Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kwenye Dabi Kariakoo miguu ya miamba hii imeshangiliwa kotekote!

KOTEKOTE Pict


SIMBA na Yanga usiku wa leo zitakuwa kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar katika pambano la kwanza la Ligi Kuu Bara msimu huu maarufu kama Dabi ya Kariakoo.


Hilo ni pambano pia la kwanza la Ligi Kuu Bara kwa watani wa jadi kukutana Zanzibar, japo ni la saba kwa michuano tofauti kwa klabu hizo kukutana visiwani humo tangu mwaka 1975.


Mara ya kwanza katika kukutana Zanzibar ilikuwa ni katika mechi ya fainali ya Klabu Bingwa Afrika Mashiriki na Kati (Sasa Kagame Cup) mwaka 1975 na Yanga kushinda kwa mabao 2-0 kisha kukutana mara mbili mfululizo 1992 katika michuano hiyo ya Cecafa na Simba kushinda kwa penalti baada ya dakika 120 kumalizika kwa sare ya 1-1, kisha Ligi Kuu ya Muungano Simba ikishinda 1-0.

KOTE 01

Baada a kupita muda mrefu timu hizo zilikutana tena mara tatu katika mechi za michuano ya Kombe la Mapinduzi, 2011 Simba ikashinda 2-0 na nusu fainali ya 2017 ikashinda pia kwa penalti na 2021 ilikuwa zamu ya Yanga kushinda kwa penalti na kubeba taji lao la pili la michuano hiyo.

Wenyeji wa pambano la leo linalosubiriwa kwa hamu n wapenzi na mashabiki wa soka ni Yanga walioamua kulipa jina la ‘Damaro Day’, ikilenga kumpaisha kiungo nyota aliyetua Jangwani katika dirisha dogo kutoka Singida Black Stars, Mohammed Damaro Camara aliyebadilisha uraia.

Kiungo huyo alikuwa raia wa Guinea kabla ya mwaka jana kudaiwa kubadilisha ili awe Mtanzania sambamba na nyota wengine wawili, Emmanuel Keyekeh na Josephat Bada aliyepo Algeria kwa sasa, ambao hata hivyo hivi karibuni ziliibuka taarifa mtaa wa pili wana wasiwasi na uraia wake.

KOTE 02

Hiyo ni mechi ya 115 kwa timu hizo katika Ligi ya Bara tangu mwaka 1965, huku likiwa ni la 10 kwa kila mmoja kwa msimu huu zikitenganishwa kwa tofauti na pointi tano tu, Yanga ikiwa na 28 ikiongoza msimamo wa ligi hiyo, huku Simba ikiwa ya tatu kwa kukusanya alama 23 hadi sasa.

Yanga imerejea kileleni ikiiengua JKT Tanzania baada ya kuwafumua maafande hao kwa mabao 5-0 juzi jioni kabla ya Simba kubanwa mbavu na Dodoma Jiji kwa kutoka suluhu jijini Dodoma, hivyo timu hizo zinakutana zikiwa na matokeo tofauti katika mbio za kuwania ubingwa wa msimu huu.

Mara ya mwisho kwa timu hizo zilipokutana katika mechi ya Ligi Kuu iliyoamua ubingwa wa msimu uliopita iliyopigwa Juni 25, mwaka jana kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam, Simba ililala kwa mabao 2-0 yaliyofungwa na Pacome Zouzoua na Clement Mzize.

KOTE 03


WAMEKIPIGA KOTEKOTE

Katika pambano la leo litakalokuwa la kwanza kwa baadhi ya mastaa wa timu hiyo sambamba na makocha Pedro Goncalves na Steve Barker, kuna wachezaji wanne ambao wamewahi kuzicheza mechi za dabi zilizopita wakiwa na uzi wa timu zote kwa vipindi tofauti.

Clatous Chama na Nickson Kibabage wa Simba walishawahi kucheza mechi hizo za watani wakiwa na uzi wa Yanga, lakini kwa upande wa Yanga mabeki wa pembeni, Israel Mwenda na Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ walishawahi kukiwasha katika Dabi wakiwa na uzi wa Msimbazi.

Hata hivyo, ni Tshabalala pekee kwa sasa ndiye nyota aliyehama mtaa moja kwenda mwingine atak ayekiwasha kwa leo, wengine walipita klabu nyingine kwanza kabla ya kutua mahali walipo, lakini ni kwamba wamekiwasha kotekote.

