Kigonya, msomi aliyesaliti vyeti vyake

KATIKA usajili wa dirisha dogo nchini kila timu ilifanya maboresho ya kikosi, huku Azam FC - matajiri wa Ligi Kuu Bara nao wakiongeza baadhi ya wachezaji akiwemo kipa Mathias Kigonya kutoka Zambia. Kigonya alikuwa akiichezea timu ya Forest Rangers inayoshiriki Ligi Kuu nchini humo.

Mwanaspoti lilifanya mahojiano na kipa huyo ambaye alieleza mambo mbalimbali juu ya soka hadi hapo alipotua Azam.


ALIPOANZIA

Kigonya anasema alianza kucheza soka kwenye akademi mbalimbali huko Uganda kama Jogoo Stars kabla ya kutua timu ya vijana ya SC Villa na wakati huo alikuwa akisoma, hivyo muda mwingi hakujihusisha kucheza soka zaidi kwani alipendelea kusoma. Anasema alicheza kwa mafanikio zaidi timu za vijana za SC Villa hadi alipandishwa kikosi cha wakubwa na hapo ndio Soana ilimuona.

“Sikucheza mechi hata saba, Soana walinihitaji na kusema licha ya umri mdogo niliokuwa nao walikuwa na imani ningewasaidia, hivyo walinisajili na nilianza kucheza hapo,” anasema na kuongeza baada ya kujiunga na Soana mwaka 2013 ndipo maisha yake mapya ya soka yakaanza.

Alidumu kwa msimu mmoja tu kisha alitua Bright Stars FC alikocheza misimu miwili, na akiwa hapo 2016 aliitwa timu ya taifa ya Uganda iliyoshiriki michuano ya Chan 2016 na kuishia hatua ya makundi.

Baada ya michuano hiyo iliyofanyika Januari 16 hadi Februari 7 nchini Rwanda, mwisho wa msimu alinunuliwa na Sofapaka ya Kenya.


USHIKAJI NA BIGIRIMANA

Taarifa zilizozagaa baada ya ujio wake nchini ni kwamba staa wa zamani wa Yanga, Issa Bigirimana alihusika kufanikisha mchakato huo, na Kigonya anafafanua juu ya hilo.

“Kabla sijaja kweli niliongea naye kumuomba ushauri kwa sababu amecheza na anafahamu mazingira, aliniambia Tanzania ni nchi nzuri na kuna ligi nzuri, lakini kama nahitaji kufanikiwa lazima niweke juhudi. Suala la kusema yeye ndio alinileta hapa sio kweli, Azam walikuwa wakinifatilia kwa muda mrefu.”


PENALTI YA CHAMA

Akizungumzia penalti ya kiungo wa Simba, Clatous Chama aliyoipangua katika mchezo wa Ligi Kuu kati ya Azam na Simba,, Kigonya anasema: “Huwezi kujua moja kwa moja kwamba mtu anapiga wapi, lakini unachotakiwa kufanya ni kutotoa macho yako kwenye miguu yake ili kukisia upande ambao anaweza kupiga, kwa hiyo aliingia kwenye hesabu zangu, ingawa ile sio jambo la ajabu kwani nimewahi kucheza penalti nyingi katika sehemu nilizowahi kucheza, ingawa siwezi kusema moja kwa moja ni ngapi.”


TOFAUTI YAKE NA MAKIPA BONGO

Anasema hana muda mrefu Tanzania hivyo hawezi kuwazungumzia makipa aliowakuta, lakini zaidi anajikita kwenye kujielezea binafsi. “Staili yangu ipo tofauti, huwa siwezi kukaa golini muda wote. Napenda kuchezea mpira, sijui kama kuna kipa mwingine mwenye staili hiyo, kama atakuwepo tutakuwa tunafanana na kama hayupo hiyo ndio staili yangu.”

Kipa huyu ana muda haijaitwa timu ya taifa ya Uganda ‘Uganda the Cranes, na hapa anasema: “Sijaitwa muda mrefu, lakini hilo halinipi shaka kwa sababu kwenye soka kila jambo lina wakati wake, hivyo muda ukifika wale wanaopata nafasi ya kucheza sasa hivi watanipisha na nitacheza tu, zaidi natakiwa kujituma.”


SIMBA NA YANGA VIPI?

Anaanza kwa kusema dili lake lilikuwa na tofauti kidogo kwa sababu hakukuwa na watu wengi wanajua zaidi ya viongozi wa Azam.

“Walikuja kufahamu mwishoni kabisa na wakati huo nilishamalizana na Azam, hivyo hawakuwa na jinsi na niseme nashukuru Mungu kwa sababu sikupata watu wa kunisumbua kutoka timu nyingine, ilikuwa ni mimi na mabosi wa Azam pekee.

“Nimewahi kucheza timu nyingi zenye presha, hivyo baada ya mechi ya Simba pongezi zilikuwa nyingi lakini hiyo hainifanya nibweteke,” anasema na kuongeza kwamba licha ya watu kusema alicheza vizuri mechi hiyo, anaona kilikuwa ni kiwango cha kawaida ambacho mechi nyingi amewahi kucheza hivyo.


TUKIO LA FURAHA KWENYE SOKA

“Nakumbuka wakati nipo shule, tulikwenda kucheza michuano ya Copa Coca Cola 2010, timu yetu ilikuwa na wachezaji 11 pekee na kipa nilikuwa mimi tu, kwenye siku ya mwisho ya michuano nilichukua tuzo tatu - ya kwanza ilikuwa kipa bora wa michuano, beki bora na mchezaji bora. Nafikiri hili ni jambo lililonifurahisha zaidi kwani nilicheza namba tofautitofauti hasa pale kulipokuwa na pengo mahali,” anasema.

Kigonya anasema kuwa ana uwezo wa kucheza zaidi ya maeneo matatu awapo uwanjani - kuanzia beki, winga na straika ndio maana haimpi shida sana kwenye kudaka kwani huisoma akili ya straika kabla hajafanya maamuzi.


TUKIO LA HUZUNI

Hili lilijiri msimu uliopita wakati anaitumikia Forest Rangers ya Zambia kwenye mechi ya mwisho ya msimu dhidi ya Zanaco walihitaji kupata bao moja ili kuchukua ubingwa mbele ya Nkana, lakini mechi iliisha kwa suluhu.

“Ndio nilikuwa naingia kwenye timu, jambo hili lilinihuzunisha sana kwa sababu ilikuwa ni nafasi ya dhahabu lakini tulifeli,” anasema.

PESA YA KWANZA KWENYE SOKA

Ukimuuliza kuhusu fedha alizopata katika soka kwa mara ya kwanza, kipa huyo anacheka kisha anasema kwanza hakuwa anajali juu ya pesa kwani, hakuwa na ndoto za kuja kuwa mchezaji mkubwa. “Ilikuwa wakati napandishwa kikosi cha kwanza cha Villa mwaka 2010. Nakumbuka nilipewa Dola 500, wakati huo ilikuwa nyingi na kwa kweli sikujua hata nitumie nini zaidi ya kwenda kumpa mama yangu,” Kigonya anasema na kuongeza kwamba baada ya kumpa kiasi hicho mama yake alimpa baraka ambazo hadi sasa anaamini ndizo zinamfanya kuwa kwenye kiwango bora.


TOFAUTI YA TANZANIA NA ZAMBIA

“Zambia ni nchi yenye joto sana, kuliko hata huku lakini masuala ya kiufundi bado sijagundua kwa sababu ndio kwanza nimefika hivyo sijasoma sana,” anasema.


AMEOA, JE AMECHEPUKA?

Anaanza kwa kusema hajawahi kupata usumbufu wowote kwenye mitandao ya kijamii baada ya kutua Tanzania na kucheza mechi ya Simba.

“Siwezi kusema sijawahi ama nimewahi kuchepuka kwa sababu binadamu wanapitia mengi, lakini tangu nimeoa sijawahi kufanya jambo kama hilo na naipenda sana familia yangu, huko nyuma kwenye maisha ya ujana mambo kama haya yanaweza kutokea.”

Kuhusu soka haamini kama Azam ni kituo chake cha mwisho, lakini kwa sasa anapambana kuhakikisha timu inafanya vizuri. “Nitatoa kila nilichonacho kuhakikisha timu inafanya vizuri, ni timu inayonipa tamaa ya kupambana kila siku, hivyo kwa kushirikiana na wachezaji wenzangu nitajaribu kupambana kuhakikisha tunafikia malengo. Kucheza nje ya Afrika ni ndoto ya kila mchezaji hivyo siwezi kusema haiwezekani,”


KUUMIZWA KWENYE MAHUSIANO

Anacheka kisha anasema: “Kiukweli sijawahi kukutana na jambo kama hilo kwa sababu nimekuwa na mwanamke huyu niliyemuoa kwa muda mrefu.”

Awapo uwanjani huwa hapendi kuona mchezaji mwenzake amefanya makosa, halafu akaja mchezaji mwingine wa timu yao akaanza kumlaumu badala ya kusahihisha kwanza.

“Kitendo cha kumfokea mchezaji mwenzako aliyefanya makosa ni kutengeneza kosa lingine, kwanza unampunguzia hali ya kujiamini, kama amekosea sahihisha kwanza makosa kisha umuelekeze sio kumlaumu.”


DERBY YAKE YA KWANZA

Anasema ilikuwa ni dhidi ya Gor Mahia wakati huo alikuwa akiitumikia Sofa Paka ya Kenya na ndio ilikuwa kwenye siku zake za mwanzo. “Mungu alisaidia kwamba iliisha kwa suluhu ya bila kufungana na ilichangia kunijengea hali ya kujiamini, na kuona kwamba naweza kufanya kitu kikubwa zaidi kwenye siku zijazo na hilo nililifanikisha.”


KUMBE JAMAA NI MSOMI

Kabonya ni mmoja kati ya wachezaji waliosoma na kucheza mpira. Amehitimu shahada ya uongozi Chuo Kikuu cha Kampala nchini Uganda na anasema kama isingekuwa soka basi angefanya kazi hiyo.