Mambo yaliyotikisa afya AFCON 2025
Muktasari:
- Mchezo huo wa fainali, uliochezwa katika mji mkuu wa Morocco, Rabat, ulikuwa na mikaranganyiko kadhaa, ikiwamo uamuzi tata wa penalti dakika ya 98, kiasi cha kusababisha mchezo huo kusimama kwa dakika 17.
SIMBA wa Teranga, timu ya Taifa ya Senegal, walifanikiwa kutwaa ubingwa wa Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2025, siku nne zilizopita baada ya kuwalaza wenyeji, Morocco, kwa bao 1-0.
Mchezo huo wa fainali, uliochezwa katika mji mkuu wa Morocco, Rabat, ulikuwa na mikaranganyiko kadhaa, ikiwamo uamuzi tata wa penalti dakika ya 98, kiasi cha kusababisha mchezo huo kusimama kwa dakika 17.
Ulikuwa moja ya fainali bora, ambapo kila timu ilionyesha uwezo wao kuanzia kimwili na kiakili, wakiwa katika ubora usio na shaka, wakisakata kandanda la safi na la kuvutia.
Fainali hiyo, iliyoteka hisia za mamilioni ya wadau wa soka duniani, iliweza kusababisha athari kadhaa za kiafya, kiakili na kimwili, kwa wachezaji na mashabiki waliopo ndani na nje ya uwanja.
Mtakumbuka, wiki iliyopita, Rais Samia Suluhu Hassan, wakati alipowalika Ikulu wachezaji wa Taifa Stars, alieleza jinsi alivyokabiliwa na hisia kali wakati akitazama mchezo wa Tanzania dhidi ya Morocco.
Hali kama hiyo ndiyo iliwapata maradufu mashabiki 66,000 waliokuwepo uwanjani kushuhudia mpambano huo, uliochezwa kwa dakika 120, kutokana na dakika 90 za awali kwenda 0-0.
Leo tutaangazia athari za kiafya ambazo zilijitokeza katika mpambano huo, ulioshuhudia Senegal wakibeba ubingwa kwa mara ya pili, wakiwa chini ya kocha mzawa, Pape Thiaw.
Ulinganifu utimamu kimwili
Hali za kiafya za wachezaji wa timu zote mbili zilionekana kuwa imara; wengi waliochezewa faulo walionekana kuwa na ustahimilivu wa juu. Hata wachezaji waliokuwa na majeraha ya awali walikuwa timamu.
Mfano ni nahodha wa Morocco, Achraf Hakimi, ambaye mechi za awali alizikosa kutokana na majeraha ya kifundo. Wachezaji wengine wote walikuwa timamu.
Ingawa, kiujumla, yule aliyebeba ubingwa ndiye pia amemzidi mwenzake utimamu wa kimwili na kiakili, wachezaji wa Senegal walionekana kujiamini na kuwa na umakini mkubwa, hatimaye kumiliki mpira zaidi.
Ukubwa wa maumbo yao haukuwafanya waonekane ni wazito; walikuwa na kasi, nguvu, walinyumbulika na hawakuchoka kirahisi. Hii ni ishara kwamba walikuwa na ukakamavu na ustahimilivu wa juu.
Miaka ya nyuma tulizoea timu za Kaskazini zenye asili ya tabaka la Kiarabu kujiangusha, lakini Morocco walionyesha kutumia nguvu wakiwa na maumbo magumu. Wachezaji hao walikwatua na walikwatuliwa pia, na waliwapa miili wapinzani wao. Hii ilikuwa ishara ya kubadilika kwa utimamu wao.
Majeraha yaliyojitokeza
Katika fainali hiyo kulikuwa na kukumbumbana sana kimwili; wachezaji walikabana sana, na faulo za hapa na pale zilikuwepo, hasa eneo la kati lililo na harakati nyingi.
Kipindi cha pili, mchezaji wa Morocco, El Aynaoui, alipata majeraha mabaya ya kichwa, yaliyosababisha kuvuja damu kutokana na kupata mchaniko usoni. Aliruhusiwa kuendelea, zikiwa zimebaki dakika nane.
Ingawa wengi waliona haikuwa sahihi kuendelea na mchezo huo, kwa jicho la kitabibu, kisaikolojia, mwanadamu wengi hupata hofu wanapoona damu inatoka, kiasi cha kuona kuwa ni tishio.
Ukweli ni kuwa kupata jeraha la mchaniko kichwani bado haikuwa hatari, kwani madaktari walidhibiti damu hiyo na hakupoteza nyingi. Uamuzi wa kumruhusu kuendelea kucheza ni kwa sababu hakuwa na viashiria vya majeraha ya ubongo, ikiwamo kupoteza fahamu. Viashiria nyeti vya mwili vilionekana kuwa imara.
