Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

KIBWANA: Yao anajua, ila namba naitaka

Muktasari:

  • Maswali ya mashabiki wengi huwa ni mchezaji huyo yuko wapi na kwa nini hachezi wakati yupo kikosini, ila ukweli ni kwamba sio jambo jepesi kwa staa yoyote kukosa namba kwenye timu aliyokuwa anaichezea.

IMEKUWA kawaida kwa mastaa kuvuma na kupotea hasa kwa upande wa soka, unaweza kuona mchezaji anafanya vizuri msimu huu alafu ujao anapotea au kwa kocha huyu anawika na anapokuja mwingine anapotea.

Maswali ya mashabiki wengi huwa ni mchezaji huyo yuko wapi na kwa nini hachezi wakati yupo kikosini, ila ukweli ni kwamba sio jambo jepesi kwa staa yoyote kukosa namba kwenye timu aliyokuwa anaichezea.

Hayo yanaelezwa na Kibwana Shomari, staa wa Yanga anayeliambia Mwanaspoti sababu iliyomfanya akae benchi takriban msimu mmoja na nusu kwa sababu tu ya machaguo ya kocha.

Staa huyo ambaye ameichezea Yanga misimu mitano akitokea Mtibwa Sugar amefundishwa na makocha watatu ndani ya kikosi hicho akianza na Nasreddine Nabi, Miguel Gamondi na sasa Sead Ramovic.


KIPINDI CHA MPITO

Kibwana anaelezea hali ilivyokuwa wakati yuko nje ya Uwanja na wakati mwingine alikuwa akitazama mechi Jukwaani na anafunguka kuwa, kwake haikuwa rahisi na kilikuwa kipindi cha mpito.

“Wakati nilipokuwa sichezi kilikuwa kipindi cha changamoto ya kazi yetu. Kucheza na kutocheza kila mchezaji huwa anapitia, ila mimi naamini nimemwomba sana Mungu na kufanya sana mazoezi na muda ukafika, basi ndio nipo naisaidia timu kupata matokeo na natamani niendelee kucheza,” anasema mchezaji huyo.


SIRI YA MAFANIKIO

Kibwana ambaye kwa kipindi kirefu hakupata nafasi ya kucheza chini ya kocha aliyepita, hivi sasa ni kama hesabu za Ramovic zimekubali kwani ameanza kupata namba na anaonyesha makali.

Ukiona aina yake ya upambanaji uwanjani ni kama mtu aliyekuwa akisubiri kupata nafasi ili aweze kuonyesha kuwa bado yupo na ana uwezo.

“Nimeanza vizuri kama wengi wanavyosema kwa sababu ya nidhamu na kujua hii ni kazi yangu na pia kusikiliza maelekezo ya mwalimu, hayo ndio mambo pekee yanayonifanikisha.”


KAZINI KUNA KAZI

Staa huyo anasema chanzo cha kuweka posti yenye ujumbe wa “KAZINI KWANGU KUNA KAZI” msimu uliopita katika mtandao wake wa kijamii kuwa, haukuwa na maana kama wengi walivyodhani.

“Ujue watu wanalichukulia tofauti sana lile neno. Leo nitasema ukweli kwani wengi wanahisi nimeandika vile kwa sababu ya Yao (Kouassi) anacheza halafu mimi sichezi,” anasema.

“Lakini niliandika lile neno kabla hata Yao hajulikani atakuja lini, nikimaanisha kuwa mtu unapambana uwanjani jasho jingi linakuvuja ndio maana nikasema vile wala sio kuhusu mchezaji mwenzangu kwamba ujio wake unanipa wakati mgumu.”


USHINDANI BALAA

Tangu kutua kwa Yao, raia wa Ivory Coast, msimu uliopita, ndipo kulimfanya Kibwana kupata namba kwa mashaka na hapa anazungumzia ushindani jinsi ulivyo ndani ya Yanga.

“Nadhani mchezaji kutoka sehemu moja kwenda sehemu nyingine ni kitu cha kawaida na ushindani kwenye nafasi moja kuwa mkubwa kunasaidia timu kupata matokeo,” anasema Kibwana.

“Halafu Yao ni mchezaji bora sana na kocha ndio anaamua mtu gani wa kucheza kutokana na mahitaji ya mechi. Ndio maana ukaona mimi sichezi kwa sababu Mwalimu alimchagua na yeye ndio alikuwa changuo la kwanza na aliisaidia timu tulikuwa tunapata matokeo, huwezi kumuweka nje mchezaji kama huyo.”


