Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mambo mawili yaliyoitega Dabi K'koo uwanjani

MBINU Pict


KARIAKOO Dabi ambayo imekuwa ikizikutanisha Yanga na Simba ni moja ya mechi zinazovuta hisia za wadau na mashabiki wengi na soka kuanzia ukanda wa Afrika Mashariki na Kati hadi Afrika kwa jumla, ikizingatiwa historia ya miamba hiyo.


Na wala sijui kama ni kweli au laa ila hii inaweza kuwa pengine mada ya siku nyingine, wanasema kama usipokuwa Simba basi wewe ni Yanga, ni wachache mno ambao timu hizi zikikutana wanaweza wasiwe na upande.


Kila msimu, Kariakoo Dabi imekuwa ikileta ushindani wa aina yake kuanzia ndani hadi nje ya uwanja. Msimu huu, mechi inaonekana kuwa na mvuto wa vitu vingi ikiwemo ulinganifu wa kimbinu na ufundi kwa makocha wa timu hizo, Pedro Soares Goncalves kwa Yanga na Steve Barker kwa Simba.

Tangu Pedro arithi mikoba ya Romain Folz, Oktoba, 2025, ameiongoza Yanga katika mechi nane za ligi dhidi ya Mtibwa Sugar mabao 2-0, KMC (4-1), Fountain Gate (2-0), Coastal Union (1-0), Mashujaa (6-0), Dodoma Jiji (3-1), Namungo (1-0) na JKT Tanzania (5-0).

Katika mechi hizo, Yanga imeshinda zote na kukusanya pointi 24 chini yake, Mreno huyo aliikuta timu hiyo ikiwa na pointi nne ambazo ilivuna baada ya kuichapa Pamba Jiji katika mechi ya kwanza ya msimu katika ligi kwa mabao 3-0 na kutoa suluhu dhidi ya Mbeya City.

PRESH 06

Kwa upande wake, Barker ameiongoza Simba katika mechi tano za Ligi Kuu Bara, alianza kwa sare ya bao 1-1 dhidi ya Mtibwa Sugar kabla ya kushinda mechi tatu mfululizo dhidi ya Mashujaa, KMC na Tanzania Prisons kila mechi ikiwa kwa mabao 2-0 na katika mechi ya mwisho kabla ya dabi akadondosha pointi mbili dhidi ya Dodoma Jiji (0-0).

Katika mechi hizo, Barker ana wastani wa ushindi kwa asilimia 60 huku Pedro akiwa na 100.

Sasa nani kati yao atamtibulia mwenzake na kumfanya kukumbana na kipigo cha kwanza katika ligi ni suala la kusubiri na kuona kitakachotokea kwenye Uwanja wa Amaan, Zanzibar. Embu tutazame kiufundi namna makocha hao watalivyo na watakavyobaliana kulingana na silaha zao.

PRESH 02

UTAMU ULIPO

Katika mechi nane za ligi, Pedro ameonekana kupenda kushambulia zaidi huku akiwa mwepesi wa kujilinda hasa katika kipindi cha pili tena baada ya kuwa mbele ili kukamilisha hesabu zao.

Kocha huyo amekuwa akipenda zaidi kutumia mfumo  4-3-3 ambao unahusisha kasi na matumizi makubwa ya wachezaji wa pembani katika kushambulia na kutengeneza nafasi za mabao. Kwa Pedro, mabeki wa pembani wamekuwa na mchango mkubwa katika mipango yake.

Ndiyo maana Mohamed Hussein ambaye ni beki wa kushoto alifunga bao lake la pili msimu huu katika ligi dhidi ya JKT Tanzania na lilikuwa bao la kwanza kwa Wananchi katika mechi hiyo, wakati wa kutengeneza mashambulizi alikuwa nusu ya wapinzani alipasua kwa kugongenana na wenzake kabla ya Prince Dube kumpenyezea pasi ya mwisho.

PRESH 05

Kuna wakati Pedro amekuwa akibadilika kimfumo kutoka 4-3-3 ambao ni mfumo wake mama hadi 4-2-3-1 hapo hutoa nafasi kwa viungo wawili wakabaji na mara nyingi hubadilika baada ya kuona wamepoteza umiliki katika eneo la kati, hivyo Mohamed Damaro na Duke Abuya huwa na kazi maalum.

Kama haitoshi kocha huyo kuna wakati huamua kuwa na nguvu kubwa katika safu yake ya ushambuliaji kwa kuanza na washambuliaji wawili wa kati, Prince Dube na Laurindo Dilson 'Depu' kama ilivyokuwa dhidi ya JKT Tanzania ambao walijikuta wakipigwa tano.

Kwa upande wake, Barker falsafa yake ni timu kuongeza kasi ya mashambulizi hasa inapokuwa katika nusu ya pili, amekuwa akipenda kushambulia kupitia maeneo yote ya uwanja hasa pembeni kutokana na kasi ya wachezaji ambao wanacheza katika maeneo hayo, Libasse Gueye na Anicet Oura.

PRESH 08

Pia kuna Ellie Mpanzu ambaye kwa sasa ni kama amepoteza nafasi ya kuanza kikosi cha kwanza cha wekundu hao wa Msimbazi.

