Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

KWAHERI MODEST: Mwandishi asimulia alivyomfuata Modest Kigoma

Muktasari:

  • Kwa mara ya kwanza kuonana ana kwa ana ilikuwa Septemba mwishoni mwaka 2024, nilipomtembelea mkoani Kigoma, ambako alikuwa anauguzwa na familia yake kwa maana ya baba yake Modest Songoro (mgane) na wadogo zake baadhi ambao ni Augustino na Teddy.

IMENIWIA ugumu kusimulia angalau kwa uchache nilivyomfahamu beki wa kushoto wa zamani wa Simba, Yanga na Taifa Stars, Alphonce Modest ambaye amefariki dunia.

Kwa mara ya kwanza kuonana ana kwa ana ilikuwa Septemba mwishoni mwaka 2024, nilipomtembelea mkoani Kigoma, ambako alikuwa anauguzwa na familia yake kwa maana ya baba yake Modest Songoro (mgane) na wadogo zake baadhi ambao ni Augustino na Teddy.

Safari ya kutoka jijini Dar es Salaam hadi Kigoma kwa basi ni sawa na kilomita 1088, kiukweli haikuwa rahisi kwani gari liliharibika kabla ya kufika Mlandizi ilichukua muda kukaa sawa, nikafika siku ya pili yake alfajiri ya saa 11, ambapo nikatafuta hoteli ili kupumzika angalau kwa saa mbili na kupata muda wa kuoga.

Baada ya kufika saa 2:00 asubuhi nilimpigia mdogo wake Augustino ili anielekeze ni sehemu gani walipo, akaniambia nitafute mgahawa kwanza ili nipate chai kisha atanifuata hapo, nikafanya hivyo.

Wakati naendelea kupata kifungua kinywa nikampigia simu kocha Zuberi Katwila ili anielezee Alphonce ni mtu wa aina gani, maana sikuwahi kumuona kabla zaidi ya kumsoma katika mitandao ya kijamii namna alivyokuwa anacheza vizuri.

Stori za hapa na pale za Katwila zilinipa picha ya kumfahamu kwa uchache Alphonce kuwa alikuwa ni mtu wa misimamo mikali na akili kubwa.

Sikuishia hapo nikamtafuta mchezaji nwingine wa zamani wa Simba, Yanga na Stars Zamoyoni Mogella aliyeniambia:” Japokuwa sikucheza naye walikuja nyuma yangu, lakini namfahamu ni mchezaji aliyevuja jasho lake na sasa anaumwa, ila nakuombea kwa Mungu umpate, maana hataki kabisa mahojiano ila sali Mungu atakuongoza na utafanikiwa ili Watanzania waone na waweze kumsaidia kwa ukubwa, ukifika nitaongea naye.”

Baadaye akaja mdogo wake Augustino, tukasalimiana lakini aliniambia:”Nisamehe sana wakati tunawasiliana ukiwa Dar es Salaam sikukwambia ukweli kwamba kaka hataki mahojiano, lakini baba na ndugu zetu tunahitaji msaada wa Watanzania, hatuna uwezo wa kumsaidia maana yeye ndiye tulikuwa tunamtegemea.

Aliendelea kusimulia: “Kuna wanahabari kutoka nje ya nchi walikuja, aliwafukuza na hakuongea nao kabisa.”

Baada ya maneno ya Augustino moyo wangu ukawa umeingia ubaridi ingawa usoni niliendelea kujikaza na kumuonyesha kila kitu kitawezekana.

Safari hiyo niliungana na mwanahabari mwenzangu anayeitwa Happy Tesha mwakilishi wa Kigoma ambaye alitukuta mgawahani.

Safari ikaanza kutoka mgawahani hadi katika mtaa wa Kisangani Mwanga Kaskazini ambako ndiko iliko nyumba yao.

Augustino akatembea kwa hatua za haraka hadi katika geti la mabati na akaniambia, “karibu usishangae hapa ni nyumbani kwetu, kama ulitegemea mjengo wa maana uhalisia ndio huu.”

Kisha tukaingia ndani ambapo nilikutana na baba yake mzazi Modest Songoro, wajomba zake na mdogo wao wa kike, Teddy.

Mzee Songoro akanipeleka moja kwa moja hadi chumba alichokuwa amelala Alphonce,  kiukweli nilivyomuona kitandani hali ikawa tofauti na picha nilizokuwa naziona mtandaoni.

