Klabu 25 bora Ulaya zilizotumia pesa ndefu kujenga vikosi sasa
Muktasari:
- Hata hivyo, matumizi makubwa si dhamana ya mafanikio. Iwe ni katika Ligi Kuu England, La Liga au kwingineko, timu nyingi zimeonyesha zinaweza kutumia fedha nyingi kwa wachezaji ambao baadaye hawaleti matokeo yaliyotarajiwa.
LONDON, ENGLAND: INASHANGAZA kuona kiwango kikubwa cha fedha kinachotumika katika soka siku hizi. Kabla ya kuingia karne ya 21, ilikuwa vigumu kufikiria klabu kutumia zaidi ya mamia ya mamilioni katika usajili. Sasa, jambo hilo limekuwa la kawaida.
Hata hivyo, matumizi makubwa si dhamana ya mafanikio. Iwe ni katika Ligi Kuu England, La Liga au kwingineko, timu nyingi zimeonyesha zinaweza kutumia fedha nyingi kwa wachezaji ambao baadaye hawaleti matokeo yaliyotarajiwa.
Zaidi ya hayo, si lazima klabu zitumie kiasi kikubwa cha fedha ili kushinda mataji. Baadhi yao hunufaika na vipaji vya nyumbani vilivyokulia katika akademi zao na tayari vipo ndani ya kikosi. Mara nyingi, ni timu zisizo na akademi za viwango vya juu ndizo hulazimika kutumia zaidi katika soko la usajili ili kufidia pengo hilo.
Sasa UEFA imeorodhesha timu 25 zilizotumia fedha nyingi zaidi kuunda vikosi vyao, ikihesabu malipo yote hadi kufikia mwisho wa mwaka wa fedha wa 2025. Klabu 16 kati ya hizo zimeripoti kuvunja rekodi zao za kihistoria za matumizi, lakini kuna timu moja iliyojenga kikosi ghali zaidi katika historia ya soka.
Klabu za Ulaya zenye vikosi vya gharama kubwa zaidi (25–21)
Fiorentina ni miongoni mwa klabu zilizovunja rekodi yao ya matumizi kwa kikosi, huku gharama za mwaka zikiongezeka kwa asilimia 3 ikilinganishwa na matumizi ya jumla ya mwaka 2024.
Hata hivyo, jumla yao iko mbali sana na AS Monaco waliopo nafasi ya 24, ambao waliongeza Pauni 67 milioni zaidi ili kujenga kikosi chao cha sasa.
Baada ya klabu hiyo ya Ligue 1, zinafuata timu mbili za Italia, AS Roma na Atalanta ambazo zote ziko karibu kufikia kiwango cha Pauni 300 milioni kwa gharama ya vikosi vyao.
Hali ni tofauti kwa Nottingham Forest, ambao chini ya umiliki wa Evangelos Marinakis wameonyesha hawaogopi kutumia fedha nyingi inapohitajika.
Kwa kuwasajili wachezaji kama Omari Hutchinson, James McAtee na Igor Jesus katika dirisha la usajili la majira ya kiangazi 2025, inatarajiwa kuwa kiwango hicho kitaongezeka zaidi iwapo watabaki ndani ya Ligi Kuu.
25.Fiorentina — Pauni 210 milioni
24.AS Monaco — Pauni 287 milioni
23.AS Roma — Pauni 292 milioni
22.Atalanta — Pauni 298 milioni
21.Nottingham Forest — Pauni 328 milioni
Klabu za Ulaya zenye vikosi vya gharama kubwa zaidi (20–16)
Ingawa Crystal Palace hawachukuliwi kama timu inayotumia fedha nyingi Ligi Kuu England, The Eagles imekuingia katika orodha ya timu 20 bora kwa gharama ya kikosi.
Baada ya kutumia Pauni 331 milioni kwa kikosi chao cha sasa, hawako mbali sana na Inter Milan walioko nafasi ya 19, licha ya hadhi ya Nerazzurri kama moja ya timu bora duniani.
