Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Karabaka afichua Mpanzu na wenzake walivyomng'oa Simba

KARABAKA Pict

Muktasari:

  • Nyota huyo wa Simba anayecheza kwa mkopo JKT Tanzania alikotua msimu huu baada ya msimu uliopita kuitumikia Namungo, ameanza na moto, huku mwenyewe akifuchua kinachombeba.

UMEANGALIA orodha ya wafungaji mabao wa Ligi Kuu Bara? Bila ya shaka umeliona jina la Salehe Karabaka akiwa ndiye kinara akifunga mabao manne na kuipaisha JKT Tanzania katika msimamo wa ligi hiyo iliyoingia raundi ya tisa wikiendi hii.

Nyota huyo wa Simba anayecheza kwa mkopo JKT Tanzania alikotua msimu huu baada ya msimu uliopita kuitumikia Namungo, ameanza na moto, huku mwenyewe akifuchua kinachombeba.

Akizungumza na Mwanaspoti katika mahojiano maalumu, Karabaka amefichua maisha yake kisoka Simba na kuweka bayana aliyemng’oa klabuni kuwa ni Ellie Mpanzu na wachezaji wengine wanaocheza nafasi ya winga, huku akimtaja Alassane Kante kama ndiye aliyekuwa swahiba Msimbazi licha ya kupata ugumu katika mawasiliano.

Ndio, hakuna ubishi kwamba kuna tatizo kubwa la wazawa kujua Kiingereza kwani imekuwa ni kikwazo mbele ya nyota wa kigeni.

Hata hivyo, kuna wachezaji wachache wamekuwa wakielewa na kuzungumza Kiingereza, na Karabaka anasema licha ya ugumu wa lugha hiyo amepata bahati ya kupata rafiki ambaye amekuwa mwalimu kwake kwa kumfundisha Kiswahili.

Karabaka amemtaja kiungo mkabaji wa Simba, Alassane Kante, raia wa Senegal kuwa ndiye rafiki yake waliyejenga urafiki huo akiwa Simba na ndiye aliyemfundisha Kiswahili huku naye pia akilazimika kujifunza Kiingereza. Ebu endelea naye...!

KARAB 01

KANTE MWANA SANA

Licha ya kuzungumzwa mengi juu ya wachezaji wa ndani kushindwa kuzungumza lugha ya kigeni, kwa upande wa Karabaka amekubaliana na hilo na kuweka wazi kuwa bado wanapata nafasi ya kuzoeana na nyota wa kigeni na kujenga urafiki kama ilivyo kwake na Kante.

“Ninachokumbuka Simba baada ya kuondoka ni utani na vituko dhidi ya marafiki zangu niliokuwa nimejenga nao urafiki akiwemo Kante. Ndiye niliyemfundisha kuzungumza Kiswahili anafahamu vizuri,” anasema Karabaka.

‘’Kante ni mtu wa vituko sana Kiswahili nimemfundisha, nami najua kuongea japo sio sana hata akizungumza lugha yake ya kigeni tunaelewana hivyo hivyo tu, kwani lugha zetu za mpira zinafahamika. Nimeondoka Simba lakini urafiki wetu unaendelea.”

Anasema ni kweli lugha ngumu, lakini walikuwa wa-nae-le-wana bado wanapigiana simu, amekuwa akizungumza naye kwa njia ya ‘video call’ na wamekuwa wakiendeleza utani nje ya Simba.

KARAB 07

MPANZU KAMNG’OA SIMBA

Licha ya kuomba mwenyewe kutoka kwenda kucheza nje ya Simba kutokana na kukosa namba kikosi cha kwanza, Karabaka anaweka wazi kuwa sababu kubwa ni ubora wa wachezaji ambao walikuwa wanacheza namba yake.

“Mimi ndiye niliomba nafasi ya kutoka kwa mkopo, lengo langu ni kwenda timu ambayo naweza kupata nafasi ya kucheza mara kwa mara. Hiki kimetokea nacheza nikiwa hapa JKT Tanzania,” anasema Karabaka na kuongeza:

“Nilifanya uamuzi huo kutokana na uwepo wa wachezaji ambao walikuwa wananinyima nafasi ya kucheza kutokana na kocha kuwapa nafasi wao zaidi, lakini pia uwezo walionao.”

Karabaka anamtaja winga Ellie Mpanzu, Kibu Denis, Ladack Chasambi na Joshua Mutale kuwa ni wachezaji ambao walikuwa wanambania namba na kumfanya aombe kuondoka.

“Wachezaji hao wote ni bora. Wana uwezo mkubwa ndio, lakini kocha ndiye alikuwa na machaguo amtumie nani amuache nani sikuwa na uwezo wa kumuomba anipange mimi amuache mtu mwingine.”

KARAB 06

SIMU YA MZAMIRU

Si kila mchezaji anashtushwa na kutokuwepo kwa mchezaji fulani kambini, lakini Karabaka anamtaja Mzamiru Yassin kuwa baada ya kutomuona siku mbili tu mazoezini alinyanyua simu yake kumpigia.

