Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Dabi ya Zenji ni vita ya kimbinu, ufundi


BAADA ya kelele na tambo nyingi za Wasemaji wa Simba na Yanga sambamba na zile za wapenzi na mashabiki wa klabu hizo, hatimaye muda umewadia wa kushuhudia pambano jingine la watani.


Simba na Yanga zilizobeba mhimili wa soka la Tanzania na kuangaliwa kama kioo katika ukuaji wa mchezo huo nchini, zinatarajiwa kuvaana wikiendi hii katika pambano la kwanza la Ligi Kuu Bara kwa msimu huu litakalopigwa kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, visiwani Zanzibar.

Hilo litakuwa pambano la saba kwa timu hizo kukutana visiwani humo, baada ya awali kukutana mara sita katika mechi za michuano tofauti, zikiwamo mbili za Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (sasa Kagame Cup) 1975 na 1992. Pia zilikutana mara moja katika mechi ya Ligi Kuu ya Muungano 1992 na mara tatu katika Kombe la Mapinduzi 2011, 2017 na 2021 iliyokuwa ya mwisho.

Katika mechi hizo sita zilizopita, Yanga imeshinda mara mbili, huku Simba ikitamba mara nne.

Hata hivyo, kwa mara ya saba wanayokutana ni katika Ligi Kuu Bara, mechi inayoenda kuandika historia kwa mara ya kwanza pambano la watani la Ligi ya Bara likienda kupigwa visiwani humo.

Utamu zaidi ni kwamba mechi hiyo itakayopigwa keshokutwa Jumapili kuanzia saa 2:15 usiku inazikutanisha timu zinazoonekana kutofautiana kimbinu na kiuchezaji zikiwa na makocha wapya wanaokutana kwa mara ya kwanza na kuziongoza timu katika pambano la Dabi ya Kariakoo.

Kwa wale wazee wa mikeka na wanaobashiri matokeo mapema kabla ya timu hazijashuka uwanjani, safari hii wasibeti kwa mazoea, kwani timu zote hazitabiriki kwa sasa kwa aina ya maingizo mapya ya wachezaji, hata kama zinazofautiana kimbinu, kiuchezaji na matokeo iliyonayo kwa sasa.

Pambano hili sio tu linaenda kuwapa burudani mashabiki na wapenzi wa soka wa Zanzibar, lakini huenda likafuatiliwa zaidi pengine kuliko dabi zilizopita.

Mwenyeji Yanga, anaingia katika mechi hiyo akiwa na msururu wa matokeo ya ushindi kupitia mechi sita mfululizo zilizopita, ikiwamo iliyopita ilipoifumua JKT Tanzania kwa mabao 5-0 na kuishusha kileleni na Vijana wa Pedro Goncalves kurejea kukalia kiti hicho cha uongozi wa Ligi.

Mechi ya juzi kwa Yanga ilikuwa ni ya 30 mfululizo kucheza bila kupoteza katika Ligi Kuu kwani tangu ilipofungwa mabao 3-1 na Tabora United (sasa TRA United) Novemba 7, 2024 timu hiyo haijaonja machungu, ikishinda mechi 28 na kutoka sare mbili tu dhidi ya JKT Tanzania na Mbeya City.

Yanga ya sasa chini ya Pedro imekuwa ikicheza kimbinu sana kiasi cha baadhi ya wadau kuhoji ubora wake na kuwa na shaka na uwezo wa kocha, huku wengine wakisema kiwango cha timu kimeshuka.

Hata hivyo, ukweli ni kwamba hakuna timu imekuwa ina kikosi imara katika ligi yetu kama Yanga kwa misimu kadhaa sasa na kama itabidi kupima kushuka au kupanda kwa kiwango tutaipima Yanga kwa Yanga yenyewe na si vinginevyo.

Ndio maana hata kuendea dabi hii bado katika karatasi Yanga inapewa nafasi ya kuendelea kushinda mbele ya mtani wake kutokana na kikosi kuwa pamoja na ubora wa wachezaji kitu ambacho Jumapili inapaswa kukithibitisha ukweli huo uwanjani.

