Kihimbwa mkali wa Mtibwa Sugar anayeteswa na kifungo kilichomkuta Polisi

Friday January 14 2022
Kihimbw PIC
By Saddam Sadick

MBEYA. LICHA ya kuanza msimu vibaya Mtibwa Sugar, lakini winga wa timu hiyo, Salum Kihimbwa amekuwa na kiwango bora akitumika kama ëpundaí kuipa heshima timu hiyo katika Ligi Kuu Bara.

Nyota huyo anaitumikia timu hiyo kwa msimu wa sita sasa ambapo amekuwa na ubora kikosini na ndiye kinara wa mabao ndani ya timu hadi sasa msimu huu akifunga mawili na asisti mbili.

Kihimbwa ambaye aliwahi kuzichezea Mkamba Rangers na Polisi Moro, pia amezitumikia timu ya Taifa ya vijana (U23) na Taifa Stars.

Winga huyo mshambuliaji alianza soka la ushindani 2010 akiwa kidato cha tatu katika Sekondari ya Nyandeo mkoani Morogoro alipokuwa akiichezea Mkamba Rangers iliyokuwa Ligi Daraja la Kwanza. Moja ya rekodi anayotamba nayo ni kudumu katika kikosi cha Mtibwa Sugar kwa muda mrefu, uhakika wa namba na kuwa miongoni mwa wafungaji wa muda wote ndani ya timu hiyo.

Kihimbwa anasema amedumu muda mrefu Mtibwa Sugar kutokana na mazingira mazuri anayoishi na ndio sababu imemfanya kutokuwa na papara za kusaka changamoto kwingine.

Anasema viongozi na mashabiki wamempa thamani na kutambua mchango wake jambo ambalo ameona ni faraja kwake kuendelea kuhudumu kikosini hapo.

Advertisement

“Kama ni maslahi hakuna tatizo, watu wanatambua na kuheshimu mchango wangu, unaweza kwenda kwingine ukakuta siasa zimetawala, hivyo hapa sijutii kitu,” anasema Kihimbwa.

Anaongeza kuwa sababu za kuwa na uhakika wa namba kwa kila kocha anayetua kikosini ni kutokana na juhudi binafsi alizonazo.

Anasema mpira ni mchezo wa wazi na kwamba ufanisi wa mchezaji kuwa bora huanzia mazoezini, hivyo kutokana na kile anachoonesha huwaondolea wasiwasi makocha na kumpa namba.

“Mpira huwezi kudanganya unajua kucheza kumbe hujui, kila mtu atakuona, unachofanya mazoezini, kocha anaelewa ndio maana wameniamini muda wote,” anasema winga huyo.

Nyota huyo anaongeza kuwa pamoja na kazi yake lakini hawezi kuusahau mwaka 2015 baada ya kufungiwa mechi 10 na kupigwa faini ya Sh2 milioni wakati akiitumikia Polisi Moro.

Anasema mwaka huo ulikuwa mgumu kwake wakati akiiongoza timu hiyo dhidi ya JKT Mlale, mmoja wa wachezaji wa timu pinzani alimshika sehemu za mwili na kujikuta akimcharukia na mwamuzi kumuonyesha kadi nyekundu.

“Siwezi kusahau 2015 mmoja wa wachezaji wa JKT Mlale katika mechi za mwisho kuwania kupanda Ligi Kuu alinigusa sehemu moja ya mwili nikamrukia, baadaye adhabu ikaja ya kunifungia mechi 10 na faini ya Sh2 milioni,” anasema Kihimbwa.

Hata hivyo, anawatoa wasiwasi wadau na mashabiki wa Mtibwa Sugar kuwa licha ya kuanza msimu kinyonge, lakini watabadilika na kumaliza nafasi nzuri huku akitarajia kufunga mabao mengi kuliko msimu uliopita.

“Tumeanza vibaya, lakini kadri tunavyokwenda kuna mabadiliko, naamini hadi kumaliza ligi tutakuwa nafasi nzuri, pia nitafunga zaidi ya mabao matano niliyofunga msimu uliopita,” anasema Kihimbwa.

Naye kocha msaidizi wa timu hiyo, Awadh Juma anasema Kihimbwa amefanikiwa kwake kutokana na utayari wake, kuelewa anachoelekezwa na kila kocha, lakini pia ana nidhamu ya kazi.

“Anawajibika, anajituma, ana uwezo na kipaji, lakini nidhamu ya kazi na mwepesi kunasa anachoelekezwa na kufanya kinachotakiwa na kuleta matokeo chanya,” anasema Juma.

Advertisement