KICHUYA: Ile kona bao Yanga wala Sikudhamiria
Muktasari:
- Ipo hivi; Wengi wanafahamu kuwa Kichuya ni jina la ukoo wa mchezaji Shiza, lakini unaambiwa kuwa hilo ni jina la utani na lilitokana na baba mzazi wa mchezaji huyo kipindi hicho anacheza soka kama anavyothibitisha winga huyo.
KICHUYA ni jina kubwa kwenye anga ya michezo nchini kutokana na winga Shiza Ramadhan ambaye kwasasa anakipiga JKT Tanzania kutambulika zaidi kwa jina hilo, lakini unaambiwa jina hilo ni la utani.
Ipo hivi; Wengi wanafahamu kuwa Kichuya ni jina la ukoo wa mchezaji Shiza, lakini unaambiwa kuwa hilo ni jina la utani na lilitokana na baba mzazi wa mchezaji huyo kipindi hicho anacheza soka kama anavyothibitisha winga huyo.
“Nilipata historia ya jina hilo na kuamua kumuuliza baba ambaye alinijibu kuwa siyo jina la ukoo na ni watu wengi hawafahamu,” anasema.
“Jina la ukoo wetu ni Yahya, nikamuuliza baba ilikuwaje sasa Kichuya, ndipo aliponiambia kuwa kipindi anacheza soka akitumika katika nafasi ya kiungo mshambuliaji, ndio alipachikwa jina hilo.”
Shiza anasema licha ya baba yake kutokucheza soka la ushindani, lakini kwa mujibu wa masimulizi aliyopata, alikuwa bora sana zaidi yake na anabainisha kuwa wakati yeye alivyokuwa akicheza soka wakawa wanamuita ni mtoto wa Kichuya na ndipo jina hilo likakua kwake pia.
“Hata nilipokuwa naanza shule kwenye vyeti vyangu nilikuwa naandika Shiza Ramadhan Kichuya kwasababu nilikuwa sifahamu, baadaye nilipoanza kubadili kwa kuandika Yahya, tayari jina la Kichuya lilishakua na watu wanalifahamu hilo.”
Anasema hadi sasa bado hajafahamu kwanini baba yake aliitwa Kichuya kwasababu alipomuuliza kwanini aliitwa hivyo hakumpa ufafanuzi wa chanzo.
Mwanaspoti lilivyoendelea kufanya mazungumzo na winga huyo ambaye alifunguka mambo mbalimbali, alitaja tukio jingine kubwa alilowahi kufanyiwa kwenye maisha yake ya mpira lililomfanya aingie kwenye nyumba ya watu bila kugonga hodi.
KUVAMIWA NA MASHABIKI
Wakati inafahamika soka ni mchezo wa burudani, unaambiwa kwa mashabiki ambao hawana uvumilivu na wanaumizwa na matokeo hilo hawaliamini kama anavyofunguka Kichuya.
“Hili tukio sitakaa nikalisahau, nikiwa Mtibwa Sugar ndiyo kwanza nimepandishwa kutoka timu ya vijana na kocha akiwa Mecky Mexime kipindi hicho, nilikimbizwa Turiani - Manungu,” anasema.
“Nakumbuka tulitoka kucheza mechi ya ligi. Nilikuwa ndiyo kwanza nimetoka kupandishwa katika kikosi cha wakubwa, kukawa na mechi nyingine ya mtaani na viongozi wa Mtibwa Sugar walikuwa na timu yao, mchezo ulikuwa wa nusu fainali, hivyo wakaja kuchukua wachezaji wa Mtibwa Sugar na mimi nikiwamo.”
Kichuya anasema aliingia kipindi cha pili, timu ya mabosi wake ilikuwa tayari imefungwa bao moja na wapinzani wao walikuwa kina Hussein Javu, mchezo ulichezwa kwenye Uwanja wa Chamazi upo Turiani.
“Niliingia kipindi cha pili mimi na Ismail Mhesa na Jafar Kibaya, tulifanikiwa kuchomoa bao la kwanza dakika za jioni, ‘niliondoka na kijiji’ nikatoa pasi mwenzangu akaunga kwa kichwa tukapata bao la pili,” anasema.
“Sina hili wala lile nikajua hakuna kitakachotokea, nakumbuka nguo zangu nilivulia upande mwingine na mara baada ya mchezo kuisha nilikuwa ng’ambo tofauti na zilipo nguo, wahuni walipotoka sikujua kama wananifuata nikajua wanashangilia.”
Kichuya anasema alisikia sauti kutoka mbali inamwambia kimbia wanakufuata wewe hao ndipo alipoanza kukimbia akiwa na bukta na njumu mguuni na kuingia kwenye nyumba ya watu bila hodi na nyuma akifuatwa mbio.
