Malindi SC Inavyoisaka heshima ya miaka ya ‘90
Muktasari:
- Mafanikio hayo ya Malindi SC ni kucheza hatua ya nusu fainali ya michuano ya CAF kwa miaka miwili mfululizo ilikuwa Kombe la Washindi mwaka 1994 na Kombe la CAF mwaka 1995, kwa sasa michuano hiyo haipo kutokana na kuunganishwa mwaka 2004 na kuzaliwa Kombe la Shirikisho Afrika.
UKIFIKA Zanzibar ukiulizia timu yenye mafanikio makubwa zaidi si ndani ya kisiwa hicho bali katika soka la Afrika utatajiwa Malindi SC, klabu iliyoanzishwa mwaka 1942. Hivi sasa ina miaka 83.
Mafanikio hayo ya Malindi SC ni kucheza hatua ya nusu fainali ya michuano ya CAF kwa miaka miwili mfululizo ilikuwa Kombe la Washindi mwaka 1994 na Kombe la CAF mwaka 1995, kwa sasa michuano hiyo haipo kutokana na kuunganishwa mwaka 2004 na kuzaliwa Kombe la Shirikisho Afrika.
Mbali na hilo, mwaka 1989, Malindi ilichukua ubingwa wa Zanzibar na ule wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kuweka rekodi tamu kwenye soka si tu visiwani humo, bali Afrika Mashariki.
Klabu hiyo baada ya kupitia kipindi cha mpito kwa misimu kadhaa kutokana na makali iliyokuwa nayo miaka ya 90, hivi sasa imedhamiria kurudisha makali yake kufuatia kufanya usajili mkubwa kabla ya kuanza kwa msimu huu wa Ligi Kuu Soka Zanzibar.
Miongoni mwa mastaa waliosajiliwa na timu hiyo ni waliowahi kutamba katika Ligi Kuu Bara akiwamo Said Juma Makapu aliyepita timu kadhaa kama Yanga na Ihefu, pia Benedict Haule aliyecheza Azam na Singida. Mbali na hao, kuna nyota wanaotoka nje ya Tanzania katika nchi za Guinea, Nigeria na Ujerumani.
Kusajili wachezaji wa kigeni kutoka Ulaya si mara ya kwanza, Malindi imewahi kuwa na mchezaji kutoka Bulgaria aitwaye Julian Albertov. Pia mastaa wa ndani ya Afrika imewahi kuwa nao kama Maldon Malitoli raia wa Zambia.
Nyota wengine waliowahi kuipa heshima kubwa Malindi ni kama Amour Aziz, Ali Bushir ‘Benitez’, Wazir Seif, Rashid Salim ‘Tall’, Edibily Lunyamila, Nico Bambaga, Victor Bambo na Abdul Malaika.
Tayari kikosi hicho kinachofundishwa na Kocha Mkuu, Mutyaba Joseph Harold raia wa Uganda kimeshuka dimbani katika mechi kumi za Ligi Kuu Soka Zanzibar na kukusanya pointi 17 zilizotokana na ushindi mara nne, sare tano na kupoteza moja.
Ilianza msimu kwa kucheza mechi mbili ugenini kisiwani Pemba ikishinda dhidi ya Chipukizi United bao 1-0, kisha ikatoka 0-0 na Junguni United. Ikarejea Unguja na kuichapa Fufuni 2-0.
Matokeo ya mechi zilizofuata yalikuwa hivi; Malindi 4-0 New Stone Town, JKU 1-1 Malindi, Malindi 3-0 KVZ, Malindi 0-0 KMKM, Mafunzo 0-0 Malindi, Mlandege 3-0 Malindi na Malindi 1-1 Polisi.
Ofisa Habari wa Malindi, Namala Suleiman, amefanya mahojiano maalum na Mwanaspoti akielezea mipango na mikakati ya klabu hiyo katika kuhakikisha ile heshima yao inarejea kwa kutawala soka la Zanzibar.