Timu zinazoshiriki mara kwa mara Ligi ya Mabingwa Ulaya kama Borussia Dortmund na Atlético Madrid zinafuata katika nafasi ya 18 na 17 mtawalia. Hata hivyo, inaweza kushangaza kuiona Barcelona ikiwa nafasi ya 16, kwa gharama ya jumla ya Pauni 405 milioni.
Vikwazo vya kifedha vimeikwamisha klabu hiyo katika soko la usajili hivi karibuni, licha ya historia yake ya kutumia fedha nyingi kuwasajili mastaa wakubwa. Pia ni muhimu kukumbuka kuwa wachezaji kama Lamine Yamal, Alejandro Balde na Pau Cubarsí walitokea katika akademi maarufu ya La Masia na kuwa sehemu muhimu ya kikosi cha kwanza.
Kwa kuzingatia mafanikio yao nchini Hispania na barani Ulaya, hii ni ishara tosha kuwa si lazima kila mara kutumia fedha nyingi sana ili kupata mafanikio.
20.Crystal Palace — Pauni 331 milioni
19.Inter Milan — Pauni 361 milioni
18.Borussia Dortmund — Pauni 387 milioni
17.Atlético Madrid — Pauni 396 milioni
16.Barcelona — Pauni 405 milioni
Klabu za Ulaya zenye vikosi vya gharama kubwa zaidi (15–11)
Kama ilivyo kwa Barcelona, AC Milan haijatumia fedha nyingi katika soko la usajili hivi karibuni kutokana na changamoto za kifedha, licha ya hadhi yao ya kihistoria kama moja ya miamba ya soka Ulaya.
Kwa sasa iko nyuma ya Bayer Leverkusen kwa jumla ya gharama ya kikosi, huku timu hiyo ya Bundesliga ikionyesha ongezeko kubwa zaidi la mwaka hadi mwaka (asilimia 44) katika ada za usajili zilizokusanywa kuliko timu yoyote katika orodha hii. Napoli hawako mbali sana wakiwa nafasi ya 13, lakini kuna pengo kubwa kuelekea timu zilizopo nafasi ya 12 na 11.
Bayern Munich wameonyesha utayari wa kutumia fedha nyingi hapo awali, jambo lililoangaziwa na dili la kuvunja rekodi la kumsajili Harry Kane mwaka 2023. Hata hivyo, licha ya uwekezaji huo mkubwa, bado wako nyuma ya Aston Villa kwa gharama ya kikosi.
Kikosi cha Unai Emery, katika jitihada zao za kuifikia Big Six ya jadi ya England, kimetumia fedha kuwasajili wachezaji kama Amadou Onana, Ian Maatsen na Ollie Watkins kwa miaka kadhaa na kwa sasa inaonekana uwekezaji huo unaanza kuzaa matunda. Aston Villa iko kwenye mbio za kufuzu Ligi ya Mabingwa Ulaya baada ya kukosa nafasi hiyo kwa tofauti ndogo sana katika msimu wa 2024/25.
15.AC Milan — Pauni 407 milioni
14.Bayer Leverkusen — Pauni 417milioni
13.Napoli — Pauni 451 milioni
12.Bayern Munich — Pauni 502 milioni
11.Aston Villa — Pauni 564 milioni
Klabu za Ulaya zenye vikosi vya gharama kubwa zaidi (10–6)
Tunapoingia kwenye nafasi 10 bora, tunaona wazi nguvu kubwa ya matumizi ya fedha waliyonayo timu za Ligi Kuu England ikilinganishwa na klabu nyingine katika ligi tano bora za Ulaya. Tangu PIF (Public Investment Fund) kuwa wamiliki matajiri zaidi ndani ya Ligi Kuu, Newcastle United imetumia fedha nyingi wakijaribu kuwa nguvu kubwa England.
Kwa kuwasajili wachezaji kama Bruno Guimarães, Anthony Elanga na Yoane Wissa miongoni mwa wengine, kikosi chao cha sasa kina thamani kubwa zaidi hata kuliko miamba wa Italia, Juventus.