Simba kwa sasa inapitia katika kutengeneza mradi wa kuirudisha kwenye ubora waliowahi kuwa nao au kuendelea pale walipoishia baada ya kupoteza mechi sita mfululizo za mashindano tofauti mbele ya watani wao hao.

Kwa sasa wanaona dabi hii ni kama mechi na muda wao muafaka na wa pekee wa kujitoa katika unyonge waliokutana nao mbele ya Yanga na hata ukiwatazama kile wanachofanya uwanjani kinatia matumaini.

Hii ni baada ya usajili wa kuboresha kikosi kupitia dirisha dogo, ambapo imeingiza wachezaji ambao moja kwa moja wameingia katika kikosi cha kwanza na kuchangia kuongeza ubora wa timu na hata ule uchezaji iliyokuwa mwanzoni mwa msimu kwa sasa umeonekana tofauti kwani ina ufanisi zaidi.

Kwa mfano tu, ongezeko la Anicet Oura pamoja na Libasse Gueye katika eneo la ushambuliaji kumeongeza ubora wa Simba na kuwa matatizo kwa timu pinzani na hata uwepo wa kocha Steve Barker umeanza kuonyesha moshi mweupe na kuibua matarajio makubwa kwa wapenzi na wanachama wa Simba, wengi wakiamini ni muda wao muafaka wa kumaliza unyonge kwa Yanga.

Hata hivyo, mbali na ubora wa kikosi katika dabi siku zote maandalizi ya kiakili yana maana kubwa sana, kitu ambacho nahisi Yanga wanakifanya vizuri na ndio kuchangia kushinda mara sita mfululizo kulinganisha na watani wao ambao wamekuwa wakivurugana kabla ya mechi kama hii. 

Nakumbuka wakati naitumikia Simba walikuwa vizuri eneo hilo, kwani viongozi walikuwa kila wakiuongelea mchezo huo kambini, walisisitiza kwamba Simba kufungwa na Yanga ni hadi watake wenyewe yaani Simba.

Ukiangalia kauli hii unaweza kuiona kama ni majigambo tu, lakini katika vichwa vya wachezaji inapokewa vizuri kama hatua ya kwanza kuondoa hofu ya mechi hiyo, mbali na ukubwa wake, wakati nikiwa Yanga nilikutana na kauli za kukata tamaa kutokujiamini kulikokuwa kunatengeneza khofu tu kuendea mchezo huo.

Kauli nyingi zilizokuwa zikitolewa wakati naitumikia Yanga ilikuwa ni; 'Safari hii hatukubali au tutauana'. Ni kweli zilikuwa ni za kusisitiza jambo, lakini kichwani mwa wachezaji haizungumzi hivyo zaidi ya kuwaondolea hali ya kujiamini mbele ya wapinzani wao.

Hata ukitazama hivi karibuni, viongozi wa Simba na kauli zao baada ya mechi utagundua hawana imani na wachezaji wao, nahisi hizi kauli nilizozitumia kama mfano zimebadilika wakati Simba wakisisitizana kwamba hawakubali, wenzao Yanga wanaambizana kufungwa labda watake wenyewe. Yaani zimekuwa kinyume na enzi nilipopita katika klabu hizo kongwe.

Yote kwa yote matarajio yangu ni kuwa Dabi ya safari hii itakuwa mechi nzuri ya ushindani kimbinu kutokana na aina ya walimu wanaofundisha timu hizo na pia tutarajie matokeo baada ya dakika 90, tusitabiri mapema hata kwa facts hizo nilizoziainisha kutokana na ukweli dabi ni dabi tu!

Kiu yangu ni kwamba natamani kushuhudia vita ya Oura v Israel Mwenda, Pacome Zouzoua v Shomary Kapombe na pale katikati ya uwanja utatu wa Simba wa Yusuph Kagoma, Clatous Chama na Inno Loemba v Duke Abuya, Maxi Nzengeli, Damaro Camara au Mudathir kwa Yanga na hii italeta burudani na vita hivyo ndivyo vitaamua pambano hilo.