Katika hilo, Namala anaanza kwa kuzungumzia mechi kumi za kwanza zilivyotoa changamoto kwa kikosi chao na mwelekeo wa zijazo akisema: “Mpaka sasa timu ipo kwenye kiwango kizuri, kwasababu mwenendo unaridhisha kwa kiasi chake, mpaka sasa ukitazama ushindani wenyewe wa ligi, bado ni mgumu.
“Kwenye mechi kumi, unaweza kuona tumepoteza mechi moja, tumeshinda nne, sare tano. Baada ya ligi kutamatika mzunguko wa kwanza kwa kucheza mechi 15, itafanyika tathmini ya jumla.
WANAKWAMA?
“Unaweza kuona kuna wachezaji wengi wapya, bila shaka kutokana na maingizo hayo mapya wanaendelea kuzoeana, tathmini hiyo itakayofanyika itaonyesha maeneo ya kuboresha iwe kwa kuongeza wachezaji au jambo lingine kufanyika, na kama yatahitajika maboresho dirisha dogo sio mbali, tunaelekea huko.”
KIWANGO CHA TIMU
Kucheza mechi kumi na kukusanya pointi 17, maana yake pointi 13 zimepotea, katika hilo, Namala anasema: “Siwezi kusema kwa asilimia mia moja tumeridhishwa na kiwango cha timu bali tupo kwenye wastani, shabaha yetu sisi ni kukaa juu ya msimamo, lakini matokeo ya hivi karibuni kidogo yametupa wakati mgumu sana.
MJINI DABI IMEWATIBULIA
Kabla ya kucheza dhidi ya Mlandege katika mechi ya Mjini Dabi iliyopigwa Novemba 20, 2025, Malindi ilikuwa ndiyo timu pekee haijapoteza mechi katika ligi hiyo katika mizunguko minane. Baada ya mechi hiyo, Malindi ililala kwa mabao 3-0 na kutibuliwa rekodi yao hiyo.
Kipigo hicho kwa kiasi fulani kimeitibulia Malindi ambayo kutoka awali kushikilia nafasi za juu ikiwamo kileleni hadi kuangukia ya tano ilipo sasa.
“Mechi tuliyopoteza ilikuwa ni dabi, na dabi huwa ni mechi ya mahasimu, mechi inakuwa ngumu sana kama unavyofahamu. Kwa hiyo kwa ufupi tulizidiwa kimchezo na kiushindani, wenzetu walikuwa bora sana ingawa sisi tulitaka kushinda japo hatukufanikiwa.
“Ukiangalia tulikuwa hatujapoteza kabla ya mechi hiyo, kwa hiyo hata ile kujiamini tulikuwa tunajiamini kwa kiasi kikubwa sana. Wachezaji waliingia uwanjani kwa kujiamini wakati mpira haupo hivyo. Nadhani hivyo vilichangia kutuharibia na kupoteza ile dabi.
“Pia ukiangalia sisi tuna wachezaji wapya wengi, kati yao wawili tu ambao tulikuwa nao msimu uliopita ndio wamecheza dabi msimu huu, waliobaki wote ni wapya. Ile presha ya dabi waliikosa, hawakuwa wakiitambua hasa. Naweza kusema hilo lilichangia pia. Yote kwa yote, dabi ya msimu huu ndio bora zaidi.”
JOTO LA MJINI DABI
Kwa Zanzibar, kuna dabi nyingi, lakini ile ya Mjini inayozikutanisha Malindi na Mlandege huwa na mvuto wa aina yake.
Namala anasema: “Dabi ya Malindi na Mlandege inapokaribia joto la ushindani linakuwa kubwa sana kuanzia nje hadi ndani ya uwanja, watu wanatambiana sana, wachezaji wanataka kuona wanashinda hiyo mechi kwani wanaahidiwa vitu vingi. Kwa hiyo kila mtu anayepata matokeo mazuri anakuwa anamtambia mwenzake.
UTAWALA WAO ULIVYOKUWA
“Timu imeanzishwa mwaka 1942 na kama tunavyofahamu timu hii ina historia kubwa sana, nikikwambia historia kubwa ni kwenye eneo la mataji tunajivunia.
