Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mastaa ‘walivyoziua’ timu zao Ligi Kuu

Muktasari:

  • Ligi Kuu inatarajiwa kuendelea Juni 12 kwa mechi tatu kupigwa katika viwanja tofauti, ambapo Fountain Gate itakuwa mwenyeji wa Azam FC, KMC ikiialika TRA United na Coastal Union ikimpokea Namungo jijini Tanga.

WAKATI Ligi Kuu ikiwa imesimama