Kwa Mkapa mtapigwa hivi!

MAKOCHA wa Simba na Yanga, Abdelhak Benchikha na Miguel Gamondi ndio waliobeba matumaini ya mashabiki na wadau wa soka la Tanzania katika mechi za robo fainali za kwanza za Ligi ya Mabingwa Afrika zitakazochezwa leo Ijumaa na kesho Jumamosi kwenye Uwanja wa Benjamini Mkapa.

Benchikha ambaye msimu uliopita alitwaa ubingwa wa Kombe la Shirikisho Afrika na CAF Super Cup akiwa na USM Alger ya Algeria mbele ya Yanga kwa kanuni na Al Ahly, kesho atakuwa na kazi ya kuiongoza Simba tena mbele ya watetezi wa Ligi ya Mabingwa Afrika, Al Ahly kutoka Misri.

Mechi hiyo ni ya kwanza ya robo fainali ya michuano hiyo mikubwa kwa ngazi ya klabu barani Afrika litapigwa kuanzia saa 3:00 usiku kabla ya kwenda kurudiana jijini Cairo, Aprili 5 na mshindi wa jumla kufuzu nusu fainali kucheza kati ya TP Mazembe ya DR Congo au Petro de Luanda ya Angola.

Kocha huyo wa kimataifa wa Algeria amemaliza maandalizi yake kwa kiasi kikubwa huku akijivunia wachezaji wake kuwa na uzoefu wa kukabiliana na mafarao hao kwani mwanzoni mwa msimu huu walikutana nao kwenye michuano ya African Football League na walitolewa kwa kanuni, walitoka sare ya mabao 2-2 Kwa Mkapa na walipoenda Misri wakatoka sare ya bao 1-1.

Hii ni mechi ya hesabu na yapo mambo ambayo yanaifanya Simba kuwa na nafasi ya kufanya vizuri kwenye mchezo ikiwemo rekodi japo sio jambo jepesi kutokana na namna ambavyo Al Ahly hubadilika katika michezo ya mtoano na hapo ndipo presha ya mchezo huo inapopanda na kushuka.

Baada ya mechi ya leo Ijumaa, kesho itakuwa ni zamu ya Yanga itakayoikaribisha Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini mchezo utakaopigwa muda ule ule wa saa 3:00 usiku kwenye uwanja huo huo wa Benjamin Mkapa kabla ya kwenda kurudiana Pretoria, Afrika Kusini siku ya Aprili 5.

Yanga ambayo imetoka kujeruhiwa kwenye mchezo wa ligi kabla ya mapumziko ya michezo ya kimataifa kwa mujibu wa kalenda ya FIFA, inatazamiwa kuibuka kivingine huku ikijiimarisha zaidi kulingana na ubora wa Mamelodi ambao wamekuwa tishio kwenye michuano hiyo.  

Uchambuzi huo unaonyesha namna timu zote nne zitakazovaana wikiendi hii zinavyofunga mabao yao, hivyo mashabiki watakaohudhuria mechi hizo wajiandae kushuhudia burudani na aina ya mabao yanayoweza kufungwa Kwa Mkapa kuanzia leo Ijumaa hadi kesho Jumamosi.


AHLY NI VICHWA,PEMBENI

Al Ahly iliyomaliza hatua ya makundi ikiwa kinara wa Kundi D, imefunga mabao sita na kufungwa moja tu katika mechi sita ilizocheza ikishinda michezo mitatu na nyingine tatu ikiisha kwa sare.

Takwimu zinaonyesha mechi ambayo ilizalisha mabao mengi zaidi kwa vigogo hao ni ile dhidi ya Medeama iliyopigwa Cairo, ilipoishindilia mabao matatu.

Ahly inaonekana hatari zaidi kwenye kupasia nyavu pale kwa kutumia vichwa inapokuwa kwenye boksi la timu pinzani.

Katika mabao sita waliyofunga matatu kati ya hayo yametokana na vichwa. Katika mchezo wa kwanza wa makundi dhidi ya Medeama ambao ilimaliza kwa ushindi wa 3-0, mawili ilifunga kwa kichwa na moja pekee ndio ilikuwa kwa kupiga shuti.

