Karibu Makonda mahali usio na ugeni nako
Muktasari:
- Hamu yetu kubwa ilikuwa ni kuona kina nani wangepewa fursa hiyo adhimu na Rais wa Nchi kusimamia wizara yetu pendwa inayohusika na michezo ambayo pia ina habari, utamaduni na sanaa.
KIJIWENI hapa siku ya Jumatatu tulikuwa bize kusubiria uteuzi wa Baraza la Mawaziri wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania walioteuliwa na Rais Samia Suluhu Hassan baada ya Uchaguzi Mkuu 2025.
Hamu yetu kubwa ilikuwa ni kuona kina nani wangepewa fursa hiyo adhimu na Rais wa Nchi kusimamia wizara yetu pendwa inayohusika na michezo ambayo pia ina habari, utamaduni na sanaa.
Hatimaye Rais Samia alitangaza Baraza hilo na katika Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo tukapewa Waziri yuleyule, Profesa Palamagamba Kabudi na msaidizi wake Hamis Mwinjuma ‘Mwana FA’ aliyerudishwa pia hapo hapo.
Hata hivyo, wizara hiyo imeongezwa Naibu Waziri mmoja ambaye ni Paul Makonda jambo lililofanya sasa Profesa Kabudi awe na Manaibu Waziri wawili chini yake.
Wanamichezo tulio wengi tunapongeza uteuzi wa mabosi hao wa wizara ya michezo kwa vile katika kipindi chao cha kwanza, Kabudi na Mwana FA waliisimamia vyema wizara hiyo na ikawa ni miongoni mwa zilizoipa sifa nzuri nchi yetu.
Lakini ongezeko la Makonda tunaamini litakuwa na tija na litaongeza kitu kwa wizara kwa vile huyo ni mtu anayeweza kusimamia vyema uwajibikaji na yeye mwenyewe amekuwa msimamizi mzuri wa idara au taasisi ambazo huwa anapewa kuzisimamia.
Kubwa zaidi katika michezo, Makonda sio mgeni na ana uzoefu na mchango mkubwa ambao wengi tunaukumbuka hapo nyuma hivyo tunaweza kusema upele umemkuta mkunaji maana ni mtu ambaye haingii michezoni kama mgeni.
Makonda aliwahi kuwa kiongozi wa Kamati ya Hamasa ya timu ya taifa, Taifa Stars ambayo ilitoa mchango mkubwa katika kuiwezesha timu hiyo kufuzu AFCON 2019 nchini Misri ambazo zilikuwa fainali zake za kwanza kushiriki tangu ilipofanya hivyo mwaka 1980.
Kwa kushirikiana na aliowakuta kwa maana ya Waziri Kabudi na Naibu mwenzake, Mwana FA, hakuna shaka michezo itapiga hatua sana.