa bao pekee la Awadh Juma.

Simba ilipenya fainali kwa kuifunga Azam kwa penalti 4-2 baada ya dakika 90 kumalizika kwa suluhu.


AZAM IMETISHA

Licha ya kupasuliwa kwenye fainali zilizopita za michuano hiyo, lakini Azam ndio baba lao la michuano hiyo, kwani katika mechi zote za fainali ambazo ilizobahatika kutinga ni mara moja tu ndio imeishia kutoka kapa kwa kushindwa kubeba ndoo.

Azam imefika na kucheza jumla ya fainali sita, kati ya hizo tano iliondoka na ushindi isipokuwa msimu uliopita ilipopasuka mbele ya Simba kuonyesha kuwa wao na Kombe la Mapinduzi ni damdam.

Mabingwa hao wa kihistoria wa michuano hiyo walicheza fainali ya kwanza mwaka 2012 dhidi ya Jamhuri Pemba na kuibamiza mabao 3-1 yaliyowekwa kimiani na John Bocco, Mrisho Ngassa na bao la kujifunga na Ahmed Mrisho, huku Ali Mmanga aliifungia Jamhuri bao la kufutia machozi.

Kisha wakarudi tena msimu uliofuata kwa kuvaana na Tusker ya Kenya na kuinyoa kwa mabao 2-1 ya Joachins Atudo na Gaudence Mwaikimba, huku Jesse Werre akiwafungia Wakenya la kufutia machozi, baada ya hapo ikasubiri kwa miaka minne bila kufika hatua hiyo ya fainali.

Iliporejea tena 2017 iliitungua Simba bao 1-0 la mkwaju mkali wa mbali wa dakika za mapema za mchezo huo uliopigwa na kiungo, Himid Mao ‘Ninja’, aliyepo Misri kwa sasa.

Mwaka 2018 ilitetea tena taji kwa kuicharaza URA ya Uganda kwa penalti 4-3 baada ya dakika 90 kumalizika kwa suluhu na kuja kulibeba jumla taji hilo mwaka juzi kwa kuichapa tena Simba mabao 2-1. Mudathir Yahya na Obrey Chirwa, beki Yusuf Mlipili aliifungia Simba bao la kufutia machozi lililokuwa la kusawazisha katika kipindi cha pili, kabla ya Mzambia Chirwa kutibua kwa kufunga la ushindi.

Msimu uliopita ikatinga fainali ya sita, lakini safari hiyo ilizimwa na Simba kwa kufungwa bao 1-0 kupitia Meddie Kagere aliyeibuka mfungaji bora wa michuano hiyo na kuifanya Azam isaliwe na mataji matano, ikifuatiwa na Simba iliyonyakua mara nne, kisha Mtibwa Sugar na Yanga ikabeba mara mbili kila mmoja, huku Miembeni ya Zanzibar, URA na KCCA zote za Uganda zikibeba mara moja moja.


ISHU KWA WAZENJI

Licha ya ukweli michuano ya Mapinduzi kufanyika Zanzibar na kuzifanya timu za visiwani hivyo ndio kuwa wenyeji wa mashindano, lakini kwa miaka 16 ya michuano hiyo wametwaa taji mara moja tu, zilipokutana wenyewe kwa wenyewe.

Fainali hiyo pekee ambayo mashabiki wa soka wa Zenji walishuhudia timu za visiwani humo zikipepetana ilipigwa katika msimu wa tatu wa michuano hiyo yaani mwaka 2009 wakati Miembeni ilipoifumua mabaharia wa KMKM kwa bao 1-0.

Baada ya hapo ni mara mbili tu timu za visiwani zilifika fainali na mara zote zilipoteza, ilianza Ocean View iliyocheza na Mtibwa Sugar mwaka 2010 na kulala 1-0 lililowekwa kimiani na Kocha msaidizi wa Ihefu, Zubeiry Katwila dakika ya 14.

Kisha ndipo Jamhuri ya Pemba timu pekee ya kisiwa hicho kufika fainali ikifanya hivyo mwaka 2012 na kulala mbele ya Azam iliyokuwa ikinyakua taji la kwanza la michuano hiyo.


YANGA UBABE

Mabingwa wa kihistoria wa Ligi Kuu Bara, Yanga licha ya ubabe wa mataji 28 hadi sasa ya TPL, lakini kwenye Mapinduzi wanatia huruma, kwani wamebeba mara mbili tu. La kwanza mwaka 2007 na kukaa kwa misimu 14 kabla ya kutwaa tena 2021 kwa kuinyoa Simba katika fainali ya aina yake ilipigwa Januai 13, 2021. Pia rekodi zinaonyesha timu hiyo imewahi kutinga fainali tatu za michuano hiyo ikiwamo ile ya 2011 ilipokutana na Simba na kucharazwa mabao 2-1 yaliyofungwa na Emmanuel Okwi na Hillary Echessa, huku chipukizi Saad Ramadhani akiifungia Yanga bao la kufutia machozi. Baada ya hapo Yanga imekuwa ikikwamia nusu fainali kama ilivyotokea tena msimu uliopita ilipotunguliwa na Azam.


USHINDANI MKALI

Klabu za Bara zimekuwa zikionyeshana kazi na kuchuana vikali kwenye michuano hiyo kama ambavyo ilivyokuwa fainali zilizopita ambapo timu nne za Bara ikiwamo Namungo, Azam, Simba na Yanga zote zilitinga nusu fainali na kutoana zenyewe kwa zenyewe. Simba ikiing’oa Namungo na Yanga kutolewa na Azam, ilihali misimu miwili nyuma Mtibwa Sugar nayo ilikuwa ikizitoa nishai ndugu zao wa Bara ikiwamo ile ya 2020 ilipoing’oa Yanga jioni na kwenda kubeba taji kwa kuifunga Simba katika fainali kali.

Safari hii michuano hiyo itakayoanza Januari 1-13, 2023 itashirikisha jumla ya klabu 12, ikiwamo Agle Noir ya Burundi iliyoalikwa kutoka nje ya nchi, pia timu za Bara safari hii zitakuwa tano na sio nne kama zilizoeleka, ikiwamo watetezi Simba, Azam, Yanga, Namungo na Singida Big Stars iliyopanda Ligi Kuu Bara msimu huu, wakati kwa Unguja itawakilishwa na watetezi wa Ligi Kuu (ZPL), KMKM, vinara wa duru la kwanza kwa msimu huu, KVZ, Mlandege na Malindi, wakati Chipukizi na Jamhuri zitaviwakilisha visiwa vya Pemba.

Kamati ya michuano hiyo imenogesha zaidi kwa kuongeza dau la zawadi za washindi ambao mbali na kubeba taji na medali, lakini watapewa mkwanja wa Sh 30 milioni tofauti na msimu uliopita huku itakayomaliza ya pili itaondoka na Sh 20 milioni, mbali na medali.

Nini kitatokea? Tusubiri wakati ratiba ya michuano hiyo ya msimu wa 17 itakapotolewa na kamati ya kusimamia imekuwa ikiimarika kila msimu tangu ilipoasisiwa.