Vichwa hivyo huwa havijalishi kwamba wanapiga kwa kona au laa, katika mechi ya Medeama Al Ahly ilikuwa na kona moja ambayo ndio ilizaa bao la kwanza lililofungwa na  Mahmoud Karhaba, mabao mengine yalitokana na krosi na mipira iliyokuwa inaelea baada ya wao kushambulia.

Lakini ukiondoa ubora wao kwenye vichwa, Ahly wamekuwa hatari pia kwa mipira ya pili (second ball), pale na timu pinzani inakuwa inaokoa shambulizi lao.

Mabao matatu kati ya haya sita iliyofunga, ilikuwa ni mipira iliyoelea baada ya kufanya shambulizi.

Pia watetezi hao wa michuano, ni hatari sana wanapokuwa katika boski la timu pinzani, hakuna bao lolote walilofunga nje ya boksi katika hatua ya makundi.

Vile vile mabao manne waliyofunga kati ya sita, yote yametokea pembeni na kila pande zimezalisha mabao mawili.

Ilifanya hivyo katika mechi mbili za Yanga, nyumbani na ugenini, pia dhidi ya Medeama mchezo wa kule Misri.

Kwa upande wa kufungwa, imeruhusu bao moja tu, ambalo ni lile dhidi ya Yanga, umakini wa mabeki wao umesababisha iwe ngumu sana kuruhusu bao.

Washambuliaji wa timu pinzani huwa wanapata tabu kuingia katika eneo lao, ndio maana hata bao hilo walilofungwa lilikuwa ni shuti la nje ya boksi.


SIMBA KATIKATI, PEMBENI FRESHI

Hadi inamalizika hatua ya makundi Simba ilishika nafasi ya pili, ikifunga mabao tisa na kufungwa mawili. Mabao hayo tisa iliyafunga katika mechi tatu.

Katika mabao hayo, moja lilitokana na penalti, saba ni kupitia mashambulizi kutoka lango lao hadi boksi la timu pinzani, moja ikafungwa kwa njia ya penalti.

Ukiondoa penalti, Simba imefunga mabao saba yote ndani ya boski, huku moja tu lile la kwanza lililofungwa na Willy Onana ndio ilikuwa ni nje ya boksi.

Hii imeonyesha Simba kuwa na hatari sana pale wanapokuwa katika boksi la timu pinzani.

Simba inaonekana kuwa hatari pia katika mashambulizi ya pembeni. Kwenye mechi dhidi ya Jwaneng ilifunga mabao matatu kupitia mipira iliyotokea pembeni.

Mabao hayo ni lile la kwanza  ambapo lilifungwa kutokea upande wa kushoto, la pili ni  kulia na la tatu likafungwa kushoto.

Ubora wa Simba pia ni katika mashambulizi yanayotokeea kati kati, kwani katika mabao tisa iliyofunga mabao matatu yalikuwa ni ya mashambulizi yaliyotokea eneo hilo.

Mabao haya ilifunga dhidi ya Jwaneng (moja), pia mbele ya Wydad yote mawili yalitokea katikati.

Kwa upande wa mipira ya kutengwa, Simba imefunga mabao mawili tu, lile la kona mbele ya Jwaneng ambalo lilifungwa na Fabrice Ngoma na penalti dhidi ya Asec Mimosa lililofungwa na Saidi Ntibazonkiza.

Hata hivyo, Simba imekuwa na udhaifu katika kuzuia mashambulizi yanayotokana na mipira ya kutengwa.

Katika mabao mawili iliyofungwa, moja lilitokana na mpira wa kutengwa na ilifungwa na Wydad katika dakika za mwisho kule Morocco.

Bao lingine ilifungwa kwa shambulizi la kawaida katika sare ya bao 1-1 dhidi ya Asec.


