Manyika Jr: Mapro mbona fresh, Okwi balaa

ULE usemi wa wahenga “maji hufuata mkondo” na “mtoto wa nyoka ni nyoka” umeonekana kwa Manyika Peter.

Manyika Jr amefuata kipaji cha baba yake Peter aliyetamba miaka ya nyuma akiwa na uzi wa Yanga na timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’. Peter alikuwa bonge la kipa enzi zake.

Usemi huo umeendana nao kwani wakati wote hawajaanza kudaka walicheza ndani ya uwanja wakitamba zaidi kwenye ushambuliaji wa kati yaani namba tisa.

Mwanaspoti linakuletea mahojiano na Manyika Jr aliyejizolea umaarufu alipokuwa akiichezea Simba licha ya sasa kutosikika katika medani ya soka.


ANAFANYA NINI?

Kwa sasa Manyika Jr hana timu licha ya kupokea ofa kadhaa wakati wa dirisha kubwa la usajili lililofungwa Agosi 31, lakini mambo hayakwenda kama alivyotarajia. “Nafanya mazoezi yangu mwenyewe tu naamini kwa uwezo wa Mungu nitapata timu wakati wa dirisha dogo lijalo la Desemba,” anasema Manyika Jr.


MAISHA SIMBA

Kipa huyo anasema kipindi anaichezea Simba ilikuwa na hali ngumu kiuchumi na kimfumo tofauti na hivi sasa.

“Wakati ule timu haikuwa na mafanikio ya vikombe. Nakumbuka toka naingia mwaka wangu wa mwisho ndio tulipata kombe la FA, ndio tukarudi kushiriki michuano ya kimataifa.

“Simba na Yanga ni timu nzuri na kubwa, hakuna mchezaji ambaye anaweza kujutia kuwepo. Kikubwa ni kuhakikisha unakaza buti ili kupata nafasi ndani ya kucheza,” anasema Manyika Jr.

Mchezaji huyo anasema alipoingia Simba kulikuwa na makipa wazuri kina Ivo Mapunda na Hussein Sharif ‘Casillas’.

“Mechi yangu ya kwanza kucheza ilikuwa dhidi ya Orlando Pirates ya Afrika Kusini, ilikuwa ya kirafiki. Nakumbuka kipindi cha kwanza Casillas aliumia na mimi nikacheza kipindi cha pili, tulitoka sare ya bila kufungana. Mchezo uliofuata nikacheza dhidi ya Bidvest ya Afrika Kusini tukarudi kucheza na Yanga.

“Mechi ya Yanga ilikuwa 2014 nilipangwa kuanza kwani ilikuwa lazima tu nicheze kwani Ivo aliumia kidole cha mkononi na Casillas alivunjika mguu, sasa ndio ilikuwa mechi yangu ya kwanza ya ligi kuanza,” anakumbuka nyota huyo.

Anasema haikuwa kazi nyepesi kwani aliyekuwa nahodha wa kikosi hicho, Joseph Owino, raia wa Uganda na Ivo walimjenga kisaikolojia ili ajiamini awapo langoni.

“Baba yangu naye alishiriki kwa asilimia kubwa kuzungumza na mimi, akiniambia unaweza ndio maana umesajiliwa nenda kadake, cheza kama unavyocheza usihofu. Niliamini na mchezo (huo) hatukufungana,” anasema.


KUTOKULA SIKU YA MECHI

Manyika Jr anaweka wazi kuwa akiwa na uhakika wa kucheza siku ya mechi, basi huwa hali chochote akihofia kujihisi kuwa mzito mchezoni.

“Ni namna ambavyo nimejiwekea (utaratibu) tu. Nikila chakula najiona mzito kwani siku hiyo natumia muda mwingi kuucheza mchezo kichwani kabla hata ya kuingia ndani ya uwanja,” anasema


KWELI ALILEWA SIFA?

Akizungumzia iwapo alilewa sifa baada kung’ara kwa muda kisha kupotea katika sok, Manyika Jr anasema: “Huwezi kuacha watu waseme maana kabla sijaingia Simba baba aliniambia nitakutana na vitu vingi katika mpira, hivyo cha msingi ni kufanya kilichonipeleka sehemu ambayo nitakuwepo. Vitu vingi vilizungumzwa juu yangu, sijui starehe mambo mengi sana na ndio maana nilinyamaza tu nikikumbuka maneno ya baba aliyoniambia mwanzoni, maana kila mtu katika mpira anaongea atakavyo.”

