Makambo: Mzee wa Kuwajaza asiyeisahau Yanga

Muktasari:
- Aliwahi kufanya hivyo mshambuliaji wa zamani wa Yanga Fiston Mayele msimu wa 2021/22 akimaliza mfungaji wa pili nyuma ya George Mpole akiwa Geita Gold, uliofuata (2022/23) akawa kinara wa mabao 17 sawa Said Ntibazonkiza ‘Saido’ akiwa Simba.
KATI ya vitu anavyotamani kuvifanya mshambuliaji wa Tabora United, Heritier Makambo ni kuifikia ama kuivunja rekodi ya mabao 17 aliyoyafunga Ligi Kuu Bara msimu wa 2018/19, ingawa anakiri siyo jambo jepesi ila linawezekana.
Aliwahi kufanya hivyo mshambuliaji wa zamani wa Yanga Fiston Mayele msimu wa 2021/22 akimaliza mfungaji wa pili nyuma ya George Mpole akiwa Geita Gold, uliofuata (2022/23) akawa kinara wa mabao 17 sawa Said Ntibazonkiza ‘Saido’ akiwa Simba.
Makambo anasema msimu wake wa kwanza kucheza Yanga akitokea FC Lupopo ya nchini kwao DR Congo, ulikuwa wa mafanikio makubwa hadi akapata dili la kujiunga na klabu ya Horoya ya Guinea.
Mwanaspoti limefanya mahojiano na Makambo na anasema mashabiki ni kipimo sahihi kwa mchezaji kumuonyesha kiwango chake kimepanda ama kimeshuka kwani ni shuhuda wa hilo “Wakati nafanya vizuri Yanga mashabiki wamenipa sana pesa tena nyingi ingawa siwezi kutaja ni kiasi gani.”
“Nakumbuka wakati naondoka Yanga mashabiki walitamani niendelee kusalia ndiyo maana baada ya kurejea mara ya pili, bado walinipokea kwa moyo mmoja, hawakuwahi kuacha kunisapoti nyakati ngumu na zenye furaha, hilo lilinifunza kujua mashabiki wa Tanzania wanavyopenda soka,” anasema.

SOKA BORA
Anasema katika Afrika ukitaja nchi ambazo zimeendelea kisoka Tanzania ni miongoni mwao, akiamini hiyo ndiyo sababu ya wachezaji kutoka mataifa mbalimbali kupata mvuto wa kuja kuchezea timu mbalimbali.
Kwa upande wake anapenda jinsi Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) linavyosimamia suala la viwanja, jambo linalosaidia usalama wa wachezaji wanapotimiza majukumu yao.
“Ndiyo maana mtu akiniuliza utofauti wa wachezaji wazawa na wageni binafsi sijaona, isipokuwa kila mchezaji ana namna yake anavyoyachukulia mambo yanayoweza yakamtafsiri ni nani katika kazi yake, ishu hapo ni bidii ya mazoezi na nidhamu binafsi ya mtu.”
Makambo ambaye nje ya uwanja anapenda kusoma vitu mbalimbali kwa njia ya mitandao na vitabu, anasema baada ya kurejea kwa mara nyingine Yanga msimu wa (2022/23) akitokea Horoya hakufanya vizuri, akajikuta anakuwa na msongo wa mawazo ila wachezaji wenzake walikuwa wanampa nguvu , Djuma Shabani, Jesus Moloko na Yacouba Songne.
“Wakati narejea Yanga kwa mara ya pili mashabiki walitarajia vitu vikubwa kutoka kwangu kwa bahati mbaya sikukata kiu yao, kusema ukweli kilikuwa kipindi kigumu kwangu, ila nashukuru wachezaji wenzangu walinisaidia kuhakikisha sikati tamaa, huwa inatokea kwa wachezaji wengi kuwa na vipindi vya kung’ara na kushuka,” anasema.