MABAO YA MAMELODI

Kocha Miguel Gamondi na vijana wake wanatakiwa kuwa macho na washambuliaji wa Mamelodi kutokana na matumizi mazuri waliyonayo ya mipira ya kutenga kwani kati ya mabao saba waliyofunga katika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, manne wamefunga kwa staili hiyo.

Katika mchezo wa kwanza wa Mamelodi iliyokuwa kundi A, iliifunga Nouadhibou ya Mauritania kwa mabao 3-0, mawili yalikuwa ya mipira ya kutenga, bao la Peter Shalulile dakika ya 28 lilikuwa la kona iliyochongwa na Marcelo Allende na bao la Gaston Sirino dakika ya 74 ilikuwa faulo.

Mamelodi ilikiona chamoto katika mchezo uliofuata Lubumbashi, DR Congo kwa kutandikwa bao 1-0 dhidi ya TP Mazembe, ilifungwa kwa kichwa na Glody Likonza baada ya krosi nzuri iliyochongwa na Philippe Kinzumbi na hilo ndio bao pekee ambalo mabingwa hao wa African Football League waliruhusu.

Ikiwa nyumbani, Afrika Kusini katika mchezo wa tatu, ilibanwa mbavu na Pyramids ambayo anaichezea mshambuliaji wa zamani wa Yanga, Fiston Mayele, lakini ilipoenda Misri iliibuka na ushindi wa bao 1-0 lililofungwa na Teboho Mokoena kwa shuti kali nje ya eneo la hatari.

Walipoenda Mauritania, Mamelodi iliendelea kutesa kwa mipira ya kutenga kwani katika ushindi wa mabao 2-0 ikiwa ugenini, bao lao la kwanza lilikuwa kwa faulo ambayo ilichongwa na mpiga wao maarufu Allende raia wa Chile na mpira huo ukamaliziwa na Grant Kekana.

Hata katika mchezo wao wa mwisho wa makundi na ulikuwa wa maamuzi juu ya nani atamaliza akiwa kinara wa kundi, Mamelodi ilibebwa na faida ya mipira ya kutenga kwani katika dakika 38, Shalulile aliwazidi ujanja mabeki wa Mazembe kiasi cha kufanyiwa madhambi ambayo refa wa mchezo huo kutoka Morocco, Jalal Jayed  aliamuru mwenyeji ipewe penalti iliyotumbukizwa wavuni na nahodha huyo wa timu ya taifa la Namibia.


YANGA NDANI YA BOX

Katika mabao tisa ambayo Yanga imefunga katika hatua ya makundi, saba yamefungwa ndani ya eneo la hatari ‘boksi’ la wapinzani, wameruhusu mabao mawili tu kati ya sita kwa mipira ya kutenga hiyo ni ishara tosha kuwa kikosi hicho kinaonekana kuimarika.

Yanga ilianza safari yake ya kuitafuta robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa kufungwa ugenini dhidi ya Belouizdad ya Algeria kwa mabao 3-0, bao la kwanza katika mchezo huo lilitokana na mpira wa kutenga.

Waliporejea jijini Dar, ilivuna pointi moja dhidi ya Al Ahly kwa kutoa sare ya bao 1-1, bao la Yanga lilifungwa ndani ya boksi na Pacome Zouzoua akimaliza pasi ya Kennedy Musonda.

Kituo kilichofuata kwa Yanga kilikuwa Ghana ilipokuwa na kibarua kizito dhidi ya Medeama, iliruhusu bao la pili kwa mpira wa kutenga ‘penalti’ katika sare ya bao 1-1 na Pacome aliendelea kufanya yake akifunga tena ndani ya boksi.

Yanga ikiwa Dar, iliifanya kitu kibaya, Medeama kwa kuitandika mabao 3-0 na huo ukawa ushindi wa kwanza katika hatua ya makundi, ni bao la Mudathir Yahya tu ambalo lilikuwa ndani ya boksi na kidogo Wananchi waruhusu bao katika mchezo huo kwa mpira wa kutenga, lakini Djigui Diarra alikuwa shujaa kwa kupangua penalti ya Jonathan Sowah katika dakika ya 54.

