MABOSI: Wanamichezo 50 tajiri zaidi duniani mwaka huu ukifungwa!
Muktasari:
- Kuna mtazamo kwamba wachezaji wa Ligi ya Kikapu Marekani (NBA), ni wanamichezo wanaolipwa zaidi duniani. Ondoa shaka. Soma jinsi kila mwanamichezo anavyogeuza ubora wake uwanjani kuwa mapato makubwa. Hii ndiyo orodha ya wanamichezo 20 matajiri zaidi duniani mwaka huu ukiwa umebakiza wiki chache kumalizika.
MIAMI, MAREKANI: SANAA, burudani na michezo inalipa. Wanasoka, wacheza gofu, tenisi na mabondia wote hupata malipo manono katika ulimwengu wa sasa. Lakini, nani anaongoza orodha ya matajiri kati yao duniani?
Kuna mtazamo kwamba wachezaji wa Ligi ya Kikapu Marekani (NBA), ni wanamichezo wanaolipwa zaidi duniani. Ondoa shaka. Soma jinsi kila mwanamichezo anavyogeuza ubora wake uwanjani kuwa mapato makubwa. Hii ndiyo orodha ya wanamichezo 20 matajiri zaidi duniani mwaka huu ukiwa umebakiza wiki chache kumalizika.
1. Michael Jordan (Dola 3.6 bilioni)
Jordan ni mcheza kikapu mstaafu aliyeng'ara kati ya 1984–2003 akiwa na Chicago Bulls na Washington Wizards akitajwa kuwa staa aliyetisha kwenye mchezo huo karne iliyopita. Kwa sasa ni mmoja wa wamiliki wenye hisa katika timu ya Charlotte Hornets, balozi wa bidhaa na mfanyabiashara mwenye utajiri wa Dola 3.6 bilioni.
2. Vincent McMahon (Dola 3.2 bilioni)
Vince McMahon ni promota wa mieleka, mchambuzi wa mchezo huo, mtayarishaji wa filamu aliyejulikana zaidi kama bosi wa Shirikisho la Mieleka Duniani (WWE) kabla ya kustaafu.
3. Ion Tiriac (Dola 2.4 bilioni)
Huyu ni mfanyabiashara kutoka Romania na mchezaji wa zamani wa tenisi na mpira wa magongo aliyepata mafanikio makubwa kibiashara baada ya kustaafu.
4. Junior Bridgeman (Dola 1.5 bilioni)
Ni mchezaji wa zamani wa NBA na mfanyabiashara wa migahawa ya chakula (fast food). Alifariki dunia Machi 11, 2025 akiwa na umri wa miaka 71, lakini mkwanja alioutengeneza unaendelezwa na familia yake kwa jina lake.
5. Cristiano Ronaldo (Dola 1.2 bilioni)
Nahodha wa Ureno na timu ya Al Nassr ya Ligi Kuu Saudi Arabia (Pro League), Ronaldo ametengeneza utajiri wake kutokana na bishara mbalimbali zinazotumia chapa ya R7, ubalozi wa kampuni mbalimbali, mapato ya mikataba ya uchezaji, matangazo na ubia wa kibiashara na wafanyabishara wakubwa. Amezichezea timu za Sporting CP, Manchester United, Real Madrid, Juventus na sasa Al Nassr. Alifikia hadhi ya ubilionea Juni mwaka huu.
6. Anna Kasprzak (Dola 1 bilioni)
Huyu ni mwendesha farasi maarufu katika mashindano makubwa duniani, ambapo shuguli zake nyingi za kibiashara amewekeza nchini kwao Denmark.
7. Lionel Messi (Dola 850 milioni)
Anachukuliwa kuwa mmoja wa wanasoka bora zaidi duniani katika historia akiwa amechezea Barcelona, PSG na sasa Inter Miami. Muargentina huyu ni mfanyabiashara na utajiri wake mkubwa umetokana na mikataba minono ambayo amekuwa akisaini na kampuni mbalimbali duniani zinazotumia jina na sura yake. Ukwasi wake mwingi aliutengeneza akiwa Barcelona alikocheza kwa miaka 18 mfululizo.
