Klopp anahitaji kubadili mfumo
Muktasari:
- Si siri kwamba Liverpool walikuwa wanamsaka beki wa Southampton, Virgil Van Dijk, katika dirisha kubwa la uhamisho mwaka huu. Lakini, uhamisho huu ulishindikana na hivyo Klopp hajakuwa na beki mwenye kiwango kikubwa katika kikosi chake cha kwanza hali ambayo imesababisha Liverpool kufungwa magoli mengi msimu huu.
KATIKA ulimwengu wa soka, kocha wa Liverpool, Jurgen Klopp ni kocha anayependwa na wafuasi wengi wa soka duniani. Si tu kutokana na kocha huyu kutaka timu zake zicheze mpira wa kushambulia bali anapendwa pia kwa jinsi anavyochangamka akiwa katika benchi la ufundi na jinsi anavyotoa majibu yanayochekesha akihojiwa na waandishi wa habari.
Hali hii imemfanya Klopp kuwa kocha anayependwa na waandishi wengi duniani na hivyo, ni mara chache sana kukoselewa. Naamini kwamba, Klopp ni kati ya makocha bora duniani na mafanikio aliyoyapata alipokuwa Borussia Dortmund akiwa na rasilimali ndogo yalinishangaza sana. Na katika klabu ya Liverpool naamini kwamba, klabu hiyo imepiga hatua chini ya uongozi wake. Msimu huu Liverpool wanashiriki katika mashindano makubwa kama Ligi ya Mabingwa Ulaya, lakini katika Ligi Kuu ya England timu hiyo haijapata mwanzo mzuri sana. Hivi sasa, Liverpool wameshika nafasi ya sita katika Ligi Kuu na wikiendi iliyopita walishinda mechi yao ya kwanza katika mechi nne katika Ligi Kuu ya England. Kwa mtazamo wangu ni wazi kwamba, safu ya ulinzi ya Liverpool haijakamilika na inahitaji kufanyiwa mabadiliko ili kwenda na kasi ya ushindani.
Si siri kwamba Liverpool walikuwa wanamsaka beki wa Southampton, Virgil Van Dijk, katika dirisha kubwa la uhamisho mwaka huu. Lakini, uhamisho huu ulishindikana na hivyo Klopp hajakuwa na beki mwenye kiwango kikubwa katika kikosi chake cha kwanza hali ambayo imesababisha Liverpool kufungwa magoli mengi msimu huu.
Klopp amesema mara kwa mara kwamba, shida ya timu yake ni kuwa hawana ngome imara na ni kweli kama Liverpool hawataweza kusajili beki mpya mpaka dirisha dogo la uhamisho litakapofunguliwa Januari, mwakani basi watakuwa na hali mbaya kwelikweli.
Klopp anataka Liverpool icheze mpira wa kushambulia katika kila mechi na anatumia mfumo wa 4-3-3. Lakini, katika mfumo huu viungo wa Liverpool wanashambulia sana na hawasaidii mabeki wa kati na hii ni sababu moja Liverpool imefungwa magoli mengi dhidi ya vilabu vyenye washambulaiji wazuri kama Manchester City na Tottenham.
Kwa mtazamo wangu Kloop anahitaji kubadilisha mfumo wake dhidi ya vilabu vikubwa na kuwalinda mabeki wa Liverpool zaidi kwa kucheza mfumo wa 4-2-3-1 au 4-4-2 na kutumia viungo wakabaji wawili badala ya mmoja tu.
Kama Kloop angebadilisha mfumo wake na kuwapa viungo wa Liverpool wajibu mkubwa zaidi wa kuwasaidia mabeki wa kati wa Liverpool kujihami, basi naamini, watapata matokeo mazuri zaidi.