Kumbe hata Yanga nayo ni masikini wa wachezaji
Muktasari:
Lakini unaweza kuwa na wachezaji wafupi wakacheza vizuri sana nafasi za viungo ama mabeki wa pembeni. Hapa ndipo unaweza kuanza kuuona umasikini wa Yanga kwa kutokuwa na wachezaji wanaoiva kimaumbile katika nafasi wanazocheza.
BAADA ya kumalizika kwa michuano ya Kombe la Mapinduzi juzi Jumanne usiku na Simba kutwaa taji, sasa mawazo ya wadau wengi wa soka yataanza kuelekezwa ndani ya timu mbili kama si nne zinazoiwakilisha Tanzania katika mashindano ya kimataifa ya klabu, Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho.
Ni wazi ukiitaja Tanzania utalazimika kuzitaja na timu za Zanzibar, ingawa katika uwakilishi wao wa miaka mingi, timu za Zanzibar zimekuwa zikifanya vibaya zaidi. Kwa msingi huo nitajikita zaidi kuzizungumzia timu za Bara, yaani Azam na Yanga.
Bila shaka hizi ndizo zinazoonekana kuwa na vikosi vyenye wachezaji mahiri kiasi, licha ya kwamba nazo huwa zinafungwa kila mara. Hata hivyo, ndizo timu zinaongoza kwa kuwalipa wachezaji mishahara mikubwa sawa na ilivyo kwa Simba, ukilinganisha na timu nyingine za nchini.
Kwa maana hiyo, timu hizi zina utajiri wa kupata wachezaji walio bora hata kama wapo katika kikosi cha timu ya Taifa, bado watajiona wanapungukiwa kitu.
Katika uwepo wake wa kwanza nchini, kocha Marcio Maximo, alipokuwa akiinoa Taifa Stars wachezaji wengi waliokuwa wakiunda kikosi hicho walikuwa wakitoka Mtibwa Sugar, miongoni mwao ni Mecky Maxime, Amir Maftah, Dickson Daudi, Shaban Nditi, Nizar Khalfan, Abdi Kassim pamoja na Kigi Makasi. Lakini baada ya muda mfupi, wanne kati yao walihama.
Ninachotaka kusema hapa ni kuwa Azam na Yanga zina utajiri wa wachezaji mahiri, lakini ni namna gani wanatumika, namna gani wanapata motisha na namna gani wanatibiwa kisaikolojia, hilo ni suala jingine.
Lakini ukiwafanyia tathimini wachezaji wa Yanga mmoja mmoja katika nafasi zao huku ukizichukua sifa kamili za wachezaji na majukumu yao uwanjani, bila shaka utagundua Yanga ina umasikini mkubwa wa baadhi ya namba.
Si kila anayecheza nafasi ya ushambuliaji anastahili kuitwa straika, vivyo hivyo kwa nafasi nyingine vilevile. Kila nafasi ina sifa zake, hata maumbile nayo ni sehemu ya sifa hizo, hauwezi kuwa mfupi wa kimo cha Mrisho Ngassa halafu ukacheza kwa mafanikio beki ya kati au mshambuliaji wa kati.
Lakini unaweza kuwa na wachezaji wafupi wakacheza vizuri sana nafasi za viungo ama mabeki wa pembeni. Hapa ndipo unaweza kuanza kuuona umasikini wa Yanga kwa kutokuwa na wachezaji wanaoiva kimaumbile katika nafasi wanazocheza.
Yanga haina mabeki wazuri wa pembeni, ila inao wachezaji wanaocheza katika nafasi hizo. Mwangalie Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ wa Simba na Oscar Joshua wa Yanga, utagundua kuwa Joshua hana furaha kabisa akicheza nafasi hiyo.
Pamoja na kuwa anatumia mguu wa kushoto, lakini hana amani. Joshua hana unyumbufu (flexibility), hana wepesi wa miguu na kibaya zaidi anakosa utulivu, hauwezi kumuona Joshua akipanda kila mara kwenda kupiga krosi na hata akipiga krosi, huwa si krosi sahihi.
Hana tofauti na Edward Charles Manyama, wote wapo taratibu. Hakuna tofauti na kulia aliko Mbuyu Twite ambaye naye si mnyumbufu wala hana ule wepesi wa beki wa kulia, humkuti akipanda kila mara. Wote hawa wanakaba muda wote.
Tunamuona Hassan Kessy wa Simba, kimo chake kifupi kinamfanya kuwa mnyumbufu na mwepesi, hili halihusiani na mfumo wa kocha. Si kweli kwamba makocha wanawalazimisha wachezaji hawa wasipande, bali ni aina ya uchezaji wao ndivyo ulivyo. Hawa akina Twite, Joshua na wenzao wanaweza kucheza vizuri kabisa wakiwa mabeki wa kati badala ya nafasi wanazocheza sasa.
Mara nyingi mabeki wa pembeni huwa wafupi kiasi wenye kukimbia kwa kuchanganya hatua fupi fupi, si warefu wa kimo cha akina Edward. Kilichopo hapa ni umasikini wa wachezaji.
Waangalieni akina Patrick Evra, Ashley Cole, Philip Lahm, Dan Alves na wengineo wa barani Ulaya. Nenda Uganda utamkuta Dan Walusimbi na kimo chake, hizi ndizo sifa za beki wa pembeni. Hutokea mara chache wachezaji warefu wakacheza vizuri pembeni, ikiwa hivyo basi itatokana na akili yake zaidi kama ilivyokuwa kwa Keneth Mkapa.
Kwa Yanga umasikini huu wa kutokuwa na wachezaji stahili wa pembeni, ni makosa ya usajili unaofanywa na watu wasio na ufundi wa soka.
Hili liendelee kuwa funzo kwa timu zetu kwani si kila mchezaji anayetumia mguu wa kushoto ni beki wa pembeni, anaweza kucheza hata ulinzi wa kati.
Kama nilivyosema, Yanga na Azam, zinatuwakilisha kwenye michuano ya kimataifa, lakini zitapata tabu sana kujenga mashambulizi pale wachezaji wao wa mbele watapokuwa wamebanwa.
Wauchukue mchezo wa Yanga na JKU kama funzo mojawapo. Mabeki wa kati na wa pembeni wa JKU walibana njia kubwa iliyokuwa ni kupitisha mashambulizi pembeni.
Lakini kama mabeki wenyewe hawapandi na wala kuonyesha kutaka kupanda, walinzi hao hawana hamu ya kupanda ili kupiga krosi bila shaka timu itakuwa na nafasi finyu ya kutengeneza mashambulizi. Siku si nyingi tutaona ingizo la mabeki wa pembeni wanaotumia mguu wa kushoto kiufasaha kwenye timu yetu ya Taifa badala ya hawa waliopo.
Ni rahisi kwa kocha wa Taifa Stars kuanza kumtumia David Luhende kama atarudi kwenye nidhamu ya uchezaji pamoja na Mohamed Hussein kwa sababu wanaitumia miguu yao ya kushoto kwa ufasaha zaidi. Hawa unaweza kuona tofauti ndani yao pale wanapopiga krosi kwani kiufundi krosi ni pasi ikiwa na maana mpira unatakiwa kupigwa alipo mchezaji na eneo analotakiwa kuwapo mshambuliaji, katika hili ndipo tunaweza kusema Yanga haina budi kurekebisha hali hii huku ikijua inakwenda kwenye michuano mikubwa.
Kwa muda uliopo, haitaweza kufanya mabadiliko ya wachezaji, badala yake ilazimishe kuingiza mabadiliko haya kifikra, lakini ijipange vizuri miaka ijayo.