Mbali na nyota hao, Barker ana silaha nyingine ambayo ni Clatous Chama anayemtumia nyuma ya mshambuliaji ya mwisho, ni mchezaji mwenye jicho la pasi za mwisho hivyo amekuwa akitekeleza vizuri mpango wa mechi hasa akiwa eneo la kati, majukumu ambayo msimu uliopita yalikuwa yakifanywa na Charles Jean Ahoua ambaye ametimkia Algeria.

Barker amekuwa akipendelea naye kutumia mfumo wa 4-3-3 kama ilivyo kwa Pedro lakini utofauti wao upo katika namna ya kuutumia. Mmoja anahitaji mabeki wake kushambulia huku wakitumia mianya iliyopo kati ya beki wa pembeni na kati na mwingine hupenda mabeki wacheze pembeni zaidi.

PRESH 04

Ukiitazama Yanga wakati ikishambulia unaweza kuona hilo kuna wakati mabeki wa pembeni hupasua ndani katika mianya kati ya beki wa kati na pembeni lakini kwa Simba wamekuwa wakitanuka pembeni na wakati ambao mawinga wakiwa huko wamekuwa wakiibia ndani au kurudi nyuma kwa ajili ya usaidizi katika kujenga mashambulizi yao.



SASA ITAKUWAJE

Vikwazo vya mechi vinaonekana wazi kwa kuzingatia rekodi za hivi karibuni. Yanga chini ya Pedro imecheza mechi nane bila kupotezi, ikifunga mabao mengi katika mechi dhidi ya Mashujaa (6-0), JKT Tanzania (5-0). Mabingwa hao watetezi wamefunga jumla ya mabao 27 huku ikiruhusu mawili tu, wana wastani wa kufunga mabao karibu matatu kwa mechi.

Hii inaonyesha ufanisi wa kikosi cha Yanga katika mashambulizi na uwezo wa kubadilika kimbinu kwa haraka. Viwango vya timu vinaonyesha Yanga ina safu kali zaidi ya ushambuliaji ambayo kwa sasa inaongozwa na Depu mwenye mabao matano katika mechi nne za ligi.

PRESH 07

Wakati Yanga ikiwa na Depu, Simba ina Rushine De Reuck ambaye amekuwa nguzo ya ukuta wao huku akifunga mabao matatu na kuwa beki wa kati mwenye mabao mengi zaidi msimu huu wa Ligi Kuu Bara.

Katika mechi tano ambazo Simba imecheza chini ya Barker imecheza mechi tano, imeonyesha kuwa na kitu licha ya kuwa na idadi kubwa ya wachezaji ambao wameingia katika dirisha la usajili la Januari.

Simba imeruhusu bao moja tu ambalo lilikuwa dhidi ya Mtibwa Sugar lakini kwa ujumla imeruhusu mabao manne, changamoto iliyopo kwa wekundu wa Msimbazi kwa sasa ni uwezo wa kuimaliza mechi kikatili kwa kufunga mabao mengi. Uchambuzi wa viwango unaonyesha tofauti kuu mbili, Yanga inaweza kumaliza mechi kikatili kama itakuwa katika ubora wake lakini Simba hata kama itaishika mechi ushindi unaweza usiwe wa mabao mengi.


SILAHA MUHIMU

Kila kocha ana wachezaji muhimu wanaounda falsafa yake. Yanga itamhitaji Pacôme Zouzoua akiwa katika siku nzuri pamoja na kwamba Pedro amekuwa na machaguo mengi lakini nyota huyo wa kimataifa wa Ivory Coast mara nyingi amekuwa akifanya vizuri katika mechi hizi kubwa.

Mbali na Pacome, Yanga ina Allan Okello ambaye bado hajawaka vizuri lakini kama atakuwa katika ubora wake naye anaweza kuwa tatizo kwa Simba kwa sababu ana uwezo mzuri wa kutengeneza nafasi, mchezaji mwingine ambaye ni muhimu katika mipango ya Pedro ni Depu.

Kati ya wachezaji  ambao majina yao yanaweza kuwa ya kwanza katika upangwaji wa kikosi cha dabi basi Depu ni mmoja wao, anaweza kuanza kama mshambuliaji kinara au akasaudiana na Dube, hii ni silaha muhimu sana kwa kocha huyo kutokana na uwezo wake wa kutumia nafasi.

Simba, kwa upande mwingine, inategemea wachezaji wenye uzoefu kama Chama katika kutengeneza nafasi na kuhakikisha usawa wakati wakishambulia na wakati wakijilinda. Hii inatengeneza mpangilio wa kiakili na viwango vya kiufundi vinavyoamua matokeo ya mechi.

Licha ya kuwa Simba inawachezaji wengi wapya kwenye kikosi chao, wapo ambao tayari wameonyesha kuwaka na pengine wanaweza kuendeleza moto wao katika dabi, miongoni mwao ni pamoja na Guaye na Oura. Ni mawinga wasumbufu ambao wakipewa nafasi ya kukaa na mpira mguuni wanaweza kuwa na madhara makubwa kwa Yanga na hata kuamua mechi zote mbili na kile walichofanya katika mechi zilizopita.