Baba yake akamwambia Alphonce kuna ugeni wa mwanahabari kutoka kampuni ya Mwananchi, gwiji huyo akasema “karibu”.

Tukasalimiana kisha akaniuliza: “Umefuata nini?”

Nikamjibu kwa ujasiri: “Nimekuja kukusalimia.”

Akasema: “Kama ni mahojiano, sipo tayari.”

Baba yake akaongea kwa uchungu huku jicho moja likimtoka machozi: “Alphonce naumia kukuona hapo, natamani kama mzazi nitimize kila hitaji lako, lakini nimechoka sina kitu, tafadhali naomba zungumza na mgeni atatusaidia kuwafikia Watanzania wengi.”

Baadaye nikamuomba mzee atoke nje ili nibakie naye, nikamuuliza: “Wewe ni Mkristo ama Muislam? Akajibu ni Mkristo.

Nikamuuliza tena: “Je, naweza nikakuombea?”

Akajibu: “Ndio.”

Kisha nikaanza maombi. Baada ya kumaliza akasema: “Nimestaajabu kuona mwandishi wa aina yako.”

Hapo zikaanza stori za maisha ya hapa na pale zilizoanza saa 5:00 asubuhi hadi saa 7:00 mchana, huku familia yake ilikuwa inachungulia dirishani ikashangazwa na kicheko na furaha aliyokuwa nayo.

Baadaye akasema: “Moyo wangu mweupe kabisa kufanya mahojiano na wewe, nimefurahia ujio wako ingawa kabla ya kuanza stori nilijikuta nachukia.”

Mahojiano hayo yalichukua saa mbili, hivyo nilikaa naye takribani kwa saa tano.

Kabla ya mahojiano, neno lake la kwanza lilikuwa: “Wanawake ninyi ni wakatili sana.”

Nikamuuliza: “Kuna shida gani?”

Japokuwa hakufunguka kiundani, nyuma yake nikagundua kuna stori ya maumivu ya mapenzi.

Alisimulia alivyoanza kuumwa kulikoanzia ndotoni akiwa Mtibwa Sugar, kuamka asubuhi akawa anajisikia vibaya.

Nilimshuhudia Alphonce umbo lake lilikuwa limekaa zig-zaga mikono na miguu, hakuweza kutingisha kichwa kilichokuwa kinaangalia juu, kuna muda nzi walimzinga usoni aliishia kutoa machozi, maana mikono yake ilikuwa haifanyi chochote, ingawa akili yake ilikuwa kubwa katika kufikiri mambo na bado hakupoteza uongozi wa familia kama kijana wa kwanza.

Swali moja gumu ambalo ilinichukua muda kumuuliza ni kutokumuona mke wake pembeni yake wakati wa shida anayoipitia hasa kwa kuwa mwanzo wa stori alianza kusema “wanawake ninyi ni wakatili”.

Baada ya swali hilo alichukua kama dakika tatu akichakata jambo kichwani. Ilikuwa kama mtu aliyetoneshwa kidonda, huku moyoni mwangu nikiwa najisikia majuto ya kwa nini nimemuuliza.

Lakini alielezea kwa kifupi: “Nilikuwa sitaki mahojiano kwa sababu mke niliyekuwa naye aliuza kila kitu ikiwamo nyumba mbili za Dar es Salaam akanitoroka bila kuniacha na kitu, sasa mtu akija hapa akaona mazingira haya tafsiri yake ataona nilikuwa nakula bata nikajisahau kuwekeza. Sitasema mengi. Na mbaya zaidi nilimuacha kwa dharau mwanamke niliyeanza naye chini wa hapa Kigoma ambaye ndiye ananijali kwa sasa, hadi naona aibu.”

Katika mazungumzo alimtaja kiungo wa zamani wa Simba, Yanga na Taifa Stars, Jonas Mkude kuwa ni miongoni mwa wachezaji ambao walimpa msaada mkubwa kipindi kigumu.

Nikampigia Mkude (video call) wakapata muda wa kuzungumza na Alphonce wakabadilishana mawazo ya hapa na pale, baada ya kumaliza mazungumzo nikampigia Mogella ambaye pia walizungumza kwa furaha na akasisitiza anipe ushirikiano.

Baada ya kumaliza kila kitu na kurudi Dar es Salaam, nikawa nawasiliana naye pamoja na ndugu zake ambao baada ya umauti kumfika walinitaarifu Oktoba 21.

