KWAKO JESSE JOHN: Mtukutu, Jeuri ila utampenda japo kimoyo moyo

DUNIA imepata kushuhudia wanandinga watukutu, wakorofi na watata kwelikweli. Ila pamoja na yote hayo Wazaramo wanao msemo usemao ‘mkono kuunyera mwana kuhudaa kuukana.’ Ikiwa na maana mkono aliounyea mtoto huwezi kuukata.

Mwanao ni mwanao huwezi kujua mbeleni atakuwa na msaada gani. Hapo wapo wazazi wanaochukia na kuwatoa akilini watoto kama hao na hata baadhi ya timu huwaacha katika usajili.

Roster Ndunguru, nyota wa zamani wa Nyota Nyekundu enzi hizo ikiwa na maskani yake Mtaa wa Congo, Dar es Salaam alikuwa mtukutu ndani na nje ya uwanja.

Timu pinzani zilimjua kwa fujo zake na waamuzi walimfahamu, lakini hakuwahi kuachwa katika kikosi cha kwanza cha timu yake labda awe hoi kwa kuumwa na pia ataitamani hiyo mechi. Michael Ballack wa Ujerumani amekuwa mtata kwa timu na kocha Joachim Law, lakini pindi kocha anapotaja majina ya kikosi alimteua Ballack.

Kiungo huyu wa zamani wa klabu ya Chelsea aliyependa kuvalia jezi namba 13 alisifika kwa kufanya utukutu uwanjani hata kuwapiga wachezaji wengine ama kulipiza visasi lakini bado alikuwa kipenzi cha watu.

Paul Gascoigne ‘Gazza’ na Terry Venables walikuwa na ugomvi kwa muda mrefu kutokana na utukutu wa Gazza hasa kushinda kwenye vilabu vya usiku.

Kuna wakati kocha Venables alikunjwa na Gazza katika ‘touch line’ akiwa mchezoni na kilikuwa ni kitendo cha ghafla baada ya kumfokea kwa kutotimiza vyema majukumu yake uwanjani, lakini baadae Venables aliishia kusema: “With all of this I still love him.” akimaanisha pamoja na yote hayo bado anampenda kijana wake huyo kutokana na mavitu yake uwanjani akiiwezesha ‘Three Lions’ timu ya taifa ya England kung’ara.

Wapo kina Gennaro Gatusso mtukutu wa kutupwa, ila kwa mavitu uwanjani balaa.

Jamaa alikuwa akifahamika zaidi kama kifaru kutokana na hasira yake asiyoweza kujidhibiti hasa anapogadhabika na matukio ya kumkunja ‘roba’. Kocha wake alikuwa ni sehemu ya kawaida. Alishawahi kunukuliwa kocha Carlo Ancelotti akisema, “ukiwa na Gatusso una mpambanaji wa namna zote… anakupatia asilimia 100 uwanjani, lakini unapaswa kuwa na tahadhari ukiwa kwenye benchi unatoa maelekezo.

Kisha akaongeza kuwa, “anaweza kukubadilikia sekunde yoyote kama hakuelewi.”

Pamoja na hayo hakuna kocha aliyewahi kumuweka benchi kwa sababu aliujua mpira. Sasa ni mmoja wa makocha wa timu kubwa huko Italia.

Wapo na wengine kadhaa kama Mario Baloteli, Joey Barton, Zlatan Ibrahimovic, Roy Keane ‘ngumi mkononi’, Patrick Viera na kadhalika. Hawa ni watukutu hasa, lakini bado huwa utukutu wao unafichwa kwa sababu ya uwezo wao mkubwa uwanjani na wamekuwa vipenzi vya makocha na waandishi wa habari kutokana na ujeuri wao, ujivuni na vipaji vikubwa vya nyota hao wanapokuwa ndani ya uwanja wakitumwa ‘kazi maalumu’.

Bernard Morrison ni aina ya hao na mara nyingi akifanyiwa mabadiliko kabla ya malengo yake hajayafikia anakasirika mara kadhaa, lakini anatajwa kuwa miongoni mwa wachezaji wacheshi kwenye ‘changing room’ kwa wenzake na hata kambini wanapenda kuwa naye hata kama anaumwa.

Mashabiki uwanjani hupenda awepo kuwafurahisha kwa sababu ana kipaji kikubwa na waandishi hupenda mahojiano naye kutokana na utundu na ucheshi katika maongezi yake.

Katika dakika ya 83 anachomoa dhidi ya Gerndamarie ugenini akitokea benchi kwenye dakika za maji ya jioni tena ikiwa ni ‘touch’ yake ya pili tu uwanjani kisha anazunguka goli, anageuka kuwaita wenzake anawaongoza kwenda Magharibi mwa uwanja karibu na benchi kwa sekunde kadhaa.

Hapo anawachezesha wanarudi kujipanga tena kuilinda alama yao moja mkononi na watu wanasahau kama ametoka kufunguliwa kwenye kusimamishwa kwa muda usiojulikana na anaibeba Simba kwa alama moja. Hiyo ndiyo sura halisi ya Bernard Morisson na watukutu wengi duniani.

Inatajwa kuwa wana vipaji vikubwa ila suala la kuvitunza ni wachache hufanikiwa kwa sababu huwa wanavumiliwa lakini hawatabiriki sana.

Wanakuokoa kwenye nyakati ngumu lakini wanaweza kukukera sekunde yoyote uwanjani. Ni kama uyoga tu… leo mboga kesho ni sumu.