Kudra Omary: Pacome ananikumbusha enzi zetu zamani

Ukiwataja mastaa wa Yanga ambao kwa sasa ni vipenzi vya mashabiki basi hutaacha kuwataja Pacome Zouzoua, Aziz Ki Stephane na Maxi Nzengeli.

 Sio siri utatu wao unawavutia wengi na wote wameingia kambani mara kadhaa katika kuhakikisha timu yao inapata matokeo.

Aziz Ki ana mabao 10, Maxi saba na Pacome manne na mbali na kufunga, kile wanachofanya uwanjani, ni burudani kwa mashabiki wa timu hiyo.

Hata hivyo, kwa Pacome, huwaambii kitu mashabiki wa timu hiyo kwa sasa, si kwenye Ligi Kuu Bara pekee, kimataifa ana balaa lake na hilo limemfanya nyota wa zamani wa Yanga, Kudra Omary kushindwa kuficha hisia zake kwa Muivory Coast huyo na kumtaja kama ndiye anayemkosha sana kwa sasa.

Pacome amefunga pia mabao mawili kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika na ndio kivutio zaidi kwa mashabiki licha ya Kudra kumtaja pia Aziz Ki na Yanga kwa jumla imekuwa moto na Kudra akihojiwa na Mwanaspoti anafunguka mengi ikiwamo ishu ya ushirikina na uchinjaji wa mbuzi wa kafara.


Pacome hatari

Kudra anasema, “Yanga mwanzo ilikuwa inacheza bila kutafuta bao, lakini sasa inajua inachokifanya ili kupata matokeo mazuri, ina kasi na wachezaji wote na wanacheza kitimu.

“Nilikuwa nacheza namba 10 ama winga, kwa sasa kusema kweli mtu kama Pacome ananikosha sana, anapita mule mule tulimopita sisi, ana uwezo binafsi na anaamua namna ya kutafuta bao, sio mchoyo kwamba afunge mwenyewe. Pacome ananikumbusha mengi ya nyuma.

“Zamani mpira ulichezwa na watu wenye vipaji na bila kipaji huchezi ila siku hizi unafundishwa na unacheza.” anasema Kudra


HAKUWA TEGEMEO

Anasema alisajiliwa Yanga akitokea timu ya daraja la chini iliyoitwa Muheza Shooting hivyo alivyotua Yanga haikuwa rahisi kuanza kikosini moja kwa moja.

“Wakati naanza Yanga sikuwa tegemeo, nikiwa chini ya Kocha, marehemu Jack Chamangwana maana ndiye anayeangalia mchezji huyu ana uwezo gani, anaweza kubadilishaje mchezo hasa timu isipokuwa na matokeo mazuri.

“Alikuwa ananianzishia benchi na nikiingia kuna kitu nakifanya anafurahia, ilikuwa ngumu kwangu maana niliwakuta mastaa kama Edibily Lunyamila, Sekilojo Chambua halafu mimi nimetoka ligi ndogo, hivyo haikuwa rahisi kupata nafasi ya kucheza kikosi cha kwanza hasa kwa hizi timu kubwa.

“Kama unafanya vizuri basi hata wachezaji wakongwe ndani ya timu watamshawishi kocha ili awe anakutumia, hivyo wakawa wanamwambia kocha ili nicheze ila aliwaambia ataangalia mechi za kunipa lakini sio za Dar es Salaam ambazo zinakuwa na presha

“Simba na Yanga wanapenda kushinda, matokeo yakiwa tofauti na matarajio yao lazima shida itokee, kocha aliniambia akinianzisha inampa wakati mgumu kuliko nikianzia benchi nampa matokeo, ingawa mwishoni nikawa naanza hadi namaliza,” anasema.


MASHABIKI WAANDAMANA ASAJILIWE

“Sikwenda Yanga kupitia mkono wa mtu mmoja, bali ni mashabiki ndio walishinikiza nisajiliwe baada ya kuniona kwenye mechi pale Uwanja wa Karume nikiwa na timu yangu ya Muheza Shooting.

