Kina Glazier ndani ya Manchester United

Sunday May 09 2021
old pic

WIKI iliyopita ilishuhudia mashabiki wa timu ya Machester United wakiandamana na kuvamia Uwanja wa Old Trafford siku ambayo timu hiyo ilipangwa kucheza na watani zao wa jadi, Liverpool katika mechi ya Ligi Kuu England.

Tukio hilo ni kubwa lililozua mijadala kila kona ya dunia kutokana na ukubwa wa mechi na timu hizo ambazo zina mashabiki kutoka kila kona ya dunia na kuweka historia katika ligi kuwa ndilo la kwanza kuwahi kutokea nchini humo lililosababisha mechi kuahirishwa kutokana na vurugu za mashabiki.

Mashabiki wa timu hiyo walionekana kubeba mabango na kuvaa fulana zilizoandikwa maneno yaliyosomeka kuwa wanataka umiliki wa timu hiyo urejeshwe kwao kutoka mikononi mwa familia ya Mmarekani na mfanyabiashara wa zamani ambaye kwa sasa ni marehemu, Malcom Glazer.

Mmarekani huyo alianza kununua hisa za timu hiyo kwa mara ya kwanza 2003 aliponunua asilimia 2.9 na kuendelea kununua hadi kufika asilimia 98, hivyo timu hiyo kuwa chini ya umiliki wake ambaye kwa sasa watoto sita ndio wamegawana hisa, huku wawili wakiwa wajumbe wa bodi ya uongozi.

Hivyo, kilio chao kimeonekana kuzungumzia eneo la umiliki wa timu ili wanachama wawe na uwezo wa kufanya uamuzi na pia wawe na uwezo wa kuisemea timu kama wanachama.

Ikumbukwe kuwa Manchester United ni timu iliyoanzishwa na wanachama na ni miongoni mwa timu kongwe duniani zilizoanzishwa miaka ya 1800 ikiwa imeanza 1878 na kuanza rasmi kutumia jina hilo 1902.

Advertisement

Timu hiyo ilisajiliwa kama kampuni na kuanza biashara mara ya kwanza 1892 kwa kuuza hisa za wanachama wakazi wa eneo hilo kwa Pauni moja kila hisa.

Hivyo hadi kufikia mwaka huu maana yake ni kuwa timu hiyo ina uzoefu sio tu katika soka, bali hata katika biashara ya soka kwa zaidi ya miaka 100, yaani zaidi ya karne moja katika soka na uchumi wake.

Kutokana na hali hiyo kuona mashabiki wanapiga kelele kuhusu jambo fulani ni ishara kwamba jambo hilo ni lazima litakuwa linawagusa moja kwa moja, na lazima watakuwa wanalihusisha na baadhi ya matukio ambayo hata kama wao hawakuwepo nyakati hizo, lakini wameyasoma au kusikia taarifa mbaya ambazo timu ilipitia kwa kuwa ni kongwe na imepita katika mabonde na milima hadi ilipo.

Kitendo cha familia ya Glazer kumiliki hisa asilimia hizo wala sio kitu kibaya, kwani kwa mujibu wa sheria, kanuni na miongozo ya EPL hakuna shida, lakini imeonekana umiliki wa timu hauendani na malengo na matarajio ya mashabiki, wapenzi na wanachama.

Ndio maana mashabiki walionekana kuzungumzia umiliki wa wa hisa wa asilimia 51 ili wanachama wawe na nguvu ya ziada katika uamuzi kwenye vikao vya bodi ya uongozi wa Manchester United. Wanachama wameonekana kuwa na wasiwasi kutokana na kiwango cha madeni ambayo kampuni inayomiliki timu hiyo inadaiwa ambacho ni zaidi ya Sh1.4 trilioni na wanatambuakuwa imekuwa ikipata mikopo kutoka benki za Marekani kutokana na thamani ya timu inayohusisha miundombinu kama viwanja na kuwa na uhakika wa kurejeshewa mikopo.

Hivyo, mikopo hiyo ambayo kibiashara ni kitu cha kawaida kwa kuwa ndio chanzo kikuu cha fedha imekuwa ikiwapa wasiwasi mashabiki na wapenzi wa timu hiyo kutokana na kutoingizwa moja kwa moja katika timu ya klabu ikiwemo eneo la wachezaji, badala yake kuwekezwa katika biashara nyingine ambazo kampuni hiyo imekuwa ikizifanya. Kwa mfano, hata 2005 ambapo Glazer alinunua hisa nyingi (zinazofikia milioni 800) kabla ya kifo chake 2014, kiasi cha fedha alizolipa zilikuwa Sh500 milioni ikiwa ni mkopo kutoka benki, hivyo timu kutwishwa deni kwa kuwa mmiliki ndiye aliyekopa na benki kumpa dhamana.

Kutokana na hali hiyo, matukio kama hayo siku zote huwa somo la kujifunza hasa kwa wale ambao bado hatujafikia hatua hiyo, kwani ikumbukwe kwamba moja kati ya vitu vilivyochangia mashabiki kuibuka pia ni hatua ya wamiliki wa timu kupitia faida ya biashara kusaini makubaliano ya kushiriki mashindano ya European Super League ambayo ingekuwa na manufaa makubwa kiuchumi kwa klabu, lakini imeonekana kuwa na madhara katika maendeleo ya mpira.

Hivyo, tunachotakiwa kuangalia na kujifunza ni kutambua kuwa madeni ni kitu cha kawaida katika biashara, lakini kwa klabu zinazoendeshwa na kampuni kibiashara kuwa nayo ni kitu cha kawaida, isipokuwa uhuru wa wanachama kufikisha ujumbe kwa uongozi wa timu na hisia za umiliki wao kuwepo ni vitu vinavyotakiwa kutunzwa na kuheshimiwa.

Kutokana na hali hiyo, biashara katika mchezo wa soka imekuwa ni suala la kawaida, lakini halipaswi kuondoa uhalisia wa mchezo wenyewe ambao upo kwa ajili ya kulinda utu, kuheshimu misingi na zaidi kuleta furaha kwa mashabiki wa mchezo huku ukiwaweka karibu wapenzi ili kufurahia maisha yao ya kila siku.

Hata hivyo, kwa Watanzania kuna jambo la kujifunza katika mkasa huu.

Imeandikwa na Ali Mayay

Advertisement