“Sikuwahi kubadili dini yangu kama ambavyo watu walisema mara nimechora tatoo.. sijawahi katika mwili wangu kufanya hicho kitu, lakini watu wakiamua lao kuwazuia ni ngumu sana mara nimeoa yote ni maneno tu.

“Ni mambo tu yalikuwa yakizungumzwa, lakini unavyoniona sio mtu wa pombe, kilabu wala uhuni kama ambavyo walikuwa wakinisema. Napenda sana kukaa ndani nacheza gemu, naweza kushinda siku nzima nisitoke nje,” anasema Manyika Jr na kwamba hatasahau kipindi cha mpito ambacho Simba ilipitia kabla ya kuanza kupata mafanikio miaka minne mfululizo


BABA NDO KILA KITU

Mchezaji huyo anasema asilimia kubwa katika maisha yake ya soka baba ndiye msimamizi wake mkubwa.

“Baba ndio kila kitu kwangu hadi hapa nilipo ni mchango wake mkubwa sana. Naheshimu sana namna ambavyo ananipambania mwanaye, hata nikikosea humuomba msamaha kwa kuwa naelewa umuhimu wake kwangu,” anasema Manyika anayependa kumuita baba yake ‘Super Coach’.


NJE YA NCHI

Kutokana na umri wake wa miaka 26 anaamini bado uwezo na nafasi anayo kwani amewahi kukipiga KCB inayoshiriki Ligi Kuu ya Kenya (KPL) kwa miaka miwili.

“Maisha yalikuwa kawaida hapo awali, lakini ilifikia wakati ligi ikawa haie-leweki timu hazitokei uwanjani, nyingine zinapata pointi tu bila ya kucheza, basi nikaona isiwe shida nikarudi nyumbani,” anasema.

“Mambo ya Mungu mengi. Wakati napenda kwenda kucheza nje haikuwezekana nilipotoa mawazo hayo ndio nikapata nafasi ya kwenda nje. Sasa inaweza ikatokea tena nikaenda,” anasema na kuongeza kuwa baba’ke mzazi ndiye alimfanya avutiwe kucheza nafasi hiyo.


MAPROO

Manyika Jr anasema mapro ruksa kukipiga katika ligi ili wawaamshe wazawa na hapa anasema: “Mchezaji anatakiwa apambane kuonyesha kiwango kuanzia mazoezini, kwani kocha hawezi kuacha kukupanga. Sema wazawa tunakuwa na mawazo vichwani na ndio maana tunafeli. Hata ningekuwa mimi nimemsajili mchezaji kutoka nje lazima nitamwangalia yeye kwanza, lakini ni jukumu letu wazawa kujituma na kuhakikisha tunapambana.”


OKWI SI MCHEZO

Manyika Jr kacheza na washambuliaji wengi Ligi Kuu Bara, lakini anamtaja straika wa zamani wa Simba, Emmanuel Okwi kuwa alikuwa balaa.

“Okwi nakumbuka wakati nikicheza naye Simba alikuwa akiwasumbua wapinzani, sasa nikaja kukutana naye nikiwa Singida United alinisumbua. Wakati anaingia (uwanjani) nikawafuata mabeki wangu wakati huo Kennedy Juma na mwenzake nikawaambia hakuna mshambuliaji mwenye madhara kama huyu mjitahidi msimpe nafasi,” anasema Manyika Jr.

“Nakwambia ndani ya dakika tano ikapigwa pasi kisha akanifunga na mazingira ya kufunga huwezi kujua ni muda gani.”


TIMU ALIZOPITA

Manyika Jr amechezea timu za Zaragoza (akiwa Sekondari ya Mbweni akicheza namba tisa), Basihaya akiwa sekondari za Makongo na Jitegemee kama kipa, Twalipo Kurasini, Mgambo, JKT Ruvu (JKT Tanzania), Kizuka, Red Coast, Bomu FC), Simba, Singida United, KCB na Dodoma Jiji.