Kiatu cha dhahabu AFCON 2025 kipo hapa!
Muktasari:
- Wakati timu hizo zikitarajia kupigana vikumbo kwenye mashindano hayo yatakayofanyika Morocco, vita nyingine itakuwa miongoni mwa wachezaji watakaokuwa na kazi ya kuonyesha ubabe kwenye nani kiboko kwa kutumbikiza mipira nyavuni.
RABAT, MOROCCO: MCHAKAMCHAKA wa mashindano ya ubingwa wa Afrika kwa timu za soka za taifa unatarajia kuanza Jumamosi hii na mataifa yataanza harakati wa kuwania ufalme wa michuano hiyo iliyofahamika kwa jina la AFCON 2025.
Wakati timu hizo zikitarajia kupigana vikumbo kwenye mashindano hayo yatakayofanyika Morocco, vita nyingine itakuwa miongoni mwa wachezaji watakaokuwa na kazi ya kuonyesha ubabe kwenye nani kiboko kwa kutumbikiza mipira nyavuni.
Kinara wa mabao kwenye Afcon 2025 ni vita inayosubiriwa kwa hamu kutokana na mashindano hayo kushirikisha mastaa wa maana na hodari kwenye kupasia nyavu.
Kwa kawaida, mchezaji mwenye uwezo wa kufunga mabao manne hadi matano atakuwa na uhakika wa kuibuka mshindi kwenye kukibeba Kiatu cha Dhahabu cha mashindano hayo. Lakini, swali linaloulizwa kwa sasa ni nani mchezaji huyo?
Hata hivyo, kuna mastaa watatu ambao wengi wanaamini mshindi wa Kiatu cha Dhahabu cha Afcon 2025 atatokea miongoni mwao. Je, utabiri utakwenda kutokea kweli au kuna mastaa mwingine asiyejulikana, atafunika kwa mabao?
1. Victor Osimhen (Nigeria)
Straika Victor Osimhen kama kuna kitu anajua kukifanyia kazi ipasavyo, basi ni kuhakikisha mpira unagusa kwenye nyavu za wapinzani. Mnigeria hiyo hajawahi kuwa mvivu kwenye suala la kutumia nafasi anazopata. Kwa sasa anakipiga kwenye kikosi cha Galatasaray na amekuwa moto kwelikweli kwenye kucheka na nyavu. Kama atatua Morocco na kikosi chake cha Super Eagles huku akiwa kwenye ubora wake, basi kuna uwezekano mkubwa Kiatu cha Dhahabu kikatua Nigeria.
2. Mohammed Salah (Misri)
Wikiendi iliyopita, Mohamed Salah aliliweka jina lake kwenye vitabu vya rekodi vya Ligi Kuu England kuwa mchezaji aliyehusika katika mabao mengi akiwa na klabu moja. Mo Salah amehusika kwenye mabao 277.
Lakini, sasa atahamishia makali yake kwenye mashindano ya Afcon 2025 akiwa na kikosi cha Misri, ambacho kimelenga kufanya vyema katika mikikimikiki hiyo ya Morocco.
Kwenye suala la kufunga mabao, Mo Salah hajawahi kuwa na tatizo, huku ubora wake wa kupachika nyavuni ndicho kilichomfanya Misri wamtambue kama mpiga wa penalti wao.
3. Sebastian Haller (Ivory Coast)
Kama Ivory Coast itafika mbali kwenye mashindano ya Afcon 2025, basi mchezaji mmoja ambaye watamhitaji sana awafungie mabao basi ni straika Sebastian Haller. Alifunga bao la ushindi kwenye mechi ya fainali ya Afcon 2023 na kuipa Ivory Coast ubingwa wa taji hilo na hivyo watakwenda Morocco wakiwa mabingwa watetezi.
Kwenye suala la kufunga mabao, Haller ni hodari kwelikweli na hilo ndilo linalomfanya kuwekwa kwenye orodha ya mastaa watatu wenye nafasi kubwa ya kunyakua Kiatu cha Dhahabu kwenye Afcon 2025.