Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Makosa yanayofanywa katika uvaaji wa suti

Muktasari:

  • Kibaya zaidi, wengi wanafikiri ukishavaa suti basi tayari wewe ni mtu wa class. Kumbe suti nayo inahitaji akili ya kuivaa. Si kila koti jeusi na suruali nyeusi vinaendana, si kila kiatu kinafaa kuingia kwenye suti, na si kila anayefunga tai anapaswa kuitwa “smart”. Wengine wanavaa suti halafu wanachomekea soksi za rangi ya chungwa au viatu vilivyochoka mpaka vinaonekana vinaomba kupumzishwa.

UKWELI usemwe, kuna watu wanavaa suti lakini badala ya kuonekana wana mvuto, wanaonekana kama wamechomekwa tu kwenye mavazi ya harusi. Unamkuta mtu amevaa suti ya milioni, lakini akitembea unaona kabisa hajui hata maana ya kuivaa. Makoti mengine yanabana mpaka vifungo vinataka kulia, suruali zimebeba miguu yote kama za mazoezi, huku wengine wakitembea na tai kubwa kama pazia la dirishani.

Kibaya zaidi, wengi wanafikiri ukishavaa suti basi tayari wewe ni mtu wa class. Kumbe suti nayo inahitaji akili ya kuivaa. Si kila koti jeusi na suruali nyeusi vinaendana, si kila kiatu kinafaa kuingia kwenye suti, na si kila anayefunga tai anapaswa kuitwa “smart”. Wengine wanavaa suti halafu wanachomekea soksi za rangi ya chungwa au viatu vilivyochoka mpaka vinaonekana vinaomba kupumzishwa.

CHAGUA SIZE YAKO

Kosa kubwa ambalo watu wengi hulifanya ni kuvaa suti kubwa sana au ndogo kupita kiasi. Baadhi ya watu wanasema suti inapokuwa kubwa huonekana kama imeazimwa, huku ndogo ikifanya mwili kuonekana kubanwa na kupoteza mvuto.

Mabega ya suti yanapaswa kukaa sawasawa na ya mvaaji bila kulegea. Mikono ya koti nayo inatakiwa kuishia karibu na kifundo cha mkono ili shati lionekane kidogo. Suruali nayo inapaswa kukaa vizuri bila kubana sana au kulegea kupita kiasi.


ZINGATIA VIATU

Viatu vina mchango mkubwa katika kukamilisha muonekano wa suti. Watu wengi huvaa viatu vya michezo au vilivyochakaa pamoja na suti nzuri, jambo ambalo huharibu kabisa mwonekano.

Kwa kawaida suti nyeusi huendana vizuri na viatu vyeusi, huku suti za rangi ya dark blue au kijivu zikiweza kuvaliwa na viatu vya kahawia au vyeusi. Pia viatu vinapaswa kuwa safi na kung’arishwa muda wote.


KUFUNGA VIFUNGO VIBAYA

Wanaume wengi hawajui namna sahihi ya kufunga vifungo vya koti la suti. Kwa suti yenye vifungo viwili, kifungo cha juu pekee ndicho hufungwa wakati wa kusimama, huku cha chini kikibaki wazi.

Kwa suti yenye vifungo vitatu, kifungo cha kati ndicho muhimu zaidi. Kufunga vifungo vyote kunaifanya suti ionekane ngumu na isiyo na mtindo mzuri.


RANGI NA TAI

Baadhi ya watu wanasema mchanganyiko mbaya wa rangi ni kosa linalofanywa mara kwa mara. Wengine huvaa suti yenye rangi kali kisha wakaunganisha na shati au tai yenye rangi zinazogongana.

Rangi salama zaidi kwa suti ni nyeusi, dark blue, kijivu na kahawia. Shati jeupe au la blue hafifu huendana na karibu kila aina ya suti. Tai nayo inapaswa kuwa ya rangi inayokamilisha muonekano badala ya kushindana na mavazi mengine.

Ncha ya tai inapaswa kufika karibu na mkanda wa suruali. Pia fundo la tai linapaswa kuwa safi na lenye mpangilio mzuri. Tai yenye michoro mingi kupita kiasi inaweza kuharibu muonekano wa suti.


UREFU WA SURUALI

Suluari ndefu sana au fupi kupita kiasi ni kosa jingine linaloharibu muonekano wa suti. Watu wengine huacha suruali ikikusanyika chini kwenye viatu, jambo linalofanya waonekane wasio nadhifu.

Suluari ya suti inapaswa kuishia vizuri juu ya kiatu bila kukunjamana sana. Urefu sahihi huongeza mvuto na kuifanya suti ionekane ya kisasa zaidi.

USIPUUZIE HIVI

Watu wengi hudharau vitu vidogo kama mkanda, saa, soksi au leso ya mfukoni, wakati navyo vina mchango mkubwa katika mtindo wa suti.

Mkanda unatakiwa kulingana na rangi ya viatu. Soksi zinapaswa kuwa ndefu kiasi cha kutofanya ngozi ionekane unapokaa. Saa nzuri na leso ya mfukoni vinaweza kuongeza mvuto mkubwa wa muonekano.