“Kwenye kundi la watu waliokuwa wananikimbiza kulikuwa na mashabiki wa timu niliyokuwa naichezea, nikasikia ‘simama’, nikajiuliza sasa nisimame vipi wakati watu wana hasira na mimi? Hata angekuwa kaka yangu nisingefanya hivyo. Nilipozama ndani kwa watu nilitokea mlango wa nyuma nikaruka ukuta breki ya kwanza kambini Turiani. Hilo ndiyo tukio sitakaa nikasau kwenye soka,” anasema Kichuya kuhusu mashabiki waliojawa na hasira naye baada ya kuizamisha timu yao kwa kiwango chake alichoonyesha alipoingia ‘sub’.
SIO BAO LAKE BORA
Mashabiki wa soka nchini daima watalikumbuka bao la Kichuya alilofunga katika dakika za jioni dhidi ya Yanga wakati akiitumikia Simba.
Siku hiyo katika Dabi ya Kariakoo, Yanga ilikuwa ikiongoza kwa bao 1-0 lililofungwa kiutata na Hamis Tambwe ambaye alionekana akiumiliki mpira kwa mkono kabla ya kwenda kuweka bao la kuongoza. Na wakati mashabiki wakidhani mechi ingeisha kwa ushindi wa bao hilo moja, Simba ilipata kona katika dakika 87. Kichuya akaenda kupiga kona. Alichonga kona moja matata sana ya kiwango cha dunia. Mpira alioupiga ulikwenda moja kwa moja wavuni na kuandika historia ya aina yake huku wasanii wa Bongofleva wakimuimba katika nyimbo kama ‘Kichuya kona’.
Licha ya bao lake hilo kutajwa kuwa ndio bao bora na wadau wa soka, Kichuya anaweka wazi kuwa kwake bao bora ambalo hatakaa alisahau, alilifunga dhidi ya Ndanda FC kabla haijashuka daraja na yeye alikuwa anaitumikia Simba kipindi hicho.
“Bao langu bora nilifunga dhidi ya Ndanda, kona ilichongwa na Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, alichonga mpira wa kona ambao ukatemwa na kipa Jackson Chove na kurudi nje kidogo ya 18 haukutua chini niliunganisha moja kwa moja na kutinga wavuni.
“Hilo bao linalotajwa na wengi kuwa ni bora nikiwafunga Yanga kwa kona ya moja kwa moja nilibahatisha tu, mimi sio mzuri kwenye mambo ya kuchonga kona, bao dhidi ya Ndanda nilitumia mguu wangu wa kushoto na kuachia shuti kali ambalo lilikwenda moja kwa moja wavuni,” anasema Kichuya akilitaja bao hilo kuwa hatalisahau.
BAO YANGA, BABA UBAYA NOMA
Wakati bao la Kichuya aliloifunga Yanga kwa kona akikiri kuwa lilimuingizia zaidi ya Sh40 milioni kutoka kwa wadau, mwenyewe anafunguka kuwa alibahatisha kwani hana ufundi wa kufanya hivyo akimtaja Issa Rashid ‘Baba Ubaya’ kuwa ndiye fundi wa hizo kazi.
“Mabao ya kona kuna mchezaji anaitwa Baba Ubaya huyo habahatishi ni fundi maeneo hayo, amefunga zaidi ya mabao manne kwenye mechi tofauti. Nafikiri huyo ndiyo anafaa kupewa sifa hizo siyo mimi,” anasema na kuongeza:
“Nasifiwa kwasababu nilifanya tukio hilo kwenye mechi kubwa ya watani, lakini nawaaminisha kuwa Baba Ubaya ndio mkali wa hizo kazi, mimi ni kweli nilichonga ule mpira, lakini dhamira yangu uende golini au ukutane na wachezaji wenzangu waliojipanga ili wakwamishe nyavuni.
“Ule mpira ulikatika juu kwa juu na kuzama nyavuni sema kwasababu niliifunga Yanga ndio maana mengi yanazungumzwa ila Baba Ubaya ndio fundi wa kufunga mabao ya kona.”
MATUKIO YAMEMBEBA
Jina la Kichuya limetajwa mara nyingi zaidi Ligi Kuu Bara akiwa Simba kutokana na ubora wake hadi kupata nafasi ya kwenda nje kucheza, lakini mwenyewe anafunguka kuwa amebebwa na matukio yaliyompa dili za pesa.
“Mimi imani yangu inaniambia kuwa sina uwezo mkubwa wa kucheza mpira matukio makubwa niliyoyafanya kwenye soka ndio yamekuza jina langu, kuna wachezaji nilianza nao mpira walikuwa wanajua sana lakini walifunikwa na matukio yangu,” anasema na kuongeza;
“Kama isingekuwa kufunga mabao kwenye dabi ningekuwa mchezaji wa kawaida kama ilivyo kwa wachezaji ambao naamini walikuwa na uwezo mkubwa zaidi yangu lakini walishindwa kujulikana kutokana na kutokufanya matukio makubwa.”