KOTE 04

Kibabange kabla ya kutua Simba kwa msimu huu alipita Singida Black Stars kama ilivyo kwa Chama ambaye alitokea huko baada ya msimu uliopita kukiwasha Yanga akitokea Msimbazi na sasa amerejea, huku akiwa mmoja ya wachezaji waandamizi wa mechi hizo za Dabi ya Kariakoo.

Mwenda naye aliwahi kukipiga Simba kisha akaenda Singiga Black Stars kabla ya kutua Yanga akiitumikia kwa msimu wa pili sasa, akimpokea Tshabalala aliyekuwa naye Simba kwa muda mrefu, huku akiwa ndiye mchezaji aliyedumu kwa muda mrefu na timu timu tangu 2014-2025.

Kwa maana hiyo nyota hao wanne watakutana uwanjani wakiwa wameshawahi kucheza pamoja na timu hizo na hivyo kila mmoja anaujua uzoefu na udhaifu wa mwenzake na pale New Amaan Complex, kwa hakika kutakuwa na kazi kwelikweli kuanzia saa 2:15 usiku.


WANAFUATA NYAYO

Nyota hao sio wa kwanza kucheza dabi wakiwa na uzi wa timu hizo mbili kongwe nchini, hapa chini ni orodha ya baadhi ya wachezaji waliowahi kuvaa uzi wa Yanga au Simba kabla ya kuibukia upande wa pili na mambo yakaendelea kuwa freshi tu hadi walipoondoka katika kabla hizo.

KOTE 05

Orodha hii haikuwagusa waasisi wa kuhama mitaa wa miaka ya 1960-1990, akiwamo Ezekiel Greyson ‘Jujuman’, Mambo Mzinga, Zamoyoni Mogella ‘Golden Boy’, Method Mogella, Ally Yusuf ‘Tigana’, Ismail Suma, Thomas Kipese, Nico Bambaga, Mohammed Hussein ‘Mmachinga’, Edibily Lunyamila, Athuman Abdallah ‘China’, Shaaban Ramadhan, Said Mwamba ‘Kizota’ na Joseph Katuba .

Hapa chini ni orodha ya baadhi ya mastaa waliokipiga kokote kuanzia miaka ya 2000 hadi sasa wakipokewa na kina Mohammed Hussein ‘Tshabalala’.


MAKIPA: Ivo Mapunda, Juma Kaseja, Mohammed Said ‘Nduda’, Yaw Berko, Ally Mustafa ‘Barthez’ na Deogratius Munishi ‘Dida’  na Beno Kakolanya.

Kwa vipindi tofauti makipa hao walizitumikia timu hizo na kuzipa mafanikio na kwa sasa baadhi yao wamestaafu kucheza na kugeukia ukocha.


MABEKI: Hassan Ramadhan ‘Kessy’, Gadiel Michael, George Owino na Kelvin Yondani.

Hawa ni baadhi ya mabeki waliofanikiwa kuvaa uzi wa Wekundu wa Msimbazi na ule wa Jangwani na kufanya mambo makubwa, japo wengine wanaendelea kukikunikisha katika Ligi Kuu.


VIUNGO: Athuman Idd ‘Chuji’, Edwin Mukenya, Haruna Moshi ‘Boban’, Amri Kiemba, Mohammed Banka na Jonas Mkude. Mafundi hao wa boli ni kati ya wachezaji waliovaa uzi wa pande zote mbili na kukinukisha sana uwanjani baadhi ao kwa sas wakiwa wamestaafu, lakini wakiacha heshima kubwa Kariakoo Dabi.


WASHAMBULIAJI: Emmanuel Okwi, Mrisho Ngassa, Nsa Job, Amissi Tambwe, Moses Odhiambo, Bernard Morrison ‘BM3’, Augustine Okrah, Amissi Kiiza ‘Diego’, Saido Ntibazonkiza, Jean Baleke na Ibrahim Ajibu. Wakali hao wa kutupi wanaendelea kukumbukwa kwa kazi nzuri wakiwa na jezi za timu hizo mbili kwa vipindi tofauti na kufanya mambo makubwa ambayo yamewafanya waache alama katika klabu hizo kongwe ambazo leo zinaenda kumaliza ubishi wa nani atakayeibuka mbabe huko Zenji.