Kocha Selemani Matola ana bastola, analinganishwa na mwenye bunduki

KUNA watu ambao wanapoandika kitu, huwa nalazimika kuwasoma. Mmoja wao ni nyota wa zamani wa Argentina na Real Madrid, Jorge Valdano.

Yeye alikuwa sehemu ya nyota wa Argentina, pamoja na hayati Diego Maradona, waliotengeneza kikosi kilichotwaa Kombe la Soka la Dunia mwaka 1986.

Kama alivyokuwa ‘mtamu’ wakati akicheza, ndivyo hivyohivyo alivyo wakati anapoandika. Huwa haandiki maandishi tu, huandika tafakari.

Nakumbuka makala yake moja ya miaka 10iliyopita katika gazeti la Guardian la Uingereza. Alieleza kwamba mcheza muhimu kuliko wote katika timu ni yule anayeweza kutuliza mchezo. Alitumia neno la lugha ya Kiingereza “pause”.

Huyu ni mchezaji mwenye utulivu. Mwenye akili na ambaye huiona pasi au muvu ambayo haijatokea bado. Wakati huo, alitoa mfano wa aliyekuwa nyota wa Argentina kipindi hicho, Juan Ramon Riquelme.

Kuna wachezaji wachache wa namna. Katika Ligi Kuu ya Tanzania kwa sasa, mchezaji wa aina hiyo mahiri kuliko wote ni, Clatous Chota Chama wa timu ya Simba.

Ndiyo sababu, sikushangaa wakati Kocha Mkuu wa Yanga, Cedrick Kaze, aliposema Simba yenye Chama na Simba inayomkosa ni timu mbili tofauti.

Katika mechi ya Watani wa Jadi iliyochezwa Zanzibar wiki hii na Yanga kuibuka washindi, Simba ilimkosa Chama kuliko mchezaji mwingine yeyote.

Mchezo ulikuwa wa kasi na matumizi makubwa ya nguvu karibu muda wote. Mtu pekee ambaye angeweza kuigeuza na kuifanya iwe vingine ni mchezaji ambaye Valdano anatuambia anaweza kuweka “pause”. Simba haikuwa na mchezaji wa aina hiyo.

Kwa aina ile ya mchezo, faida ilikuwa kwa Yanga. Watoto hao wa Jangwani hawana mchezaji wa aina ya Chama ingawa Haruna Niyonzima kwenye ubora wake angeweza kufanya kazi hiyo.

Si kosa la Kocha Msaidizi wa Simba, Selemani Matola, kuwa Wekundu wa Msimbazi walizidiwa na kufungwa katika mechi Ile. Bila wachezaji wa kaliba ya Chama, asingeweza kufanya miujiza yoyote.

Tatizo la Matola ndilo tatizo la makocha wengi wa Kitanzania wanalokutana nalo hapa nchini.

Wanahukumiwa kwa vigezo ambavyo wageni hawahukumiwi navyo.

Washabiki wanataka Simba icheze kwa kiwango kilekile wakati karibu wachezaji wote wa kikosi cha kwanza hawakuwepo. Ni kama vile Matola kaenda na bastola kwenye vita na watu wanataka ifyatue risasi kama bunduki aina ya AK 47.

Makocha wa Kitanzania utakuta wanakaa kwenye nyumba za kupanga ‘Uswahilini’ lakini akija mgeni anatafutiwa hoteli au nyumba katika maeneo ya matajiri jijini Dar es Salaam.

Mgeni atapata mshahara mkubwa kuliko mzawa na hata bonasi zinaongezeka akiwa kocha mgeni. Makocha wa kizawa wanawekewa vikwazo vingi.

Mimi ni wa kwanza kukubali kwamba kuna tatizo kubwa la upungufu wa makocha wazawa wenye uwezo mkubwa wa kufundisha timu zetu kubwa.

Tatizo langu ni kwamba wakati mzawa anapopewa nafasi, anahukumiwa kwa vigezo tofauti kabisa na wageni.

Nimewahi kufanya kazi kwenye klabu zetu kubwa na ninajua kwa yakini kwamba wamewahi kuletwa walimu wageni ambao uwezo wao ulikuwa wa kawaida sana na pengine mdogo kulinganisha na baadhi ya makocha wazawa waliopo.

Watanzania tuna wajibu wa kuwasaidia na kuwawezesha kina Selemani Matola, Mecky Mexime, Shadrack Nsajigwa, Maka Malwisi, Zuberi Katwila na wengine kuwa wazuri zaidi ya walivyo sasa.

Tunatakiwa kuwatia moyo na kuwapa nafasi ya kuonyesha uwezo wao na kama watahitaji kushindanishwa au kukosolewa, basi wakosolewe kwa haki.

Kwenye soka tuna msemo mmoja maarufu; Fair Play. Tuwe fair kwa walimu wetu.


Imeandikwa na Ezekiel Kamwaga