“Tulicheza mechi ya kwanza mashabiki wa Yanga waliojiita Mashabiki Bomba, walivutiwa na uwezo wangu wa kucheza, ndipo waliandamana mashabiki kama 30 kwenda pale Jangwani na walionana na viongozi, wakawaambia.

“Lakini kwa vile hakuna aliyenifahamu viongozi wa Yanga walikuja wakati wa mechi yetu ya pili hapo hapo Karume, waliongozwa na Katibu Mkuu wa wakati huo, Marehemu Abdul Sauko alianza kunifuatilia, alitaka kujua ninapoishi ingawa ilimpa wakati mgumu kunipata kwani kipindi hicho hakukuwepo na mambo ya simu,” anasema na kuongeza;

“Nafikiri uwezo wangu tu ndiyo walivutiwa nao, nilivyokuwa na mpira, kudribo na mambo mengine ya uwanjani, niliweza kucheza kwa kweli. Namna walivyonipata Yanga na kunisajili, ilibidi wamtumie dereva wao aliitwa Sharif.

“Sharif aliwasikia viongozi wakisema kuna mchezaji anaitwa Kudra tunamtaka ila hawajui watanipata wapi, akawaambia mimi ni mdogo wake na anafahamu ninapopatikana, wakamwambia asiponipeleka basi na yeye itakuwa ndiyo mwisho wake wa kuendesha hilo gari. Sharif alikuwa anapafahamu nyumbani hivyo ilikuwa rahisi kunipata, alinichukua na kunipeleka Jangwani.”


USAJILI WA SH1 MILIONI

“Zamani hakukuwa na mambo ya mikataba yenye masharti kama sasa hivi, tulisaini mkataba wa kila msimu ukiisha unasaini tena, mkataba wangu wa kwanza naingia Yanga nilipewa fedha ya kawaida tu ya Sh1 milioni.

“Nilikaa Yanga miaka mitano na kila msimu ukiisha naongeza kwa makubaliano tofauti, mkataba wa mwisho nilisaini Sh3 milioni ilikuwa mwaka 2016. Na kwa kipindi nilichokuwepo tulichukua ubingwa wa ligi kwa misimu mitatu, hivyo ni misimu miwili tu sikuchukua ubingwa.”


ISHU YA UFUNGAJI TUSKER

“Mwaka 2007 nilipojiunga Mtibwa Sugar nilishiriki mashindano ya Tusker Cup, wakati huo nimetoka Yanga, niliibuka Mfungaji Bora wa mashindano hayo, Mtibwa ilikuwa timu kweli kweli wakati huo, tukikosea tunaambiza, tunatafuta ushindi kwa pamoja, mshikamo ulikuwa mkubwa.

“Niliondoka Yanga sio kwa kushuka kiwango, niliingia Yanga nikiwa mdogo nimeondoka nikiwa na miaka 24, hivyo wakati uwezo wangu ndo unazidi kuwa mkubwa zaidi Yanga hawakunifaidi, Mtibwa ndio walinifaidi vizuri, kwenye soka kadri umri unavyozidi kwenda ndio uwezo unaongezeka.

“Mtibwa nilikaa misimu miwili, baada ya mkataba kumalizika kuna vitu havikukaa sawa hivyo niliwaambia nataka kifanyike hiki na hiki wakashindwa ndipo nikaamua kuondoka kwenda Moro United,” anasema Kudra.


AMKIMBIA MINZIRO MAZOEZINI

“Moro United ilikuwa msimu mmoja, tulishindwana kwenye makubaliano ya mkataba kwani tulikubaliana ratiba ya mazoezi ya mara moja kwa siku, kufanya asubuhi tu, lakini baadaye kocha akasema tunafanya asubuhi na jioni tulikuwa chini ya Kocha Fredy Felix ‘Minziro’.

“Ilikuwa vigumu kwangu nitoke Tegeta asubuhi niende mazoezini  Kariakoo, mara mbili kwa siku, ndipo niliwaambia nipo tayari ila mnipangie chumba huko Kariakoo nikitoka mazoezini nipate sehemu ya kupumzika ili niweze kufanya mazoezi ya jioni.