8. LeBron James (Dola 800 milioni)
Ndiye staa maarufu kwa sasa wa Ligi ya Kikapu Marekani (NBA) na mfanyabiashara aliyewekeza fedha nyingi kwenye masoko ya mitaji nchini humo. Akiwa na umri wa miaka 40 bado anacheza kikapu kwa kiwango cha juu akiichezea Los Angeles Lakers. Kabla ya kutua hapo alizichezea Cleveland Cavaliers na Miami Heat. Mafanikio uwanjani ni pamoja na kubeba ubingwa mara nne (2012, 2013, 2016, 2020), MVP Olimpiki (2024), NBA All-Star Game MVP (2006, 2008, 2018) na kuchaguliwa katika vikosi vya All Star tangu alipoanza kikapu 2003.
9. Magic Johnson (Dola 800 milioni)
Huyu ni staa wa zamani wa NBA na mfanyabiashara mwenye mafanikio aliyewekeza kwenye biashara za supermarket na vyakula nchini Marekani na kwenye nchi mbalimbali za Ulaya. Alicheza kikapu kati ya 1979–2000 akitumia muda mwingi Los Angeles Lakers ingawa kwa muda mfupi aliichezea Magic M7 Boras ya Sweden.
10. Dwayne Johnson (Dola 800 milioni)
Mwamba ni mcheza mieleka wa kulipwa wa zamani ambaye kwa sasa ni mwigizaji wa filamu za kivita na mjasiriamali.
11. Tiger Woods (Dola 800 milioni)
Unapoutaja mchezo wa gofu huwezi kuacha kulitaja jina la Tiger Woods ambaye katikati ya miaka ya 1990 na 2000 alitengeza utajiri mkubwa kutokana na malipo aliyokuwa akilipwa ya kati ya Dola 50 milioni hadi 60 milioni kwa mwaka. Licha ya misukosuko ya ndoa aliyokumbana nayo miaka michache iliyopita iliyomlazimu kutalikiana na mkewe Elin Nordegren pamoja na majeraha, amebaki kuwa mmoja wanamichezo matajiri duniani.
12. Roger Federer (Dola 750 milioni)
Huyu ni mcheza tenisi wa kulipwa mstaafu na mojawapo wa mastaa bora kabisa wa mchezo huo katika historia duniani. Kwa sasa anafanya shughuli zake huko kwao Uswisi, lakini biashara zake nyingi ni za ubia.
13. Eddie Jordan (Dola 600 milioni)
Aliwahi kuwa mtendaji mkuu wa mchezo wa mbio za magari wa Ireland, mtangazaji, dereva wa mbio hizo na mfanyabiashara.
14. Michael Schumacher (Dola 600 milioni)
Dereva wa zamani wa Formula One, mmoja wa mastaa wachache waliopata zaidi ya Dola 1 bilioni enzi zake akipiga mzigo. Kabla ya kustaafu 2012, Schumacher alikuwa mahiri kazini akifanikiwa kubeba ubingwa wa mashindano hayo mara saba (1994, 1995, 2000, 2001, 2002, 2003 na 2004). Kwa sasa hajitambui kitandani tangu 2013 alipopata ajali Desemba 29, 2013 katika mchezo wa kuteleza kwenye barafu milima ya Dent de Burgin huko Ufaransa. Tangu wakati huo hajawahi kuzinduka, lakini uwekezaji wake unaendelea kumuingizia fedha.
15. Shaquille O'Neal (Dola 500 milioni)
Ni miongoni mwa wachezaji bora na maarufu zaidi kwenye historia ya NBA aliyezichezea timu sita (Orlando Magic, Los Angeles Lakers, Miami Heat, Phoenix Suns, Cleveland Cavaliers na Boston Celtics. Kama ilivyo kwa Michael Jordan na LeBron James, O'Neal ni mmoja wa mastaa waliotwaa ubingwa mara nyingi (nne 2000–2002 na 2006). Pia aliwahi kuwa MVP wa fainali za NBA mara tatu (2000–2002). O'Neal alistaafu akiwa na tuzo zaidi ya 30 za kikapu. Kwa sasa ni mfanyabiashara.
16. Vinnie Johnson (Dola 500 milioni)
Huyu ni mchezaji wa zamani wa kikapu NBA na mfanyabiashara. Licha ya kucheza kikapu miaka ilee ya 1970 hadi 1992, kipato alichovuna na kuwekeza katika biashara mbalimbali kimeendelea kumlipa akiwa mstaafu.
