Prime
Kamati ya Saa 72 ilivyokosea kumuadhibu Diarra, Mrina
KWA takriban wiki tatu sasa habari kuu ni zile zinazotokana na uamuzi wa Kamati ya Usimamizi na Uendeshaji wa Ligi, ama Kamati ya Saa 72 ambayo inaonekana inafanya kazi kutokana na mihemko au shinikizo la wachambuzi.
Hii ni kamati, kwa sababu zisizojulikana, imepewa mamlaka makubwa na mengi kiasi kwamba hakuna vyombo vingine vya mpira wa miguu vinavyofanya kazi. Kibaya zaidi ni kwamba uamuzi wake hauwezi kupingwa hata kama ni mbovu kama ule wa kusema mwamuzi “alikataa goli halali” uhalali uliopatikana mezani.
Hii ni kamati ambayo inafanya uamuzi wa Kamati ya Nidhamu, inafanya uamuzi wa Kamati ya Maadili, inafanya uamuzi wa Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji. Binafsi, kwa muda mrefu wa takriban miaka mitatu sijawahi kuisikia Kamati ya Nidhamu ikishughulikia suala lolote la kinidhamu. Ni Kamati ya Saa 72 tu iwe nidhamu, maadili au sheria.
Ni muhimu sana mgawanyo wa kazi ukawepo ili kila jambo liamuliwe kulingana na muktadha wake. Kamati za nidhamu, maadili na sheria zina wataalamu wa sheria wanaojua kushughulikia masuala ya kisheria kitaaluma zaidi. Wanaojua mpira wa miguu ni ajira inayohitaji mazingira mazuri ya kuwawezesha wachezaji, makocha na waamuzi kufanya kazi zao na kushughulikiwa kisheria bila ya kuathiri taaluma yao kwa kiasi kikubwa.
Ni muhimu sana zile sababu zilizofanya Kamati ya Nidhamu iundwe, ziangaliwe upya ili masuala yote ya kinidhamu yashughulikiwe na wataalamu hao wa nidhamu. Kamati hiyo inaweza kuwa na watu waliojikita katika masuala tofauti kama hayo ya uwanjani na nje ya uwanja kama kanuni za nidhamu zinavyoeleza.
Narudia kusisitiza kuwa asili ya Kamati ya Saa 72 ni Kamati ya Mashindano ambayo jukumu lake kuu lilikuwa ni kuidhinisha uamuzi wote uliyofanywa uwanjani na kuwa rasmi ili uingie kwenye kumbukumbu za Shirikisho la Soka (TFF) na wasimamizi wa ligi. Yaani kama mchezaji ameonyeshwa kadi tatu za njano mfululizo, basi taarifa hizo zitakuwa zimeidhinishwa rasmi na Kamati ya Saa 72.
Na suala la uamuzi wake kuwa wa mwisho usiopingwa ni kutokana na kazi ya kamati hiyo kuwa ni kubariki uamuzi wa marefa uwanjani. Kwamba mambo yanayotokea ndani ya dakika 90, muda mfupi kabla ya kuanza kwa mchezo na muda mfupi baada ya kuanza kwa mchezo hayawezi kupingwa kwa kuwa ni ya waamuzi.
Ndio maana hayo uamuzi hauwezi kupingwa. Suala la kipa Djigui Diarra kuonyesha kidole cha kati si suala lililoamuliwa na refa, bali lililotokana na taarifa mbalimbali za vyombo vya habari. Hivyo, Kamati ya Saa 72 imelianzisha na kwa maana hiyo, mtuhumiwa alitakiwa ataarifiwe na kushtakiwa kwa Kamati ya Nidhamu na siyo kumhukumu kwa kutumia picha za video au za mnato bila kupewa haki ya msingi ya kusikilizwa.
Uamuzi mkubwa wa kumshusha daraja refa Gilbert Mrina haukutakiwa kufanywa na kamati ambayo uamuzi wake ni wa mwisho kwa kuwa unahusu kuathiri kwa kiasi kikubwa fani yake. Huu ni uamuzi ambao ulitakiwa ufanywe kiufundi na Kamati ya Waamuzi iridhike kuwa hakumuadhibu Diarra kwa sababu za njama, hila au kurubuniwa au aliamua kutomuadhibu kwa kuwa aliona alichokuwa akisema kina mantiki.
Kwa jinsi mwenendo ulivyo, kuna hatari ya Kamati ya Saa 72 kuadhibu kila refa au mwamuzi msaidizi atakayechezesha mechi za Simba, Yanga na kidogo Azam kwa kuwa ndizo zinazozusha mijadala mikubwa kuhusu uamuzi, kiasi kwamba watu wanasahau kuwa kuna mambo yanayowaongoza waamuzi katika kufanya tafsiri ya sheria kuamua jambo fulani na si kuiangalia sheria peke yake.
Hawa wachambuzi wa redioni, kwenye televisheni na mitandaoni hawana huo ujuzi unaoweza kuwaongoza kufikia uamuzi kama marefa waliosomea na wanaoifanya hiyo kazi kila siku. Na kibaya zaidi ni kwamba si lazima maoni yao yalingane na maoni ya refa ambaye sheria inampa mamlaka ya mwisho.
Kwa hali ilivyo, ni rahisi kwa Kamati ya Saa 72 kupanga timu itakayotwaa ubingwa. Ni rahisi kwao kuanzisha jambo na kulihukumu bila mtuhumiwa kupewa haki yake ya kusikilizwa. Sasa ikitaka kuiandama timu ambayo haitaki itwae ubingwa, kuna uwezekano ikaanzishiwa mambo mengi kiasi kwamba ikifikia wakati wa mechi muhimu, inakosa wachezaji wengi muhimu kwa sababu ya adhabu zisizopingwa na ambazo hazikutokana na makosa ya uwanjani.
Na kwa sababu kamati imeanza kuadhibu hata matukio ya kupoteza muda, mengi yanakuja.
Cha muhimu ni mamlaka ziangalie masuala haya kwa makini ili kamati za TFF zifanye kazi zake ipasavyo na si kamati moja kuamua kila kitu. Hii ni hatari kwa mpira wetu na unaweza kupoteza ladha.
Sakata la Senegal kuvuliwa ubingwa liliamsha hisia kuwa “iwapo matokeo ya uwanjani yataanza kugeuzwa mezani, watu wataacha kuamini kile wanachokiona” na matokeo yake ni mashabiki kupungua viwanjani kwa kuwa hawatavumilia tena kuona sinema.