UJIO WA RAMOVIC

Ramovic ni kocha ambaye amekuja kuwakumbusha mashabiki wa Yanga kuwa Kibwana bado yupo ndani ya Yanga baada ya kuanza kumtumia kutokana na Yao kupata majeraha na staa huyo anamzungumzia ni kocha wa aina gani kwake.

“Ni kocha mzuri na ameamua kunipa nafasi ya kucheza sio kwa sababu mimi ni chaguo lake sana kuliko wengine, lah, ila kama kocha anaangalia mechi husika inamhitaji nani kutokana na malengo aliyonayo.

“Nashukuru sana kuwa ameona nilicho nacho na ndio maana ananipa nafasi na mimi kwa sababu hii ndio kazi yangu lazima nitaifanya ipasavyo.”

MSIMU DUME

Kibwana ameichezea Yanga katika misimu mitano sasa, huku miwili ikishiriki Kombe la Shirikisho Afrika na kutinga fainali, lakini sasa inacheza Ligi ya Mabingwa Afrika.

Kibwana katika rekodi za ligi akiwa Yanga ameisaidia timu kuchukua ubingwa wa Ligi Kuu Bara mara tatu mfululizo, lakini anaweka wazi kuwa misimu yote ilikuwa migumu kwake.

“Misimu yote ni dume kwa sababu ligi yetu ni ngumu sana halafu Yanga ni timu kubwa, hivyo inabidi mjipange ili kuweza kupata matokeo, hivyo hata mechi zote sio rahisi pia.”


MIPANGO

Kibwana baada ya kuanza kucheza anasema mipango yake ndani ya kikosi cha Ramovic ambaye ameonyesha kumuelewa, huku akisema kuwa kuisaidia timu ni moja kati malengo yake.

“Malengo yangu ni kuisaidia timu kupata matokeo mazuri katika mechi zote ambazo tutacheza ili kufikia maazimio ya klabu na sisi kama wachezaji tuliojiwekea,” anasema.


UFUPI UNAVYOUMIZA

Miongoni mwa wachezaji wenye vimo vifupi katika kikosi cha Yanga na ligi kwa ujumla huwezi kuacha kumtaja Kibwana, anayeliambia Mwanaspoti kuwa ufupi wake ndio uliomfanya apambane ili kuwaaibisha waliokuwa wakimcheka.

“Kipindi niko mdogo kuna changamoto za kutengwa kutokana na umbile langu. Ilikuwa shida kwa sababu unadharaulika, lakini inaumiza na ilinifanya nipambane zaidi.”

“Kinachonifurahisha zaidi ni maisha ya Yanga, vaibu la mashabiki (kuna) wakati huwa linanifanya nitamani kufanya vizuri zaidi ili kudumisha shangwe.”


MECHI ZOTE NGUMU

“Mechi zote zilikuwa ngumu kwani kila mchezo unakuja na mipango yake hivyo nikikaa na kuangalia naona kabisa kuwa hakuna rahisi kama kuna mpinzani ujue kazi ipo.

“Ujue kila timu ni nzuri na zimejipanga na zina wachezaji na sisi huwa tunatakiwa tujipange ili kusudi tupate matokeo na hapo ndipo unapokuja ugumu wa mechi.”


NJE YA NCHI

Kama zilivyo ndoto za wachezaji wengi kuvuka mipaka na kucheza nje ya nchi zao na kwa Kibwana ni vivyo hivyo, huku akiweka wazi kuwa ikipatikana nafasi hiyo basi ataitumia.

“Mipango yangu ni kucheza nje na Yanga mwenyezi Mungu asaidie hiyo nafasi ya kuiwakilisha nchi yetu sehemu zingine ipatikane hayo ndio maombi ya wachezaji wengi.”

NJE YA UWANJA

Wengi wanawafahamu wachezaji tu kwa kuwaona uwanjani, hapa Kibwana anaeleza maisha yake nje ya soka na anasema kuwa ni mtu poa sana.

“Mimi ni kijana wa kawaida tu mstaarabu, mpole na mtu wa watu. Licha ya kuwa nataniwa sana na Denis Nkane ila tumezoeana sana, lakini pia napenda sana kuangalia sinema na kupika pia,” anasema.

“Wakati mashabiki wananiulizia na hata kutoa maoni kwenye mitandao nilikuwa na hiyo ilikuwa inanifanya nihisi upendo, lakini pia ilinifanya nijue kuwa kuna kitu niliwahi kufanya cha kukumbukwa.”