“Tumechukua ubingwa wa Ligi Kuu Zanzibar, pia Kombe la Muungano na mara ya mwisho mwaka 2019 tumechukua Kombe la FA, tukapata nafasi ya kushiriki michuano ya kimataifa.
“Lakini mafanikio mengine ya kujivuni tulishinda michuano ya Kombe la Hedex tulichukua mwaka 1994 na 1995.
KUPOTEA KWAO NA ZAMA MPYA
“Kuna vitu vingi vilitokea, timu ilikuwa inakosa matokeo mazuri uwanjani, lakini pia nadhani upepo mbaya nao ulikuwa umepita.
“Lakini kuwepo kwa wasimamiaji hawa wapya waliokuja kuongeza nguvu nadhani tunarudi kwenye makali yetu.
“Mpira siku hizi umebadilika, unahitaji uwekezaji mkubwa, watu waliokuja kuwekeza Malindi wamechagiza timu ionekane ya moto na kurudi kwenye ramani.
“Hapo katikati uwekezaji haukuwa mkubwa na hata Malindi ile ya zamani iliyokuwa na mafanikio ilikuwa na watu kama Naushad Mohammed Suleiman (marehemu) na wengineo kama Jeff, hakukuwa na mchezaji ambaye akitakiwa na Malindi akakosekana kwa nyakati hizo.
“Kwa hiyo Malindi ya mwaka huu imerudi tena zama za zamani, hakuna mchezaji ambaye tumemuhitaji tumemkosa. Kuna wachezaji nane wa kigeni, maana yake ni uwekezaji mkubwa umefanyika.
“Pia kuna wachezaji wengi kikosini kwetu kutoka Tanzania Bara waliofanya vizuri, kina Benedict Haule, Mkumbo na wengineo. Shafii Omar amecheza Sweden amerejea kucheza Malindi, kuna mchezaji kutoka Ujerumani Christian Noah.
“Uwekezaji huu ndiyo hapo katikati ulikosekana, lakini uwekezaji huu wa sasa na ile morali umekuja kuongeza kitu cha tofauti ndani ya Malindi hii mpya ambayo watu wanaisubiria na wamekuwa wakiisapoti kwa kiasi kikubwa.
“Hata mashabiki wamekuwa na mwamko mkubwa, mechi za dabi hapo nyuma walikuwa hawajitokezi kama ilivyokuwa msimu huu. Hiyo yote ni matunda ya uwekezaji, tuna kocha wa kigeni, Mganda naye amekuwa chagizo la timu kufanya vizuri kwa nyakati hizi tofauti na hapo awali.
NAFASI YA WAKONGWE
“Kwa bahati nzuri hivi sasa wachezaji wetu wa zamani wamejiunganisha, wana timu yao ya maveterani, tunapokuwa tunaelekea kwenye mechi muhimu wanatumika katika kuwahamasisha wachezaji, kutoa maoni na mawazo yao.
“Hata mechi dhidi ya Mlandege walitumika kushauri kitaalamu, wachezaji kama Abdulghani Msoma, Seif Odera na wengineo ni msaada mkubwa.
“Uzuri wa Zanzibar, ni sehemu ambayo watu wengi wanafahamiana kutokana na kuwa eneo sio kubwa sana, kwa hiyo watu inakuwa rahisi kukutana. Timu ikienda kwenye mazoezi wanakuja.
“Mechi iliyopita dhidi ya Mlandege, Abdul Wakat Jumaa alikuja akitokea Marekani kuja kuangalia mechi ya Dabi, ni watu wachache wenye uthubutu huo, bado anaendelea kutumika katika sehemu ya msaada wa timu.
UHUSIANO WAO NA KUNDI LA TAARABU
Namala anasema hakuna uhusiano wowote kati ya Malindi SC na Kundi la Taarab la Malindi, lakini kutokana na wote wanatokea eneo moja, ndio maana wengi wanazihisisha kuwa ndugu.
