Sven amewapa makocha wetu mambo matatu

Alhamisi iliyopita, Simba na kocha Sven Vandenbroeck walifikia makubaliano ya kusitisha mkataba wa miaka miwili wa Raia huyo wa Ubelgiji aliyejiunga na timu hiyo Disemba, 2019.

Uamuzi huo ulifikiwa ndani ya muda wa saa 24 baada ya kocha huyo kutoka kuiongoza Simba kutinga hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu baada ya kuitoa FC Platinum ya Zimbabwe kwa ushindi wa jumla wa mabao 4-1.

Ingawa taarifa rasmi ya klabu ya Simba haikueleza sababu hasa zilizopelekea wafikie makubaliano hayo, siku moja baadaye, kocha huyo aliandika katika kurasa zake za mitandao ya kijamii akidai kuwa alihitaji kuwa karibu zaidi na familia yake ambayo inaishi huko Ubelgiji.

Lakini katika hali ya kushangaza, Jumamosi, kulisambaa picha zinazomuonyesha kocha huyo akisaini mkataba unaotajwa kuwa na urefu wa miaka miwili wa kuifundisha timu ya FAR Rabat ya Morocco ambayo ni miongoni mwa timu kubwa nchini humo.

Limekuwa ni jambo la kushtusha kwa Simba hasa ukizingatia kwamba kocha huyo ameondoka katika kipindi kigumu ambacho Simba imebakiza muda wa mwezi mmoja kabla ya kuanza hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu ambayo wamepangwa katika kundi na timu ngumu ambazo ni Al Ahly, AS Vita na El Merrikh.

Kuanzia alipoanza kuinoa Simba hadi sasa alipondoka na kujiunga na FAR Rabat, Sven Vandenbroeck kuna mambo matatu ya msingi kutoka kwake ambayo makocha wazawa hapa nchini wanapaswa kujifunza.

Jambo la kwanza ni kusimamia kile anachokiamini kuanzia masuala ya kiufundi na yale ya kiutawala ambayo yako chini ya usimamizi wake.

Kwa muda mrefu Sven alikuwa akilaumiwa kwa masuala mbalimbali ya kiufundi na mashabiki, waandishi na wachambuzi wa soka juu ya upangaji wa kikosi na baadhi ya mbinu zake lakini alibakia kuamini katika kile alichokifikiria na kukipanga pasipo kufanya kile walichokitaka wakosoaji wake.

Mfano wa hilo ni muendelezo wake wa kutumia mfumo wa 4-2-3-1 ambao unatoa fursa ya uwepo wa mshambuliaji mmoja tu wa kati kikosini huku wachezaji katika idara ya kiungo wakiwa watano ambao wengi walikuwa hawapendezwi nao wakidai unainyima fursa timu hiyo kupata idadi kubwa ya mabao.


Lakini Sven aliendelea kushikilia msimamo wake na kuendelea kutumia mshambuliaji mmoja tu wa kati ambaye mara kwa mara alikuwa ni nahodha John Bocco licha ya kulazimishwa mara kwa mara kumtumia mshambuliaji kipenzi wa timu hiyo, Meddie Kagere.

Kingine ambacho makocha wetu wazawa wanapaswa kujifunza kutoka kwa Sven ni utayari na ujasiri wa kufanya kazi katika mazingira mapya na kukabiliana na changamoto kubwa zaidi ya uzoefu walionao.

Ukifuatilia wasifu wa Vandenbroeck utaamini kwamba ni kocha ambaye siku zote amekuwa na kiu ya kufanikiwa zaidi na haogopi kukabiliana na changamoto mpya licha ya kutokuwa na jina kubwa katika taaluma ya ukocha.

Alianzia kuwa mtathmini wa mechi katika benchi la ufundi la timu ya Taifa ya Cameroon ambayo ilitwaa taji la Mataifa ya Afrika (Afcon) mwaka 2017 lakini baada ya hapo alijitosa kuwania fursa ya kuifundisha timu ya taifa ya Zambia licha ya kutowahi kuwa kocha mkuu hapo kabla.

Kujaribu kwake kulimsaidia kwani alifanikiwa kupata fursa hiyo na hata alipoamua kuachana na Zambia, hakuhofia kuomba kazi Simba na baada ya hapo ameweza kujitengenezea thamani kama mmoja wa makocha wakubwa Afrika.

Simba ikiwa ni klabu yake ya kwanza kuifundisha, Sven ameiongoza kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu, Kombe la Shirikisho la Azam, Ngao ya Jamii na kubwa zaidi ameiongoza kutinga hatua ya makundi ambayo ndio ilikuwa lengo kuu la mashabiki na uongozi wa timu hiyo msimu huu.

Hapana shaka kwamba leo hii Sven anaondoka Simba na kujiunga na FAR Rabat akiwa shujaa na ameweza kuandika jina lake katika kitabu cha historia ndani ya klabu hiyo kama mmoja wa makocha waliofanikiwa zaidi licha ya wengi kuwa na shaka naye alipojiunga nao.