Katikati ya Tuisila, Luis nawamisi kina Lunyamila

Muktasari:

YANGA huwaambii kitu kuhusu Tuisila Kisinda kwa sasa. Wanafurahishwa na kasi yake uwanjani.

YANGA huwaambii kitu kuhusu Tuisila Kisinda kwa sasa. Wanafurahishwa na kasi yake uwanjani.

Kasi ambayo wakati mwingine huwapa tabu mabeki wa timu pinzani. Joash Onyango ni mmoja wa wahanga wa kasi ya winga huyo kutoka DR Congo.

Hata hivyo, Tuisila hana madhara makubwa kama aliyonayo Luis Miquissone. Winga matata wa Wekundu wa Msimbazi. Luis amemzidi sana Tuisila kwa mambo mengi. Luis anachenga za maudhi, ana kasi kubwa na ana uwezo wa kumiliki mpira.

Kikubwa zaidi, jamaa anajua kufunga. Al Ahly wanamjua. Aliwatungua jijini Dar es Salaam. Kama ambavyo Yanga wanatambia Kisinda, Simba nao huwaambii kitu kwa Luis.

Sio hao tu, lakini hata nyota wengine wakali waliopo ndani ya timu hizo wamekuwa wakipagawisha mashabiki wa klabu hizo za Kariakoo. Mashabiki wamekuwa wakiwaimba mdomoni na kuwatukuza.

Utabisha nini, wakati huwa mnasikia namna Clatous Chama, Meddie Kagere, Larry Bwalya, Taddeo Lwanga ama Jonas Mkude wanavyoimbwa na mashabiki wa Msimbazi?!

Utasema nini, wakati kila uchao mashabiki wa Jangwani wanawataja kina Fiston Abdulrazaq, Saido Ntibazonkiza, Yacouba Songne, Feisal Salum ama Lamine Moro?

Hii ni kawaida, ya kila upande kusifia wachezaji hao hata kama wakati mwingine huwa hawana maajabu makubwa. Ni kama tu anavyoimbwa Tuisila na kasi yake, lakini ni Yanga hao hao walikuwa na winga teleza aliyetikisa nchini na Afrika Mashariki na Kati, Edibily Lunyamila.

Utakataa nini juu ya uwezo mkubwa aliokuwa nao Lunyamila na mawinga wengine hatari waliowahi kuwika miaka kadhaa iliyopita ndani ya Yanga na klabu nyingine nchini?

Kama Tuisila leo anawapagawisha mashabiki wa Yanga wa sasa, vipi mashabiki hao wangebahatika kumwona Lunyamila aliyemstaafisha soka nahodha wa SC Villa na timu ya taifa ya Uganda, Paul Hasule?

Lunyamila aliyewapagawisha Waganda hata kuliandika jina lake kwenye migahawa, teksi na daladala zao kwa kukunwa na soka lake lililowapa burudani katika Fainali za Kagame 1993.

Fikiria tu kama Luis au Bwalya anatajwa kama viungo mshambuliaji hatari, vipi kama kizazi hiki wangemuona Itutu Kiggy ‘Road Master’, Sunday Juma ‘Pikipiki’, Damian Kimti au Abubakar Salum kama sio David Mjanja au Celestine ‘Sikinde’ Mbunga?

Ni kweli kina zama na nabii wake na kitabu chake, lakini bado kuna sehemu wachezaji wa kizazi cha sasa wazawa wamekuwa wepesi kiasi cha kuwapa ujiko usio na sababu nyota wa kigeni.

Aidha sifa kubwa wanazopewa wachezaji wa kigeni kutokana na kiwango wanavyoonyesha kwenye baadhi ya mechi zimechangia kuzivuruga akili za mashabiki wa klabu nyingi nchini.

Kwa waliomwona Lunyamila, Sunday Juma au Ephraem Makoye ‘Digidigi’ enzi za ubora wao, watakubaliana nami, ni mawinga au viungo washambuliaji wachache waliopo nchini wakiwamo wazawa na wale wa kigeni waliowafikia kwa ufundi wao.

Ni kama ambavyo viungo wa zama hizi wanavyosifiwa kwa ufundi, lakini wakiwa wameachwa mbali sana na viungo mafundi wa mpira waliowahi kutokea nchini kama Hamis Thobias Gaga ‘Gagarino’, Said Mwamba ‘Kizota’, Ramadhan Lenny Maufi, Method Mogella ‘Fundi’ na wengineo.

Viungo wa miaka ya nyuma, walikuwa wanajua kuurahisisha mpira. Waliburudisha, pia kuzipa timu matokeo uwanjani.