Lakini wiki moja nyuma kabla ya kifo chake nilipokea simu ya msemaji wa Mtibwa Sugar, Thobias Kifaru akaniambia hali ya Alphonce ni mbaya niandike ili Watanzania wamchangie kwa sababu hastahili kuishi mazingira magumu kwa namna alivyomkuta baada ya kwenda kumuona.

Bila kusita nikampigia siku na kumsalimia kupitia mdogo wake Augustino, maneno yake yaliniumiza sana.

Akizungumza kwa sauti ya chini iliyochoka zaidi ya vile nilivyozoea kumsikia, alisema: “Mdogo wangu acha, nimechoka nasubiri muujiza wangu Mungu anichukue, sioni tena nafasi nyingine (ya kuishi), acha tu nipumzike na ukiwa na nafasi ya kusaidia wengine fanya hivyo kwa bidii, kwa heri majukumu mema.”

Yalikuwa ni mazungumzo mafupi na mazito sana kwangu.


RATIBA YA MAZISHI

Kwa mujibu wa Augustino, mdogo wa wa Modest, marehemu atazikwa Ijumaa mchana katika makaburi ya Lubengela, ataagwa asubuhi nyumbani kwao mtaa wa Kisangani Mwanga Kasikazini, Kigoma Mjini, kisha watakwenda kanisa la Roman Catholic la Bikira Maria Mshindani kumfanyia misa takatifu, kisha kumpumzisha katika nyumba yake ya milele.

“Kwa sasa tunaendelea kupokea wageni mbalimbali wanaokuja kutuona na tunawasubiri watoto wake ambao ni Kelvin yupo Morogoro, Rachel yupo Mwanza na Vicky yupo Arusha.”


WOSIA WAKE

Augustino amesema kabla ya kaka yake kufariki dunia alimwambia kwamba ahakikishe wanawe wanawajua ndugu.

“Hakikisha wanangu wanawajua ndugu zao na waje kunizika. Pia naomba umwambie Nteze John (nyota wa zamani wa Simba) kwamba sipo tena duniani, pia alinishukuru kwa kumuuguza kwa kipindi chote na kuacha kila kitu. Baada ya muda hali yake ikabadilika na akaaga dunia,” amesema Augustino.

Mwanaspoti limepata nafasi ya kuzungumza na baba mzazi wa mchezaji huyo, mzee Modest Songoro aliyesema: “Bado nina maumivu makali mno. Siyo kazi rahisi baba kumzika kijana wake, Alphonce ni kijana wangu wa kwanza.”

“Nimeshuhudia maumivu makali ya kijana wangu toka anaugua hadi anaondoka duniani kwa takriban miaka 15. Moyo wangu umevunjika. Acha kwanza tuzike huenda nitakuwa nimetulia.”


MKUDE AMLILIA

Kiungo wa zamami wa Simba, Yanga na Taifa Stars, Jonas Mkude amesikitishwa na kifo cha mchezaji wa zamani wa timu hizo, Alphonce Modest aliyefariki dunia jioni ya Oktoba 21, 2025.

Mkude ni miongoni mwa wachezaji waliowahi kumpa msaada Modest aliyewahi pia kuichezea Mtibwa Sugar.

Baada ya kupata taarifa za msiba, Mkude amesema: “Nakosa neno la kusema, lakini nimejifunza kumjali mtu akiwa katika shida ili shukrani yake aitoe kwa kinywa chake akiwa hai.

“Alphonce alikuwa lejendari, alistahili heshima, upendo kutokana na jasho lake alilovuja uwanjani. Pia nikushukuru mwandishi ulipofika (kwa Modest) ukapiga simu nikazungumza naye. Kumbukumbu ya maongezi yetu itasalia kwangu.

“Naishiwa maneno Mungu ampumzishe kwa amani, kwani ana sababu ya kila jambo, sisi ni wanadamu tunapita.”

Hayati Modest aliwahi kumtaja Mkude kuwa ni miongoni mwa vipaji vikubwa nchini.


MASTAA WENGINE WAGUSWA

Staa wa zamani wa Simba, Yanga na Taifa Stars, Zamoyoni Mogella amesema: “Inaumiza sana, lakini muache akapumzike kwa amani mchango wake katika taifa utakumbukwa.”

Mchezaji mwingine wa zamani wa Simba, Steven Mapunda ‘Garincha’ amesema: “Kwa wachezaji waliomuona akicheza hadi akaazimwa Simba kwenda Yanga kwa ajili ya michuano ya kimataifa wanajua kazi yake. Mungu ampumzishe kwa amani.”