‘’Sikuaga mtu zaidi ya kocha, meneja na viongozi. Wachezaji walikuwa hawafahamu ila Mzamiru ndio alikuwa mtu wa kwanza kunipigia kuniuliza niko wapi kutokana na kutoniona mazoezini,” anasema Karabaka na kuongeza:

“Simu yake ilikuwa njema sana kwangu kwani nilijihisi ni mtu mwenye bahati licha ya kukosa nafasi, lakini kuna watu walikuwa wanaona umuhimu wangu kuonekana ndani ya Simba. Nilifurahi sana na nikamwambia nimechagua kutoka kujaribu maisha mengine nje ya Simba.”

Karabaka anasema Mzamiru alimtakia kila la heri na kumwambia yeye ni mchezaji mzuri ana uwezo wa kufanya mambo makubwa ndani ya JKT Tanzania na ni timu sahihi kwake huku akimsihi apambane.

KARAB 02

NDONDO HADI KENYA

Wachezaji wengi wanaocheza Ligi Kuu Bara wamekuwa waumini wakubwa wa kucheza ndondo kama sehemu ya kujipatia kipato na Karabaka anadai kuwa anacheza sana.

“Ndondo nimecheza sana hadi kuvuka mipaka. Si unajua Kenya na Tanga unavuka mpaka unaenda na kurudi, nimeshawahi kwenda kucheza ndondo Kenya baada ya kurudi kuchenji fedha niliyoipata nikajikuta nina Sh200,000 hii ndio fedha yangu kubwa tangu nimeanza kucheza,” anasema. “U-kiondoa hiyo ya bei ghali zaidi nimeshacheza ndondo ya kiushkaji nikalipwa Sh80,000. Licha ya kutajwa kuwa ni mechi mbaya hasa kwa wachezaji ambao wamesajiliwa timu zinazoshiriki ligi, mimi binafsi naamini ni sehemu ya kujiweka fiti kwani hizo mechi mara nyingi zinachezwa muda wa mapumziko.”

Kuhusu kuumia Karabaka anasema mchezaji anaweza kuumia akiwa hata katika mazoezi binafsi hivyo suala hilo ni mipango ya Mungu hakuna mtu anapanga kupata shida kisa tu anacheza mechi nje ya timu iliyomwajiri.

KARAB 05

BRYSON, KAPOMBE WANAKABA

Mabeki mara nyingi wanalia na washambuliaji wenye kasi kuwa wamekuwa wakiwalaza na viatu, lakini Karabaka analia na mabeki wa pembeni kuwa ni sehemu ya kikwazo kwake anapokutana nao uwanjani hasa wakiwa na kasi ya kupanda na kushuka haraka kusaidia mashambulizi.

“Nimekutana na mabeki wengi, lakini Bryson kwangu ni bora ni beki ambaye hakubali kushindwa anakaba kwa akili na nguvu sio rahisi kumpita bila  kuwa na maarifa,” anasema na kuongeza:

“Pia kuna Shomari Kapombe huyo ni balaa sijakutana naye mechi za ushindani mazoezini tu, lakini alikuwa ananikimbiza sana sijapata nafasi ya kucheza naye nikiwa mpinzani wake sijui itakuwaje lakini tayari ameshanionyesha ubora uwanja wa mazoezi.”

KARAB 04

GAMBA ALINIPOKEA

Ni msimu wa kwanza wa Karabaka kucheza JKT Tanzania akijiunga na timu hiyo mwanzoni mwa msimu, na mwenyewe anadai amekuwa mwenyeji kutokana na kukutana na mchezaji ambaye wamecheza pamoja JKU.

“Rashid Gamba ndiye aliyenipokea JKT Tanzania na kabla hata sijatua hapo alipata tetesi kuwa naweza kujiunga na timu hiyo, alinipigia na kunikaribisha kwa kuniambia ni sehemu sahihi.

“Mara baada ya mambo kwenda kama yalivyopangwa nilipokewa na Gamba. Nafurahi kukutana naye tena kwani tumecheza pamoja JKU ya Zanzibar, amenitia moyo na kuniambia kuwa kila kitu kinawezekana tunaweza kuwa bora ndani ya hii timu.” anasema Karabaka ambaye anamtaja Harmonize kuwa ndiye msanii wake bora.

KARAB 03

SHEKHAN ANAJUA SANA BOLI

Ni nadra kwa wachezaji ambao wamecheza timu watani za Simba na Yanga kusifiana au kukubali uwezo wa moja ya timu kati ya hizo, mfano mmoja akiwa Simba akakubali uwezo wa mchezaji wa Yanga hasa wazawa kwa Karabaka imekuwa tofauti.

“Nimecheza pamoja na Shekhan JKU ni mchezaji mzuri, ana uwezo wa kufanya vizuri ndani ya kikosi cha Yanga kama ataendelea kuaminiwa. Nimecheza naye na tulitoka pamoja kipindi mimi naenda Simba yeye alienda Yanga,” anasema Karabaka.

“Shekhan ni mpambanaji anaipenda kazi yake, hivyo sio rahisi kukubali kushindwa. Hilo kila mmoja analiona akiwa na Yanga licha ya kutopata nafasi ya kucheza mara kwa mara akipata nafasi anaonyesha uwezo mkubwa.”

Anasema Shekhan ana nidhamu kubwa uwanjani na nje ya uwanja akiwa anapenda zaidi kuwa bora na mchezaji mkubwa siku zote kwani amekuwa akipambana bila kuchoka.