Prime
Rekodi za makipa Simba, Yanga Dabi ya Kariakoo
MACHO na masikio ya wadau wa soka kwa sasa, yameelekezwa siku ya Jumapili ya Machi 1, 2026, kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, visiwani Zanzibar, wakati itakapopigwa mechi ya 'Kariakoo Derby', kati ya watani wa jadi Yanga dhidi ya Simba.
Mechi hiyo itakuwa ni ya 115, kwa timu hizo kukutana katika Ligi Kuu Bara tangu mwaka 1965, ambapo Simba inakibarua cha kuvunja uteja wa kuchapwa mara nne mfululizo, huku kwa upande wa Yanga ikitaka kuendeleza rekodi bora kwa wapinzani wao.
Tangu mara ya mwisho Simba ilipoifunga Yanga mabao 2-0, yaliyofungwa na waliokuwa nyota wa kikosi hicho, Henock Inonga na Kibu Denis, katika mechi ya 110, iliyopigwa, Aprili 16, 2023, haijawahi kushinda tena zaidi ya kuambulia vichapo tu.
Mechi iliyofuata ya Ligi Kuu Bara iliyopigwa, Novemba 5, 2023, Yanga iliitembezea Simba kichapo cha fedheha cha mabao 5-1, ikashinda 2-1, Aprili 20, 2024, kisha 1-0, Oktoba 19, 2024, huku pambano la mwisho ikachapwa, 2-0, Juni 25, 2025.
Ushindi huo kwa Yanga wa Juni 25, 2025, uliifanya kutangazwa mabingwa wa Ligi Kuu msimu wa 2024-2025, baada ya kucheza mechi zake 30, ikishinda 27, sare moja na kupoteza miwili, ikiwa na pointi 82, ukiwa ni ubingwa wa 31, tangu mwaka 1965.
Kwa upande wa Simba, ilimaliza msimu huo ikishika nafasi ya pili na pointi 78, baada ya kushinda mechi 25, ikitoka sare tatu na kupoteza miwili, ikitema taji la Ligi Kuu kwa msimu wa nne mfululizo, kufuatia kunyakuliwa na watani zao Yanga.
Hata hivyo, wakati mechi hiyo ya Machi 1, 2026, ikisubiriwa kwa hamu na mashabiki na wadau mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi, wapo makipa wenye rekodi za aina yake kati ya timu hizo mbili, kama ambavyo Mwanaspoti linawaelezea vizuri.
WALIOFUNGWA MABAO MENGI
Katika mechi za aina hii za 'Kariakoo Derby', wapo makipa ambao wamekuwa ni waathirika wakubwa wa kufungwa mabao mengi, kwenye pambano kati ya miamba hiyo lililozalisha vichapo vikubwa, japo kwa bahati mbaya zaidi wengi wao ni wale wazawa.
Kipa wa kwanza kufungwa mabao mengi katika mechi baina ya miamba hiyo ni, Mbaraka Salum, wa Simba, wakati kikosi hicho kilichofahamika kwa jina la Sunderland, kilipochapwa mabao 5-0, Juni 1, 1968, ikiwa ni kichapo kikubwa tangu mwaka 1965.
Katika mechi hiyo, mabao ya Yanga yalifungwa na Maulid Dilunga aliyefunga mawili dakika ya 18 kwa penalti na lingine pia dakika ya 45, kisha, Salehe Zimbwe akafunga mawili dakika ya 54 na 89, huku, Kitwana Manara, akifunga moja dakika ya 86.
Ushindi huo kwa Yanga ni wa kwanza mkubwa zaidi kwa timu hiyo tangu zilipoanza kukutana katika Ligi Kuu Bara mwaka 1965, ukiwa ni mwendelezo mzuri, baada ya kushinda bao 1-0, la Kitwana Manara, dakika ya 28, mechi iliyopigwa, Machi 30, 1968.
Kipa mwingine aliyefungwa mabao mengi ni Bernard Madale wa Yanga aliyefungwa sita, wakati kikosi hicho kikichapwa 6-0, Julai 19, 1977, huku aliyekuwa kocha na mchezaji wa Simba, Abdallah 'King' Kibadeni, akifunga matatu yaani 'Hat-Trick'.
Mechi hiyo ya 11, kukutana katika Ligi Kuu, Kibadeni alifunga mabao hayo kunako dakika ya 10, 42 na 89, wakati, Jumanne Hassan 'Masimenti', alifunga mawili dakika ya 60 na 73, huku lingine moja ni la kujifunga la Selemani Sanga, dakika ya 20.
Hat-Trick hiyo ya Kibadeni ya Julai 19, 1977, ni rekodi kwa mchezaji kufunga mabao matatu katika mechi ya watani wa jadi ambayo hadi leo unapoisoma makala hii, hakuna mwingine aliyefunga, licha ya timu hizo kusheheni nyota mbalimbali wakali.
