Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kahama Mabasi FC mzuka sana, masela wanapita njia ya Stand United

UNAIKUMBUKA Stand United 'Chama la Wana' iliyokuwa na amsha amsha za kibabe Kanda ya Ziwa ilipanda Ligi Kuu msimu wa 2014/15 tena kwa kuweka rekodi kwani iliunga moja kwa moja kutoka wilayani, mkoa, ligi ya Kanda kisha Ligi Daraja la Kwanza na kupanda kipindi hicho.
Wakati huo chama hilo la wana ambalo wamiliki wake walikuwa ni masela wa kituo kikuu cha mabasi cha mikoani na kile cha wilayani ambao wengi wao walikuwa ni wapiga debe, mawakala na wafanyabiashara waliopo vituo hivyo viwili walikuwa wa moto kwelikweli.
Siku ambayo Stand United ilikuwa ikicheza basi ujue mji wa Shinyanga lazima utasimama hata shughuli za kila siku pale kwenye vituo vya mabasi basi ujue zitasimamishwa masela wote wataelekea uwanjani tena wakiwa vitu kichwani.


Mashabiki hao katika kipindi chote timu inacheza kuanzia wilayani hadi wanapanda Ligi Kuu walikuwa wakiipa sapoti chama lao, kwao ilikuwa jambo la kawaida kukodisha mabasi zaidi ya matano na kwenda nayo mikoani kuishangilia timu yao.
Shangwe na mzuka huo wa Stand United haupo tena na timu ilishashuka na inapambana kwenye First League lakini ile amsha amsha iliyokuwa inasimamisha mji wa Shinyanga kwa sasa huwezi kuwaona mashabiki wale hawapo kabisa.
Kwa sasa habari ya mjini ni Kahama Mabasi FC ambayo amsha amsha zake zinafanana kabisa na Stand United kwani wamiliki wa hii timu ya wilayani Kahama ni wapiga debe, mawakala na masela wa vituo vya mabasi.
Hii timu sasa ndio mabingwa wapya wa wilaya ya Kahama ambayo inamilikiwa na vituo vinne vya mabasi ambavyo ni CDT, Stendi Kuu, Majengo na Stendi ya Dodoma ambazo ziko wilayani humo.
Timu hiyo siku ikicheza basi ujue mji wa Kahama utawaka moto na usiombe wakashinda au wakatoa sare mchezo watakaocheza basi hilo shangwe lake litakuwa balaa hebu angalia masela wa vituo nne vya mabasi wakiungana hilo vaibu lake kuna mtu wa kulizima kweli.
Chama hilo usilichukulie poa kabisa kwani ndio timu pekee inayowezekana iliyo katika madaraja ya chini ambayo nyota wake wanaishi kistaa, wachezaji na benchi la ufundi wanalipwa mishahara,posho huku wakikaa kwenye kambi ambayo wanapata huduma zote stahiki.
Hata hivyo pesa za kuigharamia klabu hiyo zinatoka kwa wadau hao ambao wanajichangisha kila siku ambao kila mpiga debe, wakala na mfanyabiashara aliyopo kwenye stendi hizo nne utoa sh 1000 kuichangia timu hiyo.


ILIANZISHWA JUZIJUZI
Mwenyekiti wa klabu hiyo, Baraka John alisema timu hiyo ilianzishwa Mei mwaka huu ikiwa ni lengo la kuwa na kikosi ambacho kitashiriki mashindano mbalimbali ndani na wilaya hiyo na kuwapa burudani baada ya kazi.
Anasema sasa malengo yao ni kuhakikisha wanavuka hatua moja hadi nyingine mpaka wanapanda Ligi Kuu kama walivyofanya ndugu zao Stand United miaka tisa iliyopita na watapambana ili kufanikisha mikakati hiyo.
"Ndio tumeanza kazi sasa tunataka tufikie mafanikio ya wenzetu Stand United walianzia huku tulipo mpaka wakafika Ligi Kuu najua haikuwa jambo jepesi lakini walipambana na kufikia malengo yao waliyojiwekea," anasema John.


KOCHA HUYU HAPA
Kocha wa timu hiyo, Mussa Shamba anasema haikuwa kazi rahisi kwao kutwaa ubingwa huo kutokana na ugumu wa mashindano hayo lakini walikomaa na kuweza kutwaa taji hilo kwa mara ya kwanza.
Anasema kwa sasa wako katika maandalizi ya nguvu kwa ajili ya ligi ya mkoa wa Shinyanga itakayoanza Novemba 2 ambapo katika kikosi chake atasajili wachezaji 30 huku saba wakiwa na wapya ambao muda wowote watawatangaza.
"Ligi ya mkoa huwa inakuwa ngumu sana ndio maana tumeanza kujiandaa mapema sana malengo yetu benchi la ufundi ni kuhakikisha kwanza tunanyakuwa ubingwa wa mkoa kisha tunaenda kukomaa kwenye mashindano ya mabingwa wa mikoa," anasema Shamba.


NAHODHA AWAPA MZUKA
Nahodha wa kikosi hicho, Haruna Nurdin anasema wanajua wana jukumu nzito kwa mashabiki wa soka wa wilaya hiyo hivyo watapambana ili timu hiyo ifanye vizuri na kutwaa ubingwa wa mkoa wa Shinyanga kisha kujipanga upya kwenye ligi ya mabingwa.
"Tunaona mashabiki wanavyojitoa kwa ajili yetu hivyo nasi ni lazima tukomae Ili tufanye vizuri kwenye ligi ya mkoa ambayo huwa ni ngumu sana kikubwa tunaomba waendeleze sapoti yao katika kipindi chote mashindano yatakapochezwa," anasema.


MASHABIKI HUWAELEZI KITU
Shabiki Mussa Savimbi wa Stendi kuu ya mabasi, anasema wataendelea kuisapoti timu hiyo kwa michango mbalimbali kwani wanatamani kuiona ikicheza Ligi Kuu kitu ambacho kwao itakuwa ni furaha zaidi.
"Kama ndugu zetu Stand United waliweza kupanda Ligi Kuu sisi tutashindwaje tena walianzia huku huku tuliko hivyo tunajipanga mdogo mdogo hadi tunafikia malengo yetu," anasema Savimbi.
Shabiki mwingine,William Kulagalilwa anasema hii timu ndio inayowapa furaha wao hivyo wataipambania ili kufikia malengo waliyojiwekea ya kucheza Ligi Kuu kitu ambacho anaamini kwa umoja waliokuwa nao watafanikiwa.


"Niwaombe mashabiki wenzangu tuendelee kutoa michango ya kila siku tuliyojiwekea kwa sababu ndio inayotegemewa kulipa mishahara,chakula,posho na gharama za kambi kwa timu yetu," anasema Kulagalilwa.