Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kutoka Coco Beach Hadi Iraq, Msuva asimulia safari yake

Muktasari:

  • Mwanaspoti ikiwa katika eneo hilo kwa zaidi ya nusu saa ilishuhudia Range Rover ya kifahari ikisogea na dakika chache baadaye alishuka mshambuliaji wa kimataifa wa Tanzania, Simon Msuva, anayecheza soka la kulipwa nchini Iraq akiwa na Al-Talaba SC.

UPEPO wa Bahari ya Hindi ulikuwa ukivuma taratibu katika fukwe za Coco Beach jijini Dar es Salaam, lakini kuna ambao walikuwa wakitembea na  wengine wakifanya mazoezi mepesi ya jioni huku baadhi wakifurahia mandhari ya bahari baada ya pilikapilika za siku.

Mwanaspoti ikiwa katika eneo hilo kwa zaidi ya nusu saa ilishuhudia Range Rover ya kifahari ikisogea na dakika chache baadaye alishuka mshambuliaji wa kimataifa wa Tanzania, Simon Msuva, anayecheza soka la kulipwa nchini Iraq akiwa na Al-Talaba SC.

Ikiwa ni wiki moja tu tangu arejee nchini baada ya kumaliza msimu wa soka la kulipwa Mashariki ya Kati. Kwa wengi, likizo ni muda wa kupumzika lakini kwa mshambuliaji huyo ni muda wa kujiandaa kwa ajili ya msimu mwingine, bado anaamini kuna kazi mbele yake.

Unapomwangalia kwa macho ya kawaida unaweza kuamini kwamba Msuva amefanikiwa zaidi nyuma ya Mbwana Samatta na wala hakuna ubishi kwenye hilo. Lakini, unapokaa naye kwa dakika chache tu unagundua bado ana njaa ya mafanikio, na hilo Mwanaspoti ilibaini baada ya kupata nafasi ya kufanya naye mahojiano maalumu.

LIKIZO SIYO MUDA WA KULALA

Wakati baadhi ya wachezaji wanapotumia mapumziko kurejesha nguvu kwa kupumzika, Msuva ana mtazamo tofauti. Anaamini mwili wa mwanasoka ni mtaji ambao haupaswi kuachwa kizembe hata kwa siku chache.

Anasema mara tu baada ya kupata mapumziko mafupi, huwa anarudi kwenye programu zake binafsi za mazoezi ili kuhakikisha mwili wake haupotezi kiwango alichojenga kwa msimu mzima.

"Nimekuja kupumzika lakini bado naendelea na mazoezi, hii ni programu yangu binafsi, kabla ya kuanza mazoezi ya timu unatakiwa kwanza uwe umejiandaa mwenyewe, vinginevyo unaweza kupata majeraha au kushindwa kuendana na kasi ya timu," anasema.

Msuva anasema muda anaotumia kufanya mazoezi hutegemea programu aliyojipangia siku husika, kuna wakati hutumia saa moja na wakati mwingine hadi saa mbili.

Anasema mazoezi yake hayaishii kwenye kukimbia pekee, huchanganya mazoezi ya ufukweni, gym na yale ya kugusa mpira ili kuhakikisha anabaki katika kiwango bora.

"Huwezi kukimbia muda wote kwenye mchanga au gym ukategemea ubaki mchezaji bora, lazima pia uguse mpira mara kwa mara kwa sababu mguso wa mpira ukipungua inakuwa tatizo, ndiyo maana nikipata nafasi huwa natafuta walimu wa mazoezi ya mpira na kucheza nao," anasema.


MSIMU WA IRAQ ULIVYOKUWA

Msuva anasema Watanzania wengi hawaifuatilii kwa karibu Ligi Kuu ya Iraq kutokana na changamoto za upatikanaji wa matangazo yake, lakini ndani ya nchi hiyo ushindani ni mkubwa na kiwango kinaendelea kukua.

