MAONI: Simba ijipange zaidi iishangaze Afrika

Monday April 05 2021
MAONI PIC

SIMBA imetinga hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa mara ya pili ndani ya miaka mitatu, wakati ilipoifunga AS Vita Club ya DR Congo kwa mabao 4-1.

Katika mchezo huo wa Ligi ya Mabingwa Afrika uliofanyika kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Simba ilikuwa ikihitaji pointi moja kujihakikishia nafasi hiyo adimu kwa timu za ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.

Mabao ya Luis Miquessone, Clatous Chama (mawili) na Larry Bwalya yalitosha kuishitua Afrika kuwa kuna timu ambayo inaweza kuongoza kundi lililo na bingwa mtetezi, Al Ahly, ambaye naye alichapwa katika Uwanja wa Mkapa.

Simba imeshinda michezo yake yote iliyocheza katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, ikiwa ni mwendelezo mzuri wa ushindi wa nyumbani tangu ilipoanza kuwa katika kiwango kizuri.

Hadi sasa, mabingwa hao wa soka Tanzania, Simba hawajawahi kufungwa kwenye uwanja wa nyumbani kwa miezi 97, sawa na miaka minane na mwezi mmoja na siku 13, rekodi ambayo inatia matumaini katika ushiriki wao wa sasa wa kimataifa.

Kwa mafanikio ya msimu huu, Simba sasa itakuwa ikiongoza Kundi A kabla ya mchezo wao wa mwisho wa hatua ya makundi, ambao watamaliza ugenini dhidi ya Al Ahly na kupangwa hatua ya robo fainali ya mashindano hayo.

Advertisement

Kutokana na kuongoza kundi, Simba itakuwa na faida ya kuanzia ugenini, huku pia ikicheza na mshindi wa pili wa moja kati ya makundi mengine matatu yaliyobaki, jambo ambalo pia linaweza kuleta wepesi katika michezo yao miwili kuelekea hatua ya nusu fainali.

Msimu huu, Simba imekutana na timu ngumu kama Al Ahly na AS Vita, ambazo msimu wa mwisho kukutana na timu hizo ilifungwa jumla ya mabao 10 katika michezo miwili ya ugenini iliyokutana nazo.

Simba ilifungwa mabao 5-0 na AS Vita katika hatua ya makundi na kufungwa pia idadi hiyo ya mabao dhidi ya Al Ahly, lakini ilifanikiwa kutinga robo fainali na kukutana na TP Mazembe, ambao katika mchezo wa kwanza uliofanyika Uwanja wa Mkapa, Simba ililazimishwa sare kabla ya kufungwa mabao 4-1 ugenini.

Kutokana na rekodi hiyo nzuri ya nyumbani, tunaamini kuwa Simba, kama itaendelea kuandaliwa vizuri kama ilivyofanya katika hatua ya makundi, ni wazi kuwa inaweza kutinga katika hatua ya nusu fainali ya mashindano hayo makubwa Afrika katika ngazi ya klabu.

Kwasasa, Simba ina kikosi bora, ambacho kinaweza kuleta ushindi popote, lakini rekodi nzuri ya kucheza nyumbani ikiwa na uhakika wa kuvuna pointi tatu inatoa ishara nzuri ya kuiona ikienda nusu fainali ya mashindano ya Ligi ya Mabingwa msimu huu.

Suala la kuongoza katika kundi lake limekuwa na faida ya kuanzia ugenini, ambako inaweza kulazimisha sare kama si ushindi kabisa kama ilivyofanya kwa AS Vita na kisha kuja kumaliza shughuli ikiwa nyumbani.

Kuna kila sababu kwa Simba kuangalia nafasi hii msimu huu kuwa inaweza kuleta historia nyingine katika mchezo wa nusu fainali kwani kikosi chenyewe kimeonyesha utayari wa kufika mbali katika mashindano ya msimu huu.

Tunaamini kuwa uongozi mzima wa Simba nao unatazama nafasi hii kwa jicho chanya na inaweza kusonga mbele zaidi kama mipango yao itakuwa na mtazamo wa moja kwa moja kufikia mafanikio.

Lengo lilikuwa ni nusu fainali, mashindano yanaendelea na lengo likionekana kuwa hai na maandalizi pekee ndiyo yatakayoipa nafasi Simba kutimiza walichokianza.

Advertisement