“Ratiba ilikuwa ngumu sana, mazoezi yanaanza saa 2 hadi 5 asubuhi, niende Tegeta halafu saa 8 nipande gari kurudi Kariakoo, muda unakuwa hautoshi, na ni mbaya kwa afya maana sipumzishi mwili, walisema hawawezi hivyo tulishindwana kwa namna hiyo.

“Kama kuna vitu vimeongezeka upande wao basi na kwangu viongezwe, mbaya zaidi hii mikataba huwa tunakubaliana na viongozi, makocha sio sana, ndo mpira wa Tanzania. Kocha anasema anamtaka mtu fulani wao wanatekeleza, sasa shida inakuja wakati wa utekelezaji wa majukumu upande wa mchezaji, kocha anataka yake na wewe makubaliano yako na viongozi ndio unayasimamia,” anasema na kuongeza;.

“Sikumaliza msimu, niliishia nusu nikabaki nyumbani maana hawakutaka kunisikiliza kwasababu wanataka ufuate yao, mchezaji anapaswa kupewa muda wa kupumzika ili kiwango chake kiwe kizuri ingawa pia mchezaji anapaswa kujiongeza kwa  mazoezi binafsi.”


MIAKA SITA NJE YA UWANJA

“Baada ya kutoka Moro United nilipumzika soka, sikutaka tena mambo ya soka, unacheza kwa masilahi yako na klabu, lakini kama klabu inafaidika yenyewe mchezaji hafaidiki haina maana, mwisho wa soka kuna maisha mengine, kama haukulipi ni kazi bure, maana mchezaji unaweza kuwa ombaomba mtaani.

“Nilipumzika kwa miaka sita bila kucheza ligi kuu, baadaye nilienda JKT Mlale waliniomba niwasaidie, nilienda na tulikubalia wanime kila nilichotaka.

Wakati nasajiliwa zilibaki mechi kadhaa tu za kumalizia wakanilipa pesa ya usajili na mshahara, ilikuwa nafasi ya mwisho ikishika mkia ila ikamaliza nafasi ya tatu,” anasema na kuongeza;

“Niliendelea nao msimu mwingine, timu ilimaliza nafasi ya pili, baadaye Majimaji walinifuata tukakaa mezani tukamalizana lakini nao kama wale wale wa kwanza mnakubaliana baadaye inakuwa siyo na shida ilikuwa  ni mshahara.

“Ninapokuwa kazini, nyumbani wananitegemea na wanaamini napata pesa, huwezi kueleweka kabisa, nashukuru niliweka baadhi ya vitega uchumi ndivyo vikawa vinaisaidia familia, msimu ulipoisha na timu imepanda daraja nilikataa kuongeza mkataba.

“Ligi Kuu ina muda mrefu kuliko Championship, maana walikuwa hawajanilipa mishahara ya miezi mitatu, niliona nikisaini kucheza ligi kuu ni kujiingiza kwenye moto zaidi. Ndipo nikaenda KMC wakati inashiriki Championship.

“Hapo hakukuwa na longolongo ikifika muda unalipwa ikichelewa labda wiki moja ila sio mwezi jambo ambalo ni la kawaida, nimecheza msimu mmoja kabla haijapanda, ndipo nikaamua kuacha kabisa kucheza soka. Nilicheza ule msimu ambao kocha alichezesha wachezaji wengi katika mchezo mmoja, tulinyang’anywa pointi ambazo zilituruhusu kupanda ligi kuu hivyo tukashika nafasi ya pili.”


KUSTAAFU SOKA, AWAPA SOMO MASTAA

“Wakati mwingine unalazimishwa kustaafu, maana kama unapata kipato kidogo mchezaji unakuwa huna thamani.

“Napenda kuwaweka wazi wachezaji wengi wanaotoka nje ya Dar es Salaam, hili jiji lina mambo mengi, wakifika wanapokelewa na jiji ndipo kazi iliyowaleta inaishia hapo. Kuna raha nyingi, viwango vinashuka. Ila watambue mashabiki wanaumia sana wakikosa matokeo mazuri, mchezaji anaumia moyoni na maumivu yanakuja zaidi baada ya mechi, mkifungwa.