Anakumbusha kuwa msimu uliopita alikuwa miongoni mwa wachezaji bora wa Al-Talaba baada ya kufunga mabao 13 na kutoa asisti sita.

"Msimu uliopita ulikuwa mzuri sana kwangu, nilifunga mabao 13 na kutoa asisti sita pia tulicheza mashindano ya King Cup ambapo nilifunga bao moja kabla ya kutolewa nusu fainali kwa penalti," anasema.

Katika msimu uliomalizika hivi karibuni, takwimu zake zilishuka kidogo lakini anasema kulikuwa na sababu maalumu.

"Msimu huu nimemaliza na mabao tisa na asisti nne, watu wanaweza kuona ni tofauti na mwaka uliopita lakini nilikosa mechi nyingi sana kutokana na majukumu ya timu ya taifa," anasema.

Anakumbuka kipindi cha michuano ya AFCON kilimfanya akose takribani mechi nane za ligi, jambo ambalo lilipunguza nafasi ya kuongeza takwimu zake, kwa mchezaji anayeshindania ufungaji na nafasi ya kwanza kikosini, mechi nane ni idadi kubwa sana.

Hata hivyo, anasema bado anaridhika na alichokifanya na tayari ameanza maandalizi ya kuhakikisha msimu ujao anafanya vizuri zaidi.

"Najua nilikosea wapi na nilifanya vizuri wapi, ndiyo maana nimeanza mazoezi mapema, ninaamini msimu unaokuja utakuwa bora zaidi."

KUKUTANA NA TUISILA KISINDA

Moja ya picha zilizovutia mashabiki wa soka la Tanzania hivi karibuni ni ile ya Msuva akiwa na kiungo wa zamani wa Yanga, Tuisila Kisinda, ambaye pia anacheza Iraq.

Msuva anasema walikutana katika mchezo kati ya Al-Talaba na Al-Minaa, timu inayomiliki Kisinda.

Anasema mechi hiyo ilikuwa ngumu na ya ushindani mkubwa lakini ilimalizika kwa sare ya bao 1-1.

"Tulidro moja moja, mimi ndiyo nilifunga bao letu, ilikuwa mechi nzuri sana na yenye ushindani mkubwa," anasema.

Anamuelezea Kisinda kama mchezaji mwenye ubora mkubwa ambaye bado ana uwezo wa kucheza katika viwango vya juu.

"Kule Iraq anacheza zaidi kama 'wing back' (beki wa kushoto) ni mchezaji mzuri sana, ana nguvu, ana kasi na ana uwezo mkubwa," anasema.

Msuva anasema walifurahia kukutana baada ya miaka mingi ya kufuatilia mafanikio ya kila mmoja.

"Aliniambia siku zote alikuwa anatamani kukutana na mimi na hata mimi nilifurahi sana kukutana naye,ni mchezaji mzuri na naamini bado ana mengi ya kufanya," anasema.


MIAKA TISA NJE YA TANZANIA

Safari ya Msuva nje ya Tanzania ilianza baada ya kuondoka Yanga kwenda Difaa El Jadida ya Morocco kabla ya kuhamia Saudi Arabia na baadaye Iraq.

Katika kipindi hicho amekutana na mazingira tofauti, tamaduni tofauti na changamoto nyingi ambazo mashabiki wengi hawawezi kuziona.

"Kuishi nje si rahisi kama watu wanavyofikiria, kuna changamoto nyingi sana ambazo watu hawazioni," anasema.

Anasema changamoto za lugha, chakula, utamaduni na kuiacha familia kwa muda mrefu ni sehemu ya maisha ya mwanasoka wa kulipwa nje ya nchi, Lakini anaamini siri ya kufanikiwa ni kutokuruhusu changamoto hizo zikuzuie kufikia malengo yako.

"Kikubwa ni kufosi kazi, changamoto zipo lakini huwezi kuziacha zikushinde, ukianza kulalamika sana unaweza hata kuwakatisha tamaa vijana wengine wanaotaka kucheza nje," anasema.