Sio kama hakuna viungo wazuri la hasha! Huyu Clatous Chama anajua sana soka. Hata Luis naye ni balaa, Mkude naye ni matata kama ilivyo wa Feisal Salum ama Mudathir Yahya na Salum Abubakar na wanafanya kazi kubwa uwanjani, lakini hakuna warembaji wanaoweza kuwafanya mashabiki

watokeo makwao wakiwa na hamu ya kwenda kulipa kiingilio ili washuhudie mambo mawili kwa wakati mmoja. Yaani kuona soka la nguvu na pili kupata burudani kama waliokuwa wakiitoa kina Kizota, Gagarino, Abdallah China na wenzao kadhaa baadhi wakiwa hai na wengine kutangulia mbele ya haki.

Ramadhan Chombo ‘Redondo’, Haruna Moshi ‘Boban’ ni baadhi ya viungo waliokuwa wakipita njia walizopita kina China na Gaga. Jamaa walikuwa mafundi. Kwa sasa Chombo hana ule

utamu wale aliporudi nchini kutoka Ulaya. Pengine umri umeanza kumtupa, lakini uwezo alikuwa nao fundi huyo wa zamani wa Simba na Azam, ungekuwa zama hizi sidhani kama mashabiki wa Jangwani wangekuwa wanamuimba Kisinda au Saido! Ukali aliokuwa nao George Lucas ‘Gazza’ au Abdallah Msamba, sidhani kama Simba wangepagawa na kina Luis au Chama. Sijui...!

Bahati mbaya zaidi ni kwamba wachezaji wazawa wa kizazi cha sasa ni wavivu flani na wasio na wivu wa vipaji vyao. Hawapendi mazoezi na wala hawajishughulishi kufanya makubwa ndani ya timu zao. Wameridhika kukaa benchi ilimradi akaunti zao zinasoma mihamala! Halafu sasa, vyombo vya habari navyo vimekuwa vikiwakuza sana nyota wa kigeni hata kama hawana maajabu makubwa uwanjani.

Leo hii haishangazi, Deus Kaseke anachukuliwa wa kawaida, lakini sifa akajazwa Fiston au Saido kwa kuangalia rekodi baina yao zinatofautiana sana kikosini!

Simba kuna mwanamme wa shoka, Mzamiru Yassin ambaye kazi anayoifanya kikosini wala haimbiwi, lakini jamaa ni punda anayeubeba mzigo Msimbazi, huku sifa wakipewa wengine.

Najua kuna watu hawatanielewa, lakini ukweli ni kwamba hao kina Kisinda na hata Larry Bwalya kila nikiangalia soka lao na sifa wanazopewa, huwa nawakumbuka sana kina Lunyamila.

Natamani miaka ingerudi nyuma, ili hawa mashabiki wanaopagawa kwa sasa na nyota hao wa kigeni wavurugwe kabisa na soka tamu na lenye tija kutoka kwa wakali hao wa kizawa waliotetemesha nchi.

Hata hivyo rai tangu kwa nyota wa kizawa kujitathmini juu ya vipaji walivyonavyo, umri na kazi wanazozifanya uwanjani kama zinalingana! Kwani ni jambo la aibu kina Niyonzima walioanza kuchoka wanaendelea kufunika. Leo Chama aliyepungu makali, eti akiimbwa mdomoni, ilihali kuna mayanki kibao wenye uwezo mkubwa wa kusukuma ndinga pale Msimbazi, lakini wenyewe wakiwa wameridhika...Inashangaza sana!

Inashangaza kama ambavyo Meddie Kagere, Pascal Wawa au Saido ambao umri umeanza kuwapa mkono wanavyokimbiza nchini, huku wazawa tena vijana wakiwa wanyonge, wakati damu zao bado changa na zimechangamka!

Inawezekana kuna mahali tunakosea. Ama kwenye mafunzo ambayo nyota wetu wanapewa na makocha wao, ama ubishi na kujifanya kujua kwingi kwa vijana hao na kufanya washindwe kufanya yale ambayo yalifanywa na kaka na baba zao enzi wakicheza.

Naamini kwa teknolojia na dunia iliyo sasa, inayowawezesha nyota waliopo sasa kujifunza vitu vingi kupitia mastaa kadhaa wa kimataifa, kisha kuchanganya na vipaji walivyonavyo ni wazi watafunika.

Pengine uvuvi na kuamini wamefikia kilele cha mafanikio ndio maana wala hawajali kusikia kina Chama, Kisinda, Niyonzima ama Kagere na wenzao wengine wakisifiwa na kuimbwa na mashabiki.

Imeandikwa na BADRU KIMWAAGA