“Jikataze baadhi ya vitu kufanya ili kiwango chako kibaki vile vile, ukishindwa kujitunza basi huo ndio unakuwa mwisho wako, hii inasababisha pia wachezaji wengi wa sasa kushindwa kufanya vizuri kwa muda mrefu, starehe nyingi wanafanya, ndio maana wanastaafu mpira kabla ya umri wao.”


MCHINJA MBUZI WA MECHI

Kudra anasimulia moja ya mkasa aliokutana nao akiwa Maji Maji ni juu ya imani za kishirikina. Anasema mambo haya yapo ila hayasaidii lolote bali ni kama tamaduni tu.

“Mnaweza mkaambiwa mnawe maji yenye dawa, nakumbuka nikiwa Maji Maji niliteuliwa kuchinja mbuzi kwa ajili ya kupata ushindi, nikawaambia nikichinja nusu ya nyama nachukua mimi, hawakunipa na tulipoteza ile mechi.

“Ikaja mechi nyingine napo walitaka nichinje nikagoma, huwa siogopi kuchinja ndio maana nilikuwa nakubali na niliamini hizo ni imani tu hakuna kitakachotokea uwanjani na kuwapa matokeo mazuri kama hamjajiandaa vizuri. Kama ushirikina ungekuwa unatupa matokeo mazuri basi mazoezi tusingekuwa tunafanya.

“Ni kweli wachezaji wengi wanadai wanarogana, ila naamini mchawi wako wa kwanza ni wewe mwenyewe namna unavyojitunza, kuheshimu kazi yao na sio kuendekeza starehe zinazokushusha kiwango, hii ipo kwa wachezaji, baadaye wanakimbilia kuambizana wanarogana, ingawa kuna baadhi ya wachezaji bila kufanya hayo mambo anaona kazi yake haiendi.”


WAGENI/WAZAWA

Kanuni zinaruhusu kusajili wachezaji 12 wa kigeni ambao wote wanaruhusiwa kutumika kwenye mechi moja kadri kocha atakavyoamua, Kudra anazungumzia hili;

“Hakuna ubaya, ubaya ni pale wachezaji wazawa wanapoona wageni wamesajiliwa wanakata tamaa, wanaamini wamekuja kuchukua nafasi zao, lakini ukweli ni wachezaji wa kawaida na wazawa wakiamua kupambana nao watapata nafasi ya kucheza kama wao.

“Tanzania ina wachezaji wengi wazuri ila kama nilivyosema awali hawajitunzi. Kuna wengine wanajitunza lakini timu zikiwachoka wanawaambia wazee, uwezo umeisha, jambo ambalo sio sahihi,” anasema mkongwe huyo ambaye amewahi kupewa kadi tatu nyekundu kwenye mechi za ligi kuu, moja akiipata walipocheza na Simba kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha.


HAPENDI WAAMUZI WA KIKE

“Napenda kuchezeshwa na mwamuzi wa kiume, maana wanawake wana tabaia za kujihami, mnaweza kutofautiana tu kidogo basi atakuambia kwa vile mimi mwanamke, wakati ukiwa uwanjani anatambulika ni mwamuzi.

“Wanawake wanafanya vizuri lakini siwi huru wakichezesha, kukimbia mle ndani si mchezo, mwili ukipata joto unaweza kumjibu mtu tofauti na yeye akaona umemdharau kwa vile ni mwanamke, ukimwambia kitu anakwambia chukua njano ukiongea tena nyekundu kumbe mtu umechemka tu. Wanaume wanaelewa ila hatuwadharau na tunawaheshimu dada zetu, ingawa wana majibu mabaya wakati mwingine wanapokumbushwa,”


TAIFA STARS

“Nilitamani siku moja tucheza Fainali za Afcon kweli yametimia, nakiona kikosi ni kizuri na kitafanya vyema, kilichobaki ni kumwachia kocha afanye kazi yake pasipo kuingiliwa. Tuna wachezaji wazuri na wapambanaji, zaidi wakaongeze upambanaji,” anasema Kudra mwenye watoto wanne, watatu wa kike na mmoja wa kiume anayedai anapenda kucheza soka.