Kwa zaidi ya miaka tisa, amekuwa akiishi katika nchi za Kiarabu na anasema uzoefu huo umemjenga kuwa mtu tofauti kabisa na alivyokuwa alipokuwa Yanga.

"Mungu amenijalia karibu kila ofa niliyopata imekuwa kwenye nchi za Kiarabu,kwa hiyo nimejifunza mambo mengi sana kuhusu maisha na mpira," anasema.

Anasema hata uwezo wake wa kuzungumza na kuelewa Kiarabu umeongezeka kutokana na muda mrefu aliokaa katika ukanda huo.


MAISHA YA MPIRA IRAQ

Msuva anacheka anapoulizwa kuhusu utamaduni wa mashabiki wa Iraq ukilinganisha na ule wa Tanzania.

Anasema Tanzania ni nchi yenye upendo mkubwa kwa wachezaji na mashabiki huonyesha hisia zao kwa namna ambazo si rahisi kuzikuta sehemu nyingine.

"Kule Iraq hakuna mambo ya kupewa viroba au fedha baada ya kufunga bao kama ilivyo hapa Tanzania," anasema.

Anasema baada ya mechi mchezaji huingia kwenye gari lake na kurejea nyumbani kwake kama kawaida.

"Ukifunga bao au ukicheza vizuri, watu watakupongeza sana kwenye mitandao ya kijamii, Lakini mambo ya kupewa fedha au zawadi kama yanavyotokea Tanzania hayapo," anasema.

Hata hivyo, anasisitiza kwamba hali hiyo haimaanishi mashabiki wa Iraq hawana upendo kwa wachezaji.

"Kila nchi ina utamaduni wake, Tanzania tuna ukarimu mkubwa sana, mashabiki wetu wana namna ya kipekee ya kuonyesha upendo," anasema.

Anakumbuka hata alipokuwa Yanga aliwahi kupata zawadi nyingi kutoka kwa mashabiki waliovutiwa na kiwango chake.

"Hiki si kitu kipya, hata sisi tulikipata zamani,mashabiki wa Tanzania wana moyo mkubwa sana," anasema.

Kwa mtazamo wake, jambo muhimu zaidi ni kuheshimiwa na kuthaminiwa kwa kazi unayoifanya uwanjani.

NDOTO YA KOMBE LA DUNIA

Miongoni mwa mambo yanayomgusa zaidi Msuva ni kushindwa kwa Tanzania kufuzu Kombe la Dunia 2026.

Anasema kama mchezaji, hilo lilikuwa moja ya malengo makubwa kabisa katika maisha yake ya soka.

"Nilitamani sana kucheza Kombe la Dunia ni ndoto ya kila mchezaji duniani," anasema.

Anasema kushiriki michuano hiyo kungebadilisha sura ya soka la Tanzania na kuwapa wachezaji nafasi kubwa zaidi katika soko la kimataifa:"Tungekuwa kwenye Kombe la Dunia, CV ya Tanzania na ya wachezaji wetu ingekuwa kubwa sana," anasema.

Msuva anafananisha AFCON na Kombe la Dunia akisema tofauti ya ukubwa wa mashindano hayo ni kubwa sana.

"AFCON ni mashindano makubwa lakini Kombe la Dunia ni hatua nyingine kabisa," anasema.

Anasema bado hajakata tamaa kwa sababu soka lina mambo mengi yasiyotabirika.

"Mungu akipenda bado inaweza kutokea siku moja,hakuna kinachoshindikana," anasema.


KILIO CHAKE KIKUBWA

Pamoja na mafanikio yake binafsi, jambo ambalo Msuva analitamani zaidi ni kuona Watanzania wengi wakicheza soka nje ya nchi.

Anasema mara kwa mara mawakala wa kimataifa wanamtafuta wakitaka kupata taarifa za wachezaji wa Tanzania.

"Nimekuwa nikipigiwa simu mara nyingi na mawakala wakitaka mawasiliano ya wachezaji mbalimbali wa Tanzania."

