Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wanaohoji weledi wa Kihwelo na mustakabali wa makocha wetu

Muktasari:

  • Wachambuzi wengi wamekuwa wakihoji kama Jamhuri ana weledi au la na huwa anazungumza kama kocha au shabiki wa Simba kila wakati anapokuwa na mechi dhidi ya Yanga.

KWA takriban wiki mbili sasa mjadala mkubwa umekuwa juu ya kauli za kocha wa Mashujaa FC, Jamhuri Kihwelo kabla na baada ya mechi ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Yanga iliyoisha kwa mabingwa hao watetezi kuibuka na ushindi wa mabao 2-0.

Wachambuzi wengi wamekuwa wakihoji kama Jamhuri ana weledi au la na huwa anazungumza kama kocha au shabiki wa Simba kila wakati anapokuwa na mechi dhidi ya Yanga.

Jamhuri aliwaponda wachezaji wageni wanaokuja Tanzania kuwa hawana kiwango kikubwa, akijenga hoja kwamba kama wana viwango vya juu wangeenda barani Ulaya ambako maslahi ni mazuri zaidi.

Jamhuri pia alihoji wafungaji wa mabao wa Yanga kwamba ni raia wa nchi gani baada ya Mudathir Yahya na Bakari Mwamnyeto kuifungia Yanga mabao katika mechi dhidi ya Mashujaa, akitaka kuongeza uzito kwenye hoja yake kuhusu viwango vya wachezaji kutoka nje ya nchi.

Na kibaya zaidi, bila hata kuulizwa swali kuhusu Simba, Jamhuri aliiponda safu ya ushambuliaji ya Yanga kuwa haina makali zaidi ya ile ya Simba. Haikueleweka aliingiza Simba kwenye mahojiano hayo kwa sababu gani wakati alikuwa akihojiwa kuhusu mechi ambayo Mashujaa wangecheza na Yanga wiki iliyopita.

Kauli hizo ambazo hazina uwiano na kilichotokea uwanjani ni za kawaida kwa mchezaji huyo wa zamani wa Simba na ambaye hajasema ni shabiki na mwanachama wa Simba na ambaye amekuwa akitoa kauli dhidi ya uongozi wa klabu hiyo mara kwa mara.

Kuna msimu ambao Yanga iliibuka na ushindi wa mabao manane dhidi ya Coastal Union, lakini baada ya mchezo huo Jamhuri alisema ingekuwa mechi dhidi ya Simba, timu yake ikifungwa hata mabao kumi.

Waandishi walishangaa kwa kuwa hakuwepo hata mmoja aliyemuuliza swali la kufananisha au kuulizia kama Coastal ingekutana na Simba ingekuwaje. Na msimu huo, Simba haikuweza kuishinda Coastal kwa zaidi ya mabao matatu. Unashangaa kauli hiyo ya kufananisha Simba na Yanga ilitoka wapi wakati mechi ilikuwa kati ya Coastal na Yanga.

Wachambuzi na wengine wana haki ya kuhoji juu ya Jamhuri kwa kuangalia kauli kama hizo ambazo zinatakiwa zitolewe na mashabiki na si kocha wa Ligi Kuu. Ni muhimu sana kwa Jamhuri kuanza kutafakari mwenendo wake, hasa anapokuwa kwenye ajira kama hiyo ya kuifundisha Mashujaa kwa kuwa ndio kitu kinachoangaliwa na waajiri.

Kauli kama hizo pia zinaondoa utamu wa matokeo ya mechi za Ligi Kuu na kusababisha ionekane kama kuna mechi huwa zinapangwa. Nani ataamini kwamba Mashujaa imefungwa kihalali na Simba kama kocha mwenyewe anatoa kauli kama hizo za kuisifu Simba katika mechi ambayo klabu hiyo haikucheza na wala hakukuwepo na swali linaloihusu?

Kama ni kuponda wachezaji wa kigeni, waajiri wake wanakuwa kwenye mazingira gani iwapo walikuwa wanafikiria kusajili nyota kutoka nje ya nchi? Na vipi waajiri wengine wenye timu zenye wachezaji wageni ambao labda walikuwa wanafikiria kumuajiri Jamhuri awe kocha wao?

Inakuwaje kwa mchezaji mgeni aliye katika kikosi chake? Je, wachezaji wageni ambao si wazuri ni wale wanaochezea Yanga peke yake? Vipi kwa wageni waliosajiliwa Simba?

Tunaweza kudhihaki kwamba viongozi wa klabu za soka za Tanzania wanajali sana makocha wageni, lakini ukiangalia weledi wao katika kuzungumzia mechi na wachezaji wao unaona tofauti kubwa sana iliyopo dhidi ya baadhi ya makocha wetu wazawa.

Wapo ambao huonyesha heshima kwa wapinzani wao hata kama wana uhakika wa kushinda mechi dhidi yao. Wanajua mpira wa miguu una mambo mengi yanayoweza kuathiri matokeo.

Hata Pep Guardiola angekuja na Manchester City hapa nchini na kupangiwa mchezo dhidi ya KMC asingeweza kutoa maneno ya dharau kwa sababu tu timu hiyo kutoka Kinondoni inashika mkia au kwa sababu ameshaiongoza City kutwaa hadi ubingwa wa Ulaya.

Anajua kuwa mpira wa miguu una mambo mengi. Usingetegemea Dodoma Jiji iibuke na ushindi dhidi ya Yanga. Ingekuwaje kama kocha wa Yanga angeiponda timu hiyo na wachezaji wake kabla ya mechi? Weledi ni kitu muhimu kwa tasnia yoyote ile na wale wanaoheshimu weledi si wajinga, bali wanajua kuwa taaluma yao iliwekewa misingi hiyo kwa makusudi maalumu.

Ni muhimu kwa Jamhuri kutafakari mwenendo na kauli zake mbele ya waandishi wa habari kama zinazingatia weledi.