Kipa mwingine aliyefungwa mabao mengi ni Said Mohammed 'Nduda' wa Yanga aliyefungwa manne katika kipigo cha 5-0, Mei 6, 2012, baada ya Mghana Yew Berko kupigwa bao moja na kuumia, hivyo, kumwachia nyota mwenzake msala huo wa kichapo kizito.
Mabao ya Simba yalifungwa na Mganda Emmanuel Okwi aliyefunga mawili dakika ya 1 na 65, kisha mengine matatu yalifungwa kwa penalti, akianza, Patrick Mafisango dakika 58, Juma Kaseja, dakika ya 69, huku mwingine ni Felix Sunzu dakika ya 74.
Mbali na Berko kuichezea Yanga, ila kipa huyo aliwahi kuicheza pia Simba mwaka 2013, akichukua nafasi ya Mganda Abel Dhaira, ambapo ilielezwa baada ya kuondoka nchini alirejea kwao Ghana kwa wakati huo akiwa kocha wa makipa na mchungaji.
Berko aliichezea Yanga kwa misimu miwili tangu alipojiunga nayo mwaka 2009, akitokea Liberty Professionals iliyomkuza, ingawa aliondoka mwaka 2012 na kurudi kwao Ghana, japo mnamo mwaka 2013, alijiunga na Simba aliyoichezea kwa miezi sita.
Enzi za uchezaji wake akiwa na timu za Yanga na Simba, Berko alikuwa mfano kwa wachezaji waliokuwa na msimamo na imani, kutokana na matukio yake, hali iliyosababisha kubatizwa jina la Baba mchungaji kabla ya kukabidhiwa majukumu hayo rasmi.
Kipa wa mwisho aliyepokea kichapo kizito, ni Aishi Manula akiwa Simba, wakati kikosi hicho chenye maskani yake mitaa ya Msimbazi Kariakoo, jijini, Dar es Salaam, kilipochapwa mabao 5-1, katika mechi iliyopigwa, Jumapili ya Novemba 5, 2023.
Manula ambaye msimu huu amerejea tena Azam aliyowahi kuichezea kabla ya kujiunga na Simba mwaka 2017, aliruhusu mabao hayo matano, akiwa ni kipa wa mwisho mzawa kuruhusu kichapo hicho kizito, katika mechi ilizowakutanisha miamba hiyo.
Katika mechi ya Novemba 5, 2023, ambayo ni ya 111, kwa timu hizo kukutana katika Ligi Kuu, mabao ya Yanga yalifungwa na Kennedy Musonda dakika ya tatu tu, kisha aliyekuwa nyota wa Simba, Kibu Denis, akalisawazisha bao hilo dakika ya tisa.
Baada ya Kibu kulisawazisha bao hilo, ndipo Yanga ikajibu mapigo, ambapo, Maxi Nzengeli alifunga mawili dakika ya 64 na 77, huku Stephane Aziz KI akifunga dakika ya 73, kisha Pacome Zouzoua, akahitimisha la tano kwa penalti ya dakika ya 87.
WALIOTUPIA NYAVUNI
Licha ya kuchezwa dabi 114 za Ligi Kuu tangu mwaka 1965, ila ni makipa wawili tu waliowahi kufunga mabao katika mechi hizo, ambao wote kwa pamoja wanatoka ndani ya timu ya Simba, huku kila mmoja wao akifunga kwa mkwaju wa penalti pekee.
Idd Pazi 'Father' ndiye aliyeanza kufunga katika mechi iliyopigwa Machi 10, 1984, alipoitanguliza Simba kwa penalti ya dakika ya 20, kisha, Omar Hussein akaisawazishia pia Yanga dakika ya 72 na pambano hilo kumalizika kwa sare ya bao 1-1.
Juma Kaseja alifunga pia bao la nne dakika ya 69, huku Emmanuel Okwi akifunga mawili dakika ya 1 na 65, wakati Patrick Mafisango dakika ya 58 na Felix Sunzu dakika ya 74, wakifunga kila mmoja kwa penalti, Simba ikishinda 5-0, Mei 6, 2012.
Kaseja aliyewahi kucheza Simba, Yanga na timu ya taifa ya Taifa Stars, kwa sasa ni kocha wa Kagera Sugar, inayoshiriki Ligi ya Championship kwa msimu huu wa 2025-2026, amewahi pia kukichezea kikosi hicho akiwa mchezaji na kocha wa makipa.
Kagera iliyodumu katika Ligi Kuu Bara kwa miaka 20, tangu ilipoanza kushiriki 2005, ilishuka daraja msimu wa 2024-2025, baada ya kushinda mechi tano tu, sare minane na kupoteza 17, ikishika nafasi ya 15, kufuatia kukusanya pointi zake 23.