Anasema mara zote amekuwa tayari kusaidia kwa kutoa taarifa hizo, lakini maamuzi ya mwisho hubaki kwa mchezaji mwenyewe na klabu yake.

"Mimi kazi yangu ni kuunganisha watu,baada ya hapo maamuzi yanakuwa ya mchezaji na timu yake," anasema.

Kwa mtazamo wake, kucheza Simba, Yanga au Azam ni hatua kubwa lakini kwenda kucheza nje ni hatua nyingine muhimu zaidi.

"Ningependa kuona Watanzania wengi wanacheza nje kwa sababu inasaidia maisha yao, lakini pia inasaidia timu ya taifa," anasema.

Anasisitiza kuwa Tanzania ina vipaji vya kutosha vinavyoweza kufanikiwa katika ligi mbalimbali duniani.

"Tatizo si talenti, talenti tunazo nyingi sana, kinachohitajika ni ujasiri wa kuchukua hatua, " anasema.

MAISHA YAKE YALIVYOBADILIKA

Licha ya kuwa tayari alikuwa nyota mkubwa ndani ya Yanga, Msuva anasema uamuzi wa kwenda kucheza nje ya Tanzania ndiyo uliobadilisha maisha yake kwa kiwango kikubwa zaidi.

Anakumbuka wakati alipopata ofa ya Difaa El Jadida ya Morocco kulikuwa na watu waliokuwa na mawazo tofauti, wengine wakiona ni wakati sahihi wa kwenda kutafuta changamoto mpya na wengine wakiamini bado alikuwa anahitajika zaidi ndani ya Yanga.

Kwa mujibu wa Msuva, kucheza nje kulimfundisha mambo mengi ambayo asingeyapata kama angebaki ndani ya nchi, alijifunza namna ya kuishi katika mazingira tofauti, kushindana na wachezaji kutoka mataifa mbalimbali na kujenga uwezo wa kujitegemea katika maisha ya kila siku.

"Kucheza nje kulinibadilisha sana, sio tu kama mchezaji bali hata kama mtu, kuna vitu vingi unajifunza ukiwa mbali na familia na marafiki zako, inakufanya uwe na uwajibikaji mkubwa zaidi kwenye maisha yako," anasema Msuva.

Anasema kila hatua aliyopitia tangu Morocco hadi Iraq imekuwa sehemu muhimu ya safari yake ya mafanikio na ndiyo sababu anawashauri vijana wengi kutokuwa na hofu ya kutoka nje ya Tanzania wanapopata nafasi.


KUMBUKUMBU YA BAO ANALOLIPENDA

Katika maisha yake ya soka, Msuva amefunga mabao mengi muhimu kwa klabu na timu ya taifa, hata hivyo, anasema yapo baadhi ya mabao ambayo yamebaki kwenye kumbukumbu zake kutokana na umuhimu wake kwa Taifa Stars na mashabiki wa Tanzania.

Anakiri kuwa kila anapokumbuka baadhi ya mechi za kufuzu AFCON au ushindi dhidi ya timu kubwa barani Afrika, hupata fahari kubwa kuona mchango wake katika mafanikio hayo.

"Kila bao lina historia yake, kuna mabao unafunga lakini baada ya muda watu wanayasahau, Lakini kuna mengine yanabaki kwenye mioyo ya mashabiki kwa miaka mingi kwa sababu yalikuwa muhimu kwa taifa," anasema.

Kwa mtazamo wake, mafanikio makubwa zaidi si idadi ya mabao aliyofunga bali kuona mabao hayo yakiisaidia Tanzania kufikia malengo yake katika mashindano mbalimbali ya kimataifa.

"Nakumbuka ilikuwa mechi muhimu sana kwetu dhidi ya Guinea jamaa walikuja Tanzania na wachezaji wao wote muhimu akiwemo mmoja ambaye anaichezea Borussia Dortmund (Serhou Guirassy), tulipambana na nakumbuka nilifunga bao ambalo lilitupeleka Afcon," anasema.