Hata hivyo, licha ya utajiri wa Newcastle, bado kuna pengo kubwa kati yao na Tottenham Hotspur walioko nafasi ya nane, ambao gharama ya kikosi chao iliongezeka kwa asilimia 2 mwaka 2025 walipojaribu kurejea kwenye ushindani baada ya msimu mbaya wa Ligi Kuu.
Wakati huohuo, Paris Saint-Germain wamewahi kutumia mamia ya mamilioni ya pauni katika usajili huko nyuma, lakini hali hiyo si ya mara kwa mara siku hizi. Kwa kweli, gharama yao ya jumla ilishuka kwa asilimia 5 katika mwaka huohuo waliotwaa taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Hata hivyo, hali haikuwa hivyo kwa Liverpool. Baada ya kuvunja rekodi ya usajili nchini England mara mbili mwaka 2025 kwa kuwasajili Florian Wirtz na Alexander Isak, miamba hiyo ya Anfield iliweka rekodi ya kihistoria kwa gharama ya kikosi chao kufikia Pauni 842 milioni. Hata hivyo, kutokana na kushuka kwa kiwango cha timu msimu huu, huenda haikuwa lazima kutumia fedha nyingi kiasi hicho.
10.Juventus — Pauni 578milioni
9.Newcastle United — Pauni 583milioni
8.Tottenham Hotspur — Pauni 727milioni
7.PSG — Pauni 758milioni
6.Liverpool — Pauni 842milioni
Klabu za Ulaya zenye vikosi vya gharama kubwa zaidi (5–1)
Real Madrid ni miongoni mwa timu tano zilizovuka alama ya Euro 1 bilioni kwa thamani ya kikosi, lakini Los Blancos hawakuweka rekodi mpya ya klabu licha ya matumizi yao kuongezeka kwa asilimia 16. Wakiwa maarufu kwa enzi yao ya Galactico hapo awali, miamba hiyo La Liga ndio timu pekee nje ya England iliyoingia katika kiwango cha juu kabisa cha orodha hii.
Arsenal na Manchester United zilikuwa nguvu kubwa ya Ligi Kuu England mwanzoni mwa karne hii, lakini ushawishi wao umepingwa na klabu nyingine zilizojitokeza kuzidi ubabe wao. Ingawa zote mbili bado zinatumia fedha nyingi, matumizi yao ya jumla kwa wachezaji wa sasa yako mbali sana na timu mbili za juu.
Manchester City hawajaogopa kuonyesha nguvu zao za kifedha, wakiongoza kwa mishahara mikubwa Ligi Kuu England. Hata hivyo, licha ya kikosi cha Pep Guardiola kusajili wachezaji kama Omar Marmoush na Tijjani Reijnders mwaka 2025, bado hawajakikaribia kiwango cha Chelsea kwenye matumizi.
Chelsea wamekosolewa kwa kuwa na mbinu ya kusajili bila mpangilio maalum tangu Todd Boehly na Blue Co walipochukua umiliki wa klabu hiyo yenye maskani Stamford Bridge, wakijaribu kukijenga upya kikosi kwa kusajili vipaji chipukizi vyenye matumaini.
Hali hiyo imeifanya Chelsea kukusanya kikosi ghali zaidi katika historia ya soka chenye thamani ya Pauni 1.53 bilioni, lakini gharama hizo kubwa hazijaleta mafanikio ya ndani kama ilivyotarajiwa.
Kumekuwa na mabadiliko mengi ya wachezaji na kikosi cha kocha Liam Rosenior bado kinaonekana kuwa mbali katika mbio za ubingwa wa Ligi Kuu England. Huenda kunahitajika marekebisho katika sera yao ya usajili ili matumizi yao yawe na tija zaidi.
5.Real Madrid — Pauni 942milioni
4.Arsenal — Pauni 966milioni
3.Manchester United — Pauni 1.15bilioni
2.Manchester City — Pauni 1.39bilioni
1.Chelsea — Pauni 1.53bilioni