WAZAWA ANAOWAKUBALI
Anasema kuna wachezaji wengi wazawa wanaofanya vizuri na wana vipaji vikubwa, baadhi anaowataja ni Kelvin Yondan, Erasto Nyoni, Ibrahim Hamad Bacca, Ibrahim Ajibu, Mohamed Hussein ‘Tshabalala’, Dickson Job na Feisal Salum ‘Fei Toto’.
“Tanzania ina vipaji vikubwa vya soka, kuna wachezaji wengi sana ninaowakubali hao ni baadhi tu, wengine nacheza nao Tabora United,” anasema Makambo anayewataja Andrew Vicent ‘Dante’ na Paul Godfrey ‘Boxer’ ndio waliomfundisha kuzungumza Kiswahili.

DABI ILIYOMUUMIZA
Anasema dabi ya Februari 16, 2019 Yanga 0-1 Simba ilimuumiza, mshindani wake Meddie Kagere alifunga kwa kichwa dakika ya 71 akiunganisha krosi ya John Bocco, hivyo ikawa utawala wa mashabiki wa Wanamsimbazi kutetema, huku wafuasi wa Jangwani wakiwa wamepoa.
“Nakumbuka nilikosa kuitumia nafasi vizuri kwa mpira uliokuwa umemshinda beki Pascal Wawa na kipa Aishi Manula, kama unavyojua jinsi ambavyo mashabiki wanatambiana hivyo ikawa wiki mbaya kwa upande wangu, ingawa walikuwa wananipa moyo ndio mpira niendelee kukaza buti,”anasema.
Lakini mechi iliyomfurahisha ya dabi ni Yanga ilishinda mabao 2-1 na Simba ilianza kufunga kupitia kwa Pape Ousman Sakho, yakasawazishwa na Fiston Mayele dakika ya 50 na 81, Agosti 13, 2022 Uwanja wa Benjamin Mkapa.
MALENGO YAKE
“Kwa sasa ni ngumu kuzungumza chochote nimeamua kuiweka akili yangu katika kazi, uwezo wangu wa uwanjani uwe na nguvu kuliko maneno.”
KABLA YA KUJA YANGA
Anasema kabla ya kujiunga Yanga msimu wa 2018/19 alipitia changamoto ngumu ambayo ilitaka kumuondoa katika ramani ya soka kipindi hicho alikuwa akiichezea FC Lupopo (2018), lakini anasisitiza itabakia kuwa siri yake hadi pale moyo wake utakapokuwa tayari kusimulia kilichompata.
“Moyo wangu bado unakumbuka maumivu hayo, sipendi kuongelea ilikuwa ni kitu gani, ila changamoto hiyo ndio sababu ya kuivaa jezi namba 19 hadi leo, hivyo kujiunga na Yanga kukanirejesha katika mstari wa kuzipigania ndoto zangu,” anasema.
Mbali na hilo anasema maisha yake Tabora United ni mazuri yanamfanya awajibike uwanjani kwa moyo wa kujitoa,

UJAZO ULIANZIA CHUMBANI
Msimu 2018/19 alifikisha mabao 17 kiwango chake kilikuwa juu, hivyo staili yake ya ushangiliaji ya kupiga makofi ya ujazo ilikuwa maarufu kwa kipindi hicho, ukisikia makofi unajua tayari kacheka na nyavu.
Anasimulia ilipoanzia staili hiyo, Septemba 18, 2018 Yanga ilikuwa inajiandaa na mechi dhidi ya Coastal Union siku inayofuata, hivyo wakati yupo chumbani akawa anajaribisha staili mbalimbali akaona ya kupiga makofi inafaa zaidi.
“Mechi tulicheza Septemba 19 Uwanja wa Taifa kwa sasa unatambulika kama Benjamin Mkapa, tulishinda bao 1-0 nilifunga mimi na ndiyo lilikuwa bao langu la kwanza, nikaanza kushangilia kwa kupiga makofi nikaona mashabiki wameipokea kwa ukubwa, mechi zilizofuata nilikuwa nikifunga wao ndio walikuwa wanaanza kupiga makofi.
Anaongeza: “Nakumbuka msimu huo mimi na Meddie Kagere ndio staili zetu zilivuna zaidi kutokana na muendelezo wa kufunga ambao tulikuwa nao, nilichojifunza ukifanya vizuri staili ambayo utawaonyesha mashabiki zako wataiungana mkono kwa asilimia 100 ili mradi isiwe ya matusi.”