Ndio maana aliweza kucheza bila shida yoyote, huku akiwa na bendeji kichwani. Niwatoe hofu pia, wachezaji wote hupimwa afya, ikiwamo yale magonjwa ya kuambukiza kama VVU na homa ya ini.
Mchezaji mwingine ni Hamza Igamane, aliyeingia dakika za nyongeza, alipata majeraha mabaya ya goti, akijeruhi nyuzi ngumu za mbele ya goti, yaani ligamenti ijulikanayo kifupi ACL.
Majeraha kihisia, kisaikolojia
Mpira unabeba hisia. Mliona kilichotokea baada ya kutolewa kwa penati iliyozua ghadhabu na hasira; wengi walidhani refa hakutenda haki.
Kocha wa Senegal aligadhibika kiasi cha kuamua kuwatoa wachezaji kususia penati hiyo. Lakini, kumbe kulikuwa na mchezaji mshauri, Sadio Mane, ambaye ndiye aliyewatuliza kisaikolojia.
Alifanikiwa sana kuweza kutumia ushauri tiba wa papo kwa hapo, kutuliza hasira ya wachezaji na kocha, hatimaye kuleta utulivu ulioleta kujiamini upya na kufanikiwa kushinda.
Utulivu waliorudi nao uwanjani uliwafanya kuonekana katika dakika za nyongeza, kama vile walikuwa wananza dakika za mwanzo. Waliweza kuwa wastahimilivu dhidi ya presha zote.
Baada ya kipyenga cha mwisho kupigwa, wachezaji na maelfu ya mashabiki wa Morocco walipata mpasuko wa hisia, wasiamini kilichotokea.
Walipata huzuni kali sana, ikiwamo mchezaji aliyekosa penati, Ibrahim Diaz, ambaye wakati wote baada ya mchezo kuisha alionekana kulia, huku sura ikionekana nyekundu.
Itakumbukwa pia kulitokea vurugu kwa dakika chache, baada ya mashabiki kuanza kurusha viti, kupiga wengine, na huku baadhi wakipigana. Hali hii imeacha majeraha ya kimwili na kiakili.
Imani potofu dhidi ya Taulo
Moja ya vituko ni pale mataulo ya golikipa Mendy wa Senegal; mchezaji wa Morocco alimzuia kipa wa akiba kulinda taulo hizo. Wengi mitandaoni walihusisha na imani potofu za kishirikina na dawa za kulegeza mwili.
Ukweli ni kuwa mataulo yale huwa yanahitajika kunyonya vizuri maji kwenye mikono ya makipa. Bila hivyo, mpira unaweza kuteleza, hatimaye kuwa faida kwa wapinzani.
Uwepo wa mchezaji wa Morocco kuiba mataulo hayo ni dhahiri; walitaka mikono ya Mendy iteleze iwe faida kwao, kwani walidhani wangekwenda hatua za matuta.
Kama kweli ndumba au juju zinafanya kazi katika soka, basi kuna nchi au klabu zingeliweza kufanikiwa sana kutokana na baadhi ya nchi kuamini imani hizo.
Zaidi, viashiria vya ushirikina huwa ni mbinu za kuwadhoogisha wapinzani kisaikolojia, hatimaye kuwatoa mchezoni na kushindwa kuwa makini uwanjani kutokana na hofu.
Tuzo ya fair play
Kifungu cha 8 cha Kanuni za CAF za Kombe la Mataifa ya Afrika kinasema kwamba: “Tuzo ya ‘fair play’ litatolewa kwa timu ambayo itaonyesha roho nzuri ya haki wakati wa awamu ya mwisho ya Kombe la Mataifa ya Afrika, kwa mujibu wa kanuni za fair play za CAF.”
Tuzo hiyo imekwenda kwa timu ya Morocco, ingawa wamepata ukosoaji kutokana na matukio yaliyojitokeza. Ukweli ni kuwa walionyesha uungwana na utu katika matukio mengi, ikiwamo waliopofanya faulo mbaya.
Uungwana katika kandanda ni muhimu sana ili kuwalinda wale walijeruhiwa uwanjani, ili wapate huduma ya kwanza kwa wakati.
Chukua hii
Senegal imetwaa ubingwa wa Afrika kwa mara ya pili. Ni dhahiri wamewekeza katika soka la kisasa kwa miongo mingi, na uwepo wa maandalizi thabiti ya muda mrefu ndio umeleta matokeo makubwa.