KWAKO JESSE JOHN: Tuanze na nyasi bandia ndipo VAR ifuate

NIANZE kwa kumpongeza Ally Mayay kwa ushauri wake wa kuwakumbusha watangazaji na waandishi wanaowapachika majina ya utani wachezaji, kutoa majina yenye manufaa yanayoakisi uhalisia wa mchezaji na kile anachokifanya uwanjani na sio bora jina tu.

Kumwita mchezaji Nungunungu au kichuguu, haileti maana katika muktadha wa mchezo wa soka, japo huenda mtoaji wa jina alikuwa na maana yake kwa jinsi mnyama huyo alivyo kimaumbile na yale ayafanyayo anapokabiliwa na hatari.

Nadhani kuna umuhimu wa kuwapa majina yatakayodumu muda mrefu na yenye MAANA na uhalisia fulani.

Zamani Sunday Manara aliitwa’Computer’ kabla ya kitendea kazi hicho kuingia na kufahamika nchini. Hao kina ‘Golden Boy’ Zamoyoni Mogella, ‘Valmet’ Abuu Yasin Napili. Valmet ni aina ya trekta lililokuwa likitifua sana udongo na nguvu kubwa kuhimili kishindo cha heka na maheka.

Nilimpa Waziri Mahadhi jina la utani la MENDIETA na hadi kesho wazazi wake wanamwita hivyo kiasi kwamba jina lake halisi la WAZIRI MAHADHI likawa halisikiki, hadi watoto wadogo wakimfahamu kwa jina hilo na hasa mama yake mzazi alilizoea na kupenda kumwita hivyo. Tumuite JONAS MKUDE Edger Davids, Gattuso au Claude Makelele basi na sio jina la Nungunungu.

Tuachane na ishu za a.k.a, turejee kwa mjadala ulioibuka baada ya Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba kutoa pendekezo la kuletwa kwa Teknolojia ya kusaidia waamuzi uwanjani (VAR).

Pendekezo hilo limeibua mjadala na watu kutoa maoni mbalimbali kuhusu ingizo hilo la VAR ili kuondoa utata katika matokeo mbalimbali ya Ligi Kuu Bara na hasa ikihusisha mechi za SIMBA NA YANGA TU. Mabao yanayofungwa katika mechi zao timu hizi yanaonekana kuwa ‘ya mbeleko, mchongo na wengine kutania eti ya chupli chupli kama yanavyojulikana.

Hoja hiyo imetamalaki hadi katika mhimili wa kutunga sheria yaani BUNGENI, likizungumzwa si katika njia ya utani kama tunavyowafahamu waheshimiwa na mapenzi yao kwa timu hizi.

Bali ni ujumbe kwa mamlaka husika ili kuufanya mchezo wa mpira wa miguu uwe na HAKI kwa pande zote.

Ni jambo jema sana lakini bado soka letu limegubikwa na changamoto nyingi sana ambazo kwazo lazima zitatuliwe kabla ya kuingia katika V.A.R na mojawapo ni hilo la usimba na uyanga linaleta matatizo makubwa ambayo hayataweza kutufikisha pema iwapo pia shutuma za kwamba kuna viongozi wakubwa wanapendelea timu fulani na kuleta mdororo kwa timu nyingine.

Suala la viwanja mfano upeleke VAR Manungu ama Uwanja wa Sokoine Mbeya ambapo mvua ikinyesha hakuna tofauti na ‘Majaruba la Mpunga’?

Ni kama vile wadau wamesahau kuwa mheshimiwa Rais wa Jamhuri wa Tanzania, Samia Saluhu Hassan, aliwahi kusema mapema kwamba atapunguza au kuweka msamaha wa kodi katika nyasi bandia ili kuwezesha wamiliki wa viwanja hivyo na mamlaka husika kuhakikisha vinakuwa bora ili kuleta maendeleo ya mpira wa miguu. Sasa mbona hilo hatulijadili na kulifanyia kazi, badala take tunabaki ‘Simba..Yanga, Simba ..Yanga’, kila uchao...Simba Yanga ...Simba Yanga!!

Mbaya zaidi klabu nyingi hazina viwanja na sasa mdhamini mwenza wa Ligi Kuu Bara, GSM amejitoa. Pengine upo umuhimu wa kuweka sawa taratibu na sheria na vigezo katika kuwafanya wadhamini wabaki katika udhamini na kuvutia wengine.

Hili la kujitoa kwa GSM ni doa kubwa sana katika mustakabali wa soka letu, usimba na uyanga unatumaliza, hauna tija! Halafu tukumbuke kuwa, Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mohamed Mchengerwa, amesema TAIFA STARS tutacheza Kombe la Dunia kwa Mwaka wa 2026 baada ya hizi zitakazofanyika mwaka huu nchini QATAR. Hili ni jambo zito sana na sio jepesi.

Tusubiri tuone!