KIJIWE CHA SALIM SAID SALIM: Negrete utamtaja tu Kombe la Dunia

WAPO wahenga waliosema “kila msitu na komba wake” na wengine wakaja na kauli ya “kila zama na kitabu chake”.

Falsafa hii yenye tafsiri iliyojificha katika hii misemo pia ipo katika michezo ikiwa ni pamoja na kandanda ambao umeshuhudia ukweli wa maelezo haya.

Kwa muhtasari, medani ya kandanda imeshuhudia mengi katika historia ndefu ya mchezo huu kwenye kila pembe ya dunia na yapo mambo ambayo hayasahauliki na ni sehemu ya historia.


Ukizungumzia Kombe la Dunia yapo yanayosimuliwa kila wakati kwa uzuri au ubaya. Hii ni pamoja na mabao mazuri katika michezo ya mtoano na fainali za mashindano hayo yaliyoanzia Uruguay 1930.

Mmoja wa wachezaji ambao bao alilofunga linahesabiwa kati ya mabao 10 bora ya muda wote ni aliyekuwa kiungo wa kutegemewa wa Mexico, Manuel Negrete katika fainali za 1986 zilizofanyika Mexico.

Negrete alipelekewa mpira wa juu nje kidogo ya eneo la hatari katika dakika ya 35 ya mchezo. Aliuzuia kwa ustadi kifuani, akauteremsha kwenye mapaja na kuusubiri udunde na ulipokuja juu kama futi moja na nusu kutoka ardhini alimpasia mshambuliaji mwenzake Javier Aguirre.


Kisha, Aguirre akamrudishia Negrete mpira ukiwa kimo cha magoti na Negrete aliyekuwa akikimbia kama swala alijipinda na kufyatua mkwaju mkali hadi kwenye pembe ya chini ya mwamba wa kushoto wa goli.

Katika tukio hilo kipa Borislav Mikhailov wa Bulgaria aliduwaa aliposikia umati uliofurika uwanjani ukishangilia na alionekana kama hakujua kilichotokea.

Watazamaji walimcheka na kupiga kelele zilizomtaka Mikhailov kugeuka nyuma auone mpira uliotulia kimiani.

Mexico iliibuka mshindi kwa mabao 2-0 katika mchezo huo na kusonga mbele hadi robo fainali, kama ilivyotokea katika fainali za 1970 ilipokuwa mwenyeji wa fainali za kombe hilo.

Watazamaji hawakushangaa kuona ulipomalizika mchezo yule kipa wa Bulgaria alimfuata Negrete na kumpa mkono wa pongezi kwa kazi nzuri aliyoifanya ya kupachika bao la kihistoria.


Namna Negrete alivyocheza kwa mbwembwe na kujiamini, kama vile hakuwajali wapinzani ambao aliona uwezo wao wa kumbana ni mdogo iliwavutia pia watazamaji nchini kwao Mexico, nchi za Amerika Kusini na Ulaya.

Baadhi ya makocha wa zama zile walipowakemea wachezaji walioonyesha dharau walimtumia Negrete kama mfano usiofaa kuigwa kwa kusema: “Acha kuwa Negrete wa pili...unaweza kutuletea balaa”.

Siku moja Ngerete alipoulizwa na waandishi wa habari kwa nini alijiamini kupita kiasi alisema: “Ninapokuwa uwanjani huhisi kama dereva na wapinzani, kama abiria wangu wanapaswa kwenda nilikotaka kwa vile mimi ndiye niliyeshika usukani.”

Manuel Negrete alizaliwa katika mji wa Altamirano, Mexico, Machi 11, 1950. Tofauti na wachezaji wengi mashuhuri alitumia muda mwingi akiwa na klabu ndogo  akicheza soka ya kulipwa 1980 akiwa na miaka 30 akiwa na Klabu ya Universidad Nacional ya Mexico, ambayo pia inajulikana kwa jina la Puma.

Wakati alipojiunga na UNAM Pumas akiwa na umri mkubwa aliulizwa kwa nini alikawia kuamua kucheza soka la kulipwa na jibu lake lilikuwa kali kama mashuti yake ya kuelekea golini.

Alisema: “Hata nje ya uwanja wa kandanda wapo wanaofunga ndoa mapema na wengine wanakawia hadi wafikapo miaka 50 na zaidi. Uamuzi ni mapenzi ya mtu na sio vizuri kumuingilia katika mapenzi yake.”

Alipoambiwa mchezo wa kandanda unahitaji nguvu za misuli ambazo huwa katika hali nzuri mtu anapokuwa kijana alisema: “Kila kitu hakiwi mpaka ufike wakati wake. Hata katika uzazi wapo wanaozaliwa baada ya miezi saba, tisa au 10.”

Negrete aliichezea Puma kwa miaka 16 akaenda Ureno kujiunga na Sporting Lisbon na baadaye Hispania ambako aliichezea Atlante F.C, Toros Neza CF na Acapulco.

Wakati akiwa Mexico na kuamua kwenda Ureno aliichezea timu ya taifa ya nchi hiyo kwa miaka 19 tangu 1981 hadi 1990 alipostaafu akiwa na miaka 40. Aliifungia nchi yake mabao 57.

Baada ya kustaafu Negrete alizifundisha timu za vijana za Mexico, lakini zaidi za watoto za klabu ya UNAM Pumas. Kuanzia wakati huo hadi sasa amekuwa akiifundisha klabu ya Leon ambayo inacheza Ligi Kuu nchini humo.

Awali, nyota huyo aliajiriwa kuwa kocha msaidizi wa timu hiyo na kuchaguliwa kocha mkuu kufuatia kufukuzwa kazi kwa Mario Alberto Garcia.

Alipotimuliwa Garcia na yeye kuchukua nafasi yake, waandishi wa habari walimzonga na kumuuliza alihisi vipi kushika nafasi hiyo ukitilia maanani yeye na Garcia walikuwa marafiki.

“Acheni kuchanganya mambo. Nani kakwambieni kuichukua nafasi ya Garcia ni kuvunja urafiki wetu. Kumbukeni nimefundisha kwa siku nyingi na Garcia na sasa mimi ndio kocha mkuu na Garcia hayupo. Nilichochukua ni nafasi ya ajira aliyokuwa nayo Garcia na sio mke au mpenzi wake,” alisema. Manuel Negerete hatasahaulika kila yanapozungumzwa mashindano ya Kombe la Dunia na historia yake, habari za soka nchini Mexico na za klabu za soka za Ulaya.


Atakumbukwa sio kwa mchezo wake mzuri tu, bali pia kwa ustadi wa kuunganisha vizuri maneno na kutoa kauli zenye vijembe kama mashuti yake makali aliyokuwa akiyaelekeza golini alipokuwa akilisakata kabumbu.

Pamoja na hayo, nyota huyo anakumbukwa na nchi yake kama mmoja wa malenjedari walioiletea heshima na kuifanya itamkwe mara kwa ra enzi zao.