ANAVYOITAZAMA YANGA YA SASA

Ingawa kwa sasa anacheza nje ya nchi, Msuva bado anaendelea kufuatilia mwenendo wa Yanga, klabu iliyompa umaarufu mkubwa katika soka la Tanzania.

Anasema bado ana marafiki wengi ndani ya kikosi hicho na huwa anafuatilia mechi zake mara kwa mara anapopata nafasi.

Mafanikio ambayo Yanga imekuwa ikiyapata katika miaka ya karibuni yanaonyesha namna klabu hiyo ilivyopiga hatua kubwa katika maeneo mbalimbali ndani na nje ya uwanja.

"Yanga ni sehemu ya maisha yangu ya soka,nimekaa pale kwa muda mrefu na nimepata mambo mengi mazuri,nikiona timu inafanya vizuri huwa naona ni jambo jema," anasema.

Anaamini ushindani kati ya Yanga na Simba umechangia kwa kiasi kikubwa kukuza kiwango cha soka la Tanzania na kuvutia macho ya watu wengi kutoka nje ya nchi.

Anasema kadri timu hizo zinavyoendelea kufanya vizuri katika mashindano ya kimataifa, ndivyo zinavyoongeza thamani ya wachezaji wa Tanzania katika soko la kimataifa.

KINACHOMBEBA TAIFA STARS

Katika kipindi ambacho kizazi kipya cha wachezaji kinaendelea kuibuka, Msuva bado ameendelea kuwa sehemu ya wachezaji wanaoaminiwa ndani ya Taifa Stars,wengi wamekuwa wakijiuliza ni nini hasa kinachomfanya aendelee kuwa na nafasi katika timu hiyo licha ya ushindani mkubwa uliopo.

Anasema siri kubwa ni kutoridhika na mafanikio ya jana, kwa mujibu wake kila anapoitwa timu ya taifa hujiona kama mchezaji mpya anayepaswa kuthibitisha uwezo wake upya.

"Ukianza kuamini kwamba nafasi yako ni ya kudumu unakuwa umeanza kushuka,mimi kila ninapoitwa timu ya taifa najiona kama ninaenda kupambania nafasi yangu upya," anasema.

Anaongeza kuwa kucheza nje ya nchi kumemsaidia kukutana na aina mbalimbali za mifumo ya uchezaji na ushindani mkubwa, jambo ambalo limeendelea kumjenga kisoka.

Kwa sababu hiyo, bado anaamini ana uwezo wa kuchangia mafanikio ya Taifa Stars katika miaka ijayo.


UJUMBE WAKE KWA KIZAZI KIPYA

Mwishoni mwa mazungumzo yetu, Msuva anatuma ujumbe maalumu kwa vijana wanaoota kufikia mafanikio aliyoyapata katika soka,anasema jambo la kwanza wanapaswa kulifanya ni kuamini uwezo wao wenyewe kabla ya kutaka watu wengine wawaamini.

Anasisitiza kuwa vipaji vya Tanzania havina tofauti kubwa na vya nchi nyingine ambazo zimeendelea kisoka, kinachohitajika ni kujituma, kuwa na nidhamu na kutokuwa na hofu ya kuchukua hatua kubwa katika maisha.

"Vijana wa Tanzania wana uwezo mkubwa sana, ninachowaomba ni wasikate tamaa na wasiwe na hofu ya kujaribu changamoto mpya,wakiendelea kufanya kazi kwa bidii wanaweza kufika mbali zaidi kuliko sisi tulivyofika," anasema.

Anasema mafanikio ya mchezaji mmoja hayapaswi kuwa mwisho wa safari, bali yanapaswa kuwa daraja la kuwafungulia wengine milango mipya.

"Natamani kuona miaka michache ijayo tukizungumza kuhusu Watanzania wanaocheza nje tusitaje Msuva na Samatta pekee, natamani tuwe na majina mengi zaidi yanayocheza katika ligi mbalimbali duniani."