“Hakuna uhusiano wowote isipokuwa tu, sote tupo jimbo moja la Malindi ndio maana inakuwa hivyo. Watu waelewe Malindi SC na hilo kundi la taarabu hakuna uhusiano wowote wa moja kwa moja zaidi ya kutoka eneo moja.
NINI KIFANYIKE KUWA NA LIGI BORA?
“Ili kuwa na ligi bora kulinganisha na uwekezaji uliopo hivi sasa, ukiangalia wadhamini wapo, bingwa anachukua Sh50 milioni, si haba. Kipindi cha nyuma alikuwa hachukui, kwa hiyo uwekezaji umeanzia hapo.
“Kwa hiyo uwekezaji uongezwe, mpira wa miguu ni gharama, wapatikane wafadhili wengine wa kuongezea zaidi, lakini pia kuongezwa kwa thamani ya ligi iendane na thamani ya fedha yenyewe.
“Kuna waamuzi, nao wazingatiwe kwa upande wa stahiki zao, kama kuna changamoto yoyote wasikilizwe kwa umakini ili kutengenezewa mazingira mazuri.
“Kiukweli bado tupo chini, inatakiwa makampuni mengi yajitokeze, watu waje kuisapoti ligi. Kuwa na kampuni mbili za kuendesha ligi bado haiwezi kuchangia kwa kiasi kikubwa, kwa hiyo waje wadau wengine kuongeza nguvu.
“Nadhani fedha zikimwagika kwa wingi basi hata hizi changamoto ndogondogo zitapotea. Hata wachezaji watakuwa wanapata stahiki zao kwa wakati.
“Naamini hayo yatakuja kuchochea kukua kwa kasi mpira wetu wa Zanzibar kwa ujumla.
“Ligi au timu uendeshaji wa klabu ni sehemu ya kazi, sio kuja kujiburudisha. Ifikie wakati mchezaji anapokwenda uwanjani aseme anakwenda kazini, sio kujiburudisha.
“Wawekezaji wanatakiwa kuongezeka, tuliokuwa nao wanajitahidi lakini tuongeze nguvu zaidi.
UJUMBE KWA MASHABIKI WA MALINDI
“Tulipoanza msimu huu tuliwaambia Malindi Yetu, Furaha Yetu. Sasa wao waendelee kushikamana, wasituache. Tukishinda furaha ni yetu sote na ikitokea tumepoteza tuendelee kuwa pamoja.
“Malindi safari hii tumejizatiti vizuri kabisa na ukizingatia katika kila mechi mechi tunayoielekea tunakuja na kauli mbiu.
Mechi dhidi ya Mlandege tulisema ‘Hii ni Yetu’, iliyopita tulisema ‘Ijumaa ya Matumaini’, huko nyuma tushasema ‘Alama Tatu Muhimu’. Mechi dhidi ya Mwembe Makumbi tunasema ‘Hakuna Kukata Tamaa’.
“Katika hii tunawaambia Wanamalindi hakuna kukata tamaa, timu haijapoteza, tunaendelea kujipanga na tunaamini tutafanya vizuri.”
WACHEZAJI WAPYA
Said Makapu, Benedick Haule, Mathias Antony, Shafii Lumambo, Kelvin John, Mohammed Mwinchande Shaaban ‘Kwacha’, Fred Mack, Maulid Tamila, Salum Abdallah Ali, Tamtah Hussein, Lally Yusuph, Erick Paul Mwita, Ramadhan Amri, Mohamed Abdalla Ali ‘Kijeshi’, Juma Mohamed Khtaib ‘Mata’, Juma Baluna Prince, Frank Mkumbo, hawa wote ni raia wa Tanzania.
Kwa upande wa wanaotoka nje ya Tanzania kuna Tchakei Asko (Togo), Obinde Ganiyu (Nigeria), David Isaiah Edache (Nigeria), Christian Noah Kamé Ekué (Ujerumani), Mohamed Bangoura ‘Tevez’ (Guinea), Mohamed Diallo (Guinea) na Ismaël Zemga Oularé (Guinea).