Mvua nyingine ya mabao kwa Wananchi ilinyesha wakati wakiivaa Belouizdad, ililipa kisasi kwa kuibuka na ushindi wa mabao 4-0 na yote yalifungwa ndani ya boksi kabla ya kumaliza hatua hiyo kwa kupoteza kwa bao 1-0 dhidi ya Al Ahly.


HALI  ITAKAVYOKUWA

Kwa namna timu zote zinavyocheza na kufunga mabao ni wazi kuanzia mechi ya leo kati ya Simba na Al Ahly, lolote linaweza kutokea kwani ni timu zinazojuana kwani zimeshakutana mara nane katika michuano ya CAF tangu 1985 zilipovaana kwa mara ya kwanza katika Kombe la Washindi, kisha katika Ligi ya Mabingwa Afrika huku kukiwa hakuna mbabe kati yao.

Katika mechi ya mwaka 1985 ya Kombe la Washindi iliyochezwa Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza Simba ilishinda mabao 2-1 yaliyofungwa na Zamoyoni Magella na Mtemi Ramadhani, lakini ikaenda kupasuka 2-0 ugenini na kutolewa raundi ya pili na Al Ahly ikafika hadi fainali na kubeba ndoo.

Ndipo msimu wa 2018-2019 zikutana katika makundi ya Ligi ya Mabingwa na Al Ahly kushinda nyumbani mabao 5-0 na Simba kulipa kisasi ikiwa Kwa Mkapa kwa bao 1-0, kisha zikakutana tena katika makundi pia 2020-2021 kila moja ikashinda nyumbani bao 1-0.

Mwaka jana katika michuano mipya ya Ligi ya Afrika (African Football League) timu hizo zilitoshana nguvu kwa sare ya 2-2 jijini Dar es Salaam kisha 1-1 jijini Cairo na Wamisri wakanufaika na kanuni ya kanuni ya faina ya bao la ugenini kwani matokeo jumla yalikuwa ni sare ya 3-3.

Huenda matokeo yakaendelea kuwa upande wa Simba ikiwa nyumbani, kwani haijawahi kupoteza kwa wababe hao wa Misri, japo katika soka lolote linaweza kutokea.

Kwa upande wa Yanga na Mamelodi hii ni mara ya pili kwao kukutana katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, baada ya awali kuvaana katika raundi ya pili mwaka 2001 na Wasauzi kuopata ushindi wa 3-2 nyumbani na kulazimisha sare ya 3-3 ugenini na kuwanyoa wenyeji wao kwa mabaoa 6-5.

Timu hizo zinakutana zikiwa kila moja imeimarika zaidi kulinganisha na msimu wa 2001, hivyo soka litapigwa kesho Kwa Mkapa na ni ngumu kutabiri matokeo licha ya timu hizo kuwa na nafasi sawa ya kuibuka na ushindi.

Rekodi kwa Yanga kwa mechi za nyumbani kwa michuano ya CAF zinawabeba, huku Mamelodi kwa mechi za ugenini imekuwa ni fiftefifte litu kinachoweza kufanya mchezo huo kuwa mkali na nyota wa timu hizo ndio waliobeba hatma ya matokeo.

Bahati nzuri ni kwamba makocha wa timu zote, Rhulani Mokwena wa Mamelodi na Gamondi wa Yanga wamekaririwa mapema wakieleza ugumu wa mchezo huo na walivyojipanga ili kupata matokeo mazuri kabla ya mechi ya mwisho itakayoamua timu ipi iende nusu fainali ili kukutana na mshindi wa mchezo kati ya Esperance ya Tunisia na Asec Mimosas ya Ivory Coast.

Rekodi zinaonyesha mara ya mwisho kwa timu za Tanzania kufuika hatua ya nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika ni Simba mwaka 1974 wakati michuano hiyo ikifahamika kama Klabu Bingwa ilipovaana na Mehalla El Kubra ya Misri na kung’olewa kwa penalti 3-0 baada ya sare ya 1-1 katika mechi mbili, kila timu ikishinda nyumbani kwa bao 1-0.