KIJIWE CHA SALIM SAID SALIM: Timoumi Yuko nyuma ya mafanikio ya Morocco kisoka

MIAKA ya 1970, moja kati ya nchi zilizokuwa bora kisoka duniani ni Morocco. Ilikuwa ndani ya mataifa bora 20 kabla ya kushuka na kufika nafasi ya 95, Septemba, 2010.

Baada ya kugundua hilo, kulifanyika mageuzi makubwa ya kuwaweka pembeni wachezaji wakongwe na kuingiza kizazi kipya, vijana. Mageuzi hayo yalileta mabadiliko chanya na kwa sasa taifa hilo la Afrika ya Kaskazini linashika nafasi ya 13 katika orodha ya viwango vya soka duniani vya Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa).

Ndiyo nchi inayoongoza Afrika kwenye orodha hiyo ambayo kinara ni Argentina, huku ikifuatiwa na Senegal na Tanzania ni ya 123, ikitanguliwa na nchi 30 za Bara la Afrika.

Hata hivyo, usilolijua, mafanikio ya Morocco iliyomaliza nafasi ya nne kwenye Fainali za Kombe la Dunia mwaka 2022, zilizofanyika Qatar, yako nyuma ya mmoja wa washauri wakubwa wa mipango kwenye soka la nchi hiyo na mchezaji wa zamani wa timu ya taifa hilo ambaye hatajwi sana.

Sio mwingine ni Mohammed Khalid Timoumi. Aling’ara kama kiungo mahiri wa Morocco miaka ya 1970 na 1980.

Akiwa na miaka 64 sasa, ni mshauri wa klabu ya AS FAR iliyo chini ya jeshi la nchi hiyo na inashiriki Ligi Kuu ya Botola, kazi aliyopewa miaka miwili iliyopita na Mfalme Mohammed ambaye ni mpenzi mkubwa wa soka na anatoa fedha nyingi kwa timu ya taifa ya nchi hiyo.

Timoumi aliikataa kazi hiyo kwa vile alitaka kupumzika baada ya matibabu ya upasuaji wa tumbo Ufaransa, lakini baada ya mfalme kumwomba kuisaidia nchi yake alikubali.

Kiungo huyu maarufu wa Morocco  amepata mafanikio makubwa, ikiwa ni pamoja na kuchaguliwa kwa kura nyingi kama mchezaji bora wa soka wa Afrika mwaka 1985.

Mchezaji pekee wa Morocco aliyemtangulia kwa kupewa heshima hiyo ni Ahmed Faras (1975) na kufuatiwa na Badou Zaki (1986) na Mustapha Hadji (1998).

Timoumi ambaye ni mrefu na mwenye mwili mkubwa, alilisakata soka kwa uhakika na kujiamini kwa miaka 20.

Ni mchezaji anayekumbukwa kwa namna alivyozichezesha mchakamchaka timu za Ujerumani Magharibi, Ureno, England na Poland na kuiwezesha Morocco kuingia mzunguko wa pili wa fainali za Kombe la Dunia za 1986 zilizofanyika Mexico.

Morocco ilifungwa 1-0 na Ujerumani Magharibi katika mchezo wa kwanza, ikaichapa Ureno 3-1 na ikatoka sare bila ya kufungana na England, hata hivyo, mchezo wa mwisho ilitoka suluhu dhidi ya Poland na kusonga mbele.

Matokeo haya yaliandika ukurasa mpya wa historia kwa kuwa nchi ya kwanza ya Afrika kuvuka mzunguko wa kwanza wa fainali za Kombe la Dunia.

Akiwa nahodha wa Morocco, Timoumi atakumbukwa na Wareno kwani ndiye aliyetoa pasi mbili za mabao yaliyofungwa na Abderrazik Khairi dhidi ya Ureno wakiichapa mabao 3-1 na kufanya ushindi huo kuwa moja ya matukio ya kihistoria katika soka.

Nyota wa zamani wa Ureno wanasema hawataisahau siku ile waliyoipa jina la ‘Siku Nyeusi’ kwani baada ya mchezo huo magazeti ya Ureno yalijitokeza na vichwa vya habari vya ajabu kama: ‘Huwezi kuamini, Ureno ipo kwenye msiba’ na ‘Masikini Ureno’.

Akizungumzia fainali hizo hivi karibuni, Timoumi alisema; “Tulipokuwa Mexico tulikuwa tumebeba mizigo mitatu vichwani na kila mmoja ulikuwa mzito kuliko mwengine. Kwanza ni kulinda heshima yetu kama wachezaji, pili kuiwakilisha vyema Morocco na tatu kuonyesha wakati umepita wa kuidharau Afrika katika soka. Nashurukuru tulifanikiwa kuyafanya yote hayo.”

Timoumi ambaye alizaliwa katika mji wa Rabat, Morocco, Januari 15, 1960 baada ya kuchezea klabu za mtaani na shule, alijiunga na FAR inayopatikana katika mji wa Rabat na kukaa nayo kwa zaidi ya miaka 10, huku akiiwezesha kutwaa ubingwa wa Morocco mara kadhaa. Pia alikuwemo katika kikosi cha timu ya taifa iliyoshiriki Michezo ya Olimpiki ya 1984.

Alishirikiana vizuri na washambuliaji Abdelkarim ‘Fery’ Krimau na Bourdeballa na kipa Badou Zaki ambaye alichaguliwa na Fifa kuwa kipa bora wa Afrika wa karne iliyopita.

Pia alizichezea klabu za Ulaya, ikiwamo Lokeren ya Ubelgiji na Murcia ya Hispania.

Mwaka 2006, Shirikisho la Soka la Afrika (Caf) lilimchagua kuwa mmoja wa wachezaji bora wa bara hili katika kipindi cha miaka 50 iliyopita.

Baada ya Morocco kushindwa kuingia fainali za Kombe la Dunia zilizofanyika Afrika Kusini 2010 na Kombe la Mataifa ya Afrika kule Angola, Timoumi alisema inasikitisha kuona kiwango cha soka cha Morocco kimeshuka.

“Ni aibu na fedheha. Mataifa mengi ya Afrika yalikuwa yanatuogopa, lakini leo sisi ndio waoga,” aliongeza.

Kutokana na hali hii, aliamua kuwafundisha vijana chipukizi wa kuanzia miaka 11 hadi 15 na kuamini pakifanywa juhudi za kutosha hali itarudi kama zamani, lakini kinachohitajika ni mashirikiano na kujituma na sio kulaumiana. Ndiyo maana leo Morocco imepanda kisoka.

Alisema na kuitolea mfano klabu yake ya FAR ilifanikiwa kutokana na kulea vijana waliopandishwa, anaamini kwa kuwapa mafunzo vijana na mechi za kirafiki wangefanikiwa.

Timoumi hatasahaulika kwao Morocco kwa mchango wake mkubwa na namna alivyoshirikiana na wenzake kuipa Afrika sura kisoka baada ya kuviangusha vigogo au kutoka navyo sare kwenye Fainali za Kombe la Dunia 1986, Mexico.

Sasa wachezaji aliowalea wameanza kuwa na umri mkubwa. Suala linalosubiriwa kupatiwa jawabu ni je, chipukizi wanaonolewa sasa wataweza kuwa kivuli cha wenzao waliotangulia?

Muda ndio utakaotoa jawabu.