Maisha yameenda kasi kwa Sven Vandenbroeck

MAISHA yameenda kasi kwa Kocha Sven Vandenbroeck. Aliyekuwa kocha wa Simba. Ghafla kwa sasa ni kocha wa klabu maarufu ya FAR Rabat ya Morroco. Ni miongoni mwa klabu kubwa zaidi nchini Morocco ikiwa inaongoza kwa kutwaa mataji. Ina mataji ya jumla 29.

FAR Rabat ndio klabu yenye mafanikio zaidi katika soka la Morocco kwa karne ya 20. Kwa rekodi wametwaa mataji 12 ya Ligi Kuu ya Morocco. Mwaka 1985 walitwaa ubingwa wa Afrika. Mwaka 2005 ilitwaa Kombe la Shirikisho Afrika. Wana mataji mengi. Hata Super Cup wamewahi kutwaa.

Kifupi Sven ametoka katika klabu ndogo Afrika amekwenda katika klabu kubwa. Kifupi ni kwamba Sven hata angetoka Yanga au Azam bado angekuwa amekwenda katika timu kubwa zaidi. Ukubwa wa timu ni mataji. Lakini hata kama unaamini ukubwa wa timu ni bajeti pamoja na huduma zilizopo klabuni bado FAR Rabat ni klabu kubwa kuliko Simba, Yanga au Azam.

Sven ametuacha midomo wazi kidogo. Kwanini? Bado kulikuwa na hisia tofauti kuhusu uwezo wake pale Msimbazi. Asikudanganye mtu. Kabla ya msimu huu kuanza Sven alikuwa hana uhakika kama atakuwa kocha wa Simba. Kilichomuokoa ni namna ambavyo Simba walitwaa mataji mawili mwishoni mwa msimu uliopita.

Awali ilitajwa kwamba kama Simba wangefungwa na Yanga katika pambano la nusu fainali za FA msimu uliopita basi Sven angeonyeshwa mlango wa kutokea. Hii ilitokana na kichapo cha awali ambacho Simba walikuwa wamepokea katika ligi kupitia kwa Bernard Morrison. Simba hawakumtazama vema Sven baada ya kichapo kile. Pambano lile la nusu fainali Sven aliruka mtego baada ya Simba kuibamiza Yanga mabao 4-0, huku wakicheza kandanda safi. Baada ya hapo Sven aliwekewa mtego wa kushindwa kuvuka kuelekea hatua ya makundi. Lakini ghafla amevuka.

Kulikuwa na sintofahamu kwa sababu baada ya pambano dhidi ya Platinum ilitazamiwa Sven afukuzwe kama timu ingeshindwa kuvuka. Lakini ghafla ikavuka na ikatangazwa kwamba Simba imeachana na Sven. Pale ilitokea sintofahamu kiasi kwamba watu wengine walizusha tu kwamba Simba imeamua kuachana na Sven kwa sababu inahitaji kocha imara zaidi hatua ya makundi. Uongo umejitenga kando na juzi Sven ametambulishwa kuwa Kocha Mpya wa FAR Rabat. Kuna maswali mengi yanaibuka nyuma yake. Kwa kila kilichotokea, watu wa Simba na mashabiki ambao wengine walikuwa hawaridhiki naye wanajisikiaje?

Huku kwa vigogo wa Simba kuna watu nawafahamu ambao walikuwa hawaridhiki na kocha kwa sababu ya misimamo yake. Kama unavyojua mabosi wetu wa soka. Wanapenda mtu ambaye watamuendesha. Sven hakuwa kocha wa namna hii.

Kwa upande wa mashabiki, wengi walikuwa hawana hoja za msingi. Walikuwa wanamshutumu kocha kwa mfumo wake wa kushambulia akitumia mshambuliaji mmoja. Alipendelea zaidi kumtumia, John Bocco lakini wao walitaka atumie washambuliaji wawili.

Ilikuwa ni hoja hafifu kwa sababu mara nyingi iliibuka pale tu ambapo Simba wangekosa matokeo uwanjani. Pindi ambapo Simba wangepata sare au kufungwa basi Sven alikuwa anashutumiwa kwa kupanga mshambuliaji mmoja. Zipo nyakati ambazo Simba ilishinda mabao mengi huku ikiwa na mshambuliaji mmoja tu mbele lakini mashabiki walikuwa wanakaa kimya. Kwa mfano, katika pambano dhidi ya Platinum majuzi, Simba walitumia washambuliaji wote watatu katika nyakati tofauti. Chris Mugalu alianza, akatoka akaingia, Meddie Kagere ambaye naye aliumia akatoka akaingia Bocco. Hakukuwa na muda ambao washambuliaji wote walikaa pamoja uwanjani lakini Simba ilishinda 4-0.

Sven hakutazamana na mashabiki vizuri kwa sababu hii tu, lakini ukweli ni kwamba Simba waling’ara katika kipindi chake pengine kuliko muda wowote ule katika miaka ya karibu. Na hapo ndipo lilipozuka jina la ‘pira biriani’. Hata hivyo mashabiki walikuwa wanapeleka sifa kwa mastaa kina Clatous Chama na sio Sven. Inachekesha sana.

Nadhani ni katika muda huu huu ambao Simba walikuwa bize kusifia wachezaji, FAR Rabat wao walikuwa bize kuchunguza ubora wa kocha. Haiwezekani tu kwamba wamchukua bila ya kuitazama Simba ikicheza, huku ikionyesha ubora wake. Kuna mahala walikuwa wanaitazama Simba na kocha wao akawakosha. Hili ni fundisho kwa mashabiki na viongozi wetu. Sikuwahi kumkosoa Sven kwa sababu mara zote ambao Simba walikuwa wanacheza, bila ya kujali matokeo ya aina yoyote ile, lakini wao ndio walikuwa wanakuwa timu bora uwanjani.

Kitu kingine cha kuchunguza ni namna gani Simba ilijiandaa kuachana na Sven. Kuna mambo mawili hapo. Simba wamelipwa chochote na FAR Rabat kama Sven bado alikuwa na mkataba nao? Nadhani alikuwa na mkataba naye.

Kitu kingine ni namna gani ambavyo Simba inaweza kujipanga kwa haraka kumpata kocha ambaye atawapitisha katika bonde la mauti. Kundi lao ni bonde la mauti. Mechi zao zote sita hazitakuwa rahisi. Hili nitalizungumza kwa upana na marefu kesho.

Imeandikwa na EDO KUMWEMBE