17. David Beckham (Dola 450 milioni)
Nyota wa zamani wa soka kutoka England aliyezichezea Manchester United, Real Madrid na PSG, Beckham kwa sasa ni mmiliki mwenza wa timu ya soka ya Inter Miami nchini Marekani.
18. Lewis Hamilton (Dola 450 milioni)
Dereva wa Mwingereza wa Formula One aliyeshinda mataji mengi, akiwa ndiye supastaa wa mchezo huo kwa sasa. Utajiri wake unatokana na malipo anayovuna kutokana na mikataba ya Ferrari na ubalozi wa kampuni mbalimbali duniani. Huyu ni bingwa mara saba wa Formula One (2008, 2014, 2015, 2017, 2018, 2019 na 2020).
19. Neymar (Dola 450 milioni)
Mchezaji wa Kibrazili aliyezichezea timu za Santos, Barcelona, PSG na Al Hilal. Ni mfanyabiashara aliyevuna utajiri kutokana na mikataba ya soka na ubalozi.
20. Floyd Mayweather (Dola 400 milioni)
Bondia mwenye mafanikio makubwa zaidi kibiashara katika historia ya ngumi duniani. Kawekeza katika masoko ya fedha Marekani na pia ni mwanahisa wa kampuni kibao hukohuko kwao.
Wanamichezo wengine matajiri ni Greg Norman (Dola 400 milioni) ambaye ni mcheza gofu kutoka Australia na mfanyabishara, Jack Nicklaus (Dola 400 milioni), mcheza gofu mstaafu wa Marekani na mmoja wa mastaa wanaolipwa zaidi katika historia ya michezo na Alex Rodriguez (Dola 350 milioni) mchezaji wa zamani wa mpira wa magongo na mchambuzi wa televisheni wa mchezo huo aliyekipiga Seattle Mariners na Texas Rangers.
Wengine ni Fran Tarkenton (Dola 350 milioni) ambaye ni mcheza soka la Kimarekani wa zamani, mtangazaji wa televisheni na mfanyabiashara wa programu za kompyuta. Yupo pia Dale Earnhardt Jr (Dola 300 milioni) ambaye ni dereva wa zamani wa mbio za NASCAR, mmiliki wa timu ya mchezo huo ya JR Motorsports, mwandishi na mchambuzi wa televisheni ya NBC.
Matajiri wengine ni George Foreman (Dola 300 milioni) ambaye ni bondia maarufu wa zamani akimiliki chapa ya 'George Foreman Grill', Hakeem Olajuwon (Dola 300 milioni), nyota wa zamani wa kikapu NBA aliyeiongoza Houston Rockets kutwaa ubingwa mfululizo miaka ya 1990 na Kevin Durant (Dola 300 milioni) staa wa NBA anayelipwa mkwanja mrefu akivuna zaidi ya Dola 42 milioni kwa msimu.
Vilevile kuna Mario Lemieux (Dola 300 milioni) ambaye ni mchezaji wa zamani wa magongo anayetambulika kama mmoja wa mastaa bora kabisa katika historia ya mchezo huo, Paul Caddick (Dola 300 milioni) staa wa zamani wa raga, Phil Mickelson (Dola 300 milioni) mcheza gofu maarufu wa Marekani.
Wengine wenye Dola 300 milioni ni Roger Goodell, Roger Staubach na Tom Brady (American football), Russell Westbrook (kikapu NBA), Saul 'Canelo' Alvarez (bondia), Serena Williams (tenisi) na Fernando Alonso (dereva Formula One).
Wenye Dola 25 milioni ni Grant Hill (staa wa zamani wa NBA, Kimi Raikkonen (Formula One), Kylian Mbappe (mwanasoka Real Madrid, Peyton Manning (soka la Marekani), Rory McIlroy (mcheza gofu), Stephanie McMahon na Triple H (mieleka WWE) pamoja na Wayne Gretzky (magongo).
Pia kuna wenye Dola 240 milioni wakiwamo Novak Djokovic (tenisi) na Steph Curry (kikapu NBA), huku Manny Pacquiao ambaye ni bondia bingwa wa dunia wa ngumi za madaraja manne ya uzito tofauti (flyweight, featherweight, lightweight, na welterweight) akiwa na Dola 220 milioni sawa na Rafael Nadal, mcheza tenisi maarufu wa zamani na mmoja wa magwiji wa muda wote hasa kwenye mashindano yanayotumia viwanja vya udongo (clay).