Kichuya anasema kuna wachezaji ambao wanafanya vizuri kila msimu kutokana na uwezo wao wa kucheza soka lakini kutokana na kutofanya matukio makubwa kama aliyofanya hawajaonekana.
SOPU, NKANE WAPEWE NAFASI
Licha ya wachezaji Denis Nkane kukosa namba kwenye kikosi cha Yanga kutokana na uwepo wa mawinga wa kigeni wanaofanya vizuri, Kichuya amemkingia kifua na akimtaja kuwa ni mchezaji mzuri anatakiwa kupewa nafasi ili aonyeshe.
“Nkane ni winga mzuri sana na sio huyo tu kwa upande wa wazawa eneo hilo tupo vizuri kuna Iddy Nado na Abdallah Suleiman ‘Sopu’ wote wana uwezo mkubwa na wakipewa nafasi watafanya mambo makubwa kama ilivyo kwa Feisal Salum ‘Fei Toto’ ambaye ameonyesha changamoto akitupia mabao mengi kuzidi washambuliaji,” anasema winga huyo.
“Kila msimu kunaibuka vipaji vipya na kuna vingine vinakosa kuonyesha uwezo wao kutokana na uwepo wa wachezaji wa kigeni ambao wengine hata hawana uwezo lakini kutokana na gharama kubwa wanazopewa wanalazimika kutumiwa tu.”
Anasema hana maana kwamba wachezaji wanaocheza eneo la wingi wote hawana uwezo kuna wengine wamekuwa chachu ya kupandisha uwezo wa wengine lakini anatamani kuona wachezaji wazawa pia wanapewa kipaumbele ili waonyeshe uwezo walionao.
BEKI NI NGALEMA TU
Mawinga na washambuliaji kwenye upambanaji wao wana wababe zao ambao ni mabeki katika harakati za kuwazuia wasifunge kama ambavyo anathibitisha Kichuya.
“Kuna mchezaji anaitwa Paul Ngalema, tangu yupo Ndanda ni beki ambaye tumekuwa tukifanya bato uwanjani kila tunapokutana lazima tusumbuane, sio miaka hiyo tu bali hadi sasa bado tunapambana,” anasema.
“Ni beki ambaye hakubali unyonge, winga ukijiona una kasi sana basi utasikia nipo kazini twende tufanye kazi pamoja, hivyo ilikuwa kazi yangu kuumiza kichwa ili niweze kumtoka na kufanya kitu dhidi yake.”
Kichuya anasema Ngalema ni mtu wa shoka muda wote sio kwake tu lakini ilikuwa akikutana naye alikuwa anajua kabisa atakuwa na kazi kubwa ya kufanya.
TIMU ZOTE ZIWE NA MABASI
Hakuna kitu kigumu ambacho wanakumbana nacho wachezaji kama kusafiri kutoka mkoa mmoja hadi mwingine kutokana na safari ndefu hasa kwa timu ile ambazo zinatumia usafiri wa mabasi.
“Natamani kuona Shirikisho la Soka Tanzania liweke kanuni ya kila timu inayoshiriki Ligi Kuu Bara iweze kumiliki basi kubwa la kusafiria na sio magari mandogo aina ya Toyota Coaster ambayo imekuwa chngamoto kutokana na umbali wa safari,” anasema.
“Mfano timu inatoka Mtwara kwenda Bukoba coaster safari yake ni ndefu sana na ukizingatia ratiba zetu zilivyo, sisi JKT Tanzania tumetoka Bukoba na basi kubwa saa tano usiku tumefika saa tano usiku.”
Kichuya anasema safari ndefu zinachangia wachezaji kushindwa kufanya kazi zao kwa ubora kutokana na uchovu walionao.
MPUNGA, NYANYA, VITUNGUU
Mbali na kutumika kwenye viwanja mbalimbali vya soka winga Kichuya amekiri kuwa yeye amewekeza kwenye kilimo na hata ikitokea akaamua kustaafu basi atarudi mashambani.
“Nisingepata nafasi ya kucheza mpira ningekuwa mkulima kutokana na kutokusoma kulingana na mazingira niliyokulia lakini pia pamoja na kupata nafasi bado nimeamua kuwekeza kwenye kilimo,” anasema.
“Silimi mimi lakini nina mashamba mengi ambayo nalimisha mpunga, nyanya, vitunguu na mazao mengine. Nasema nalima kwa sababu nahusika kwa asilimia kubwa kwenye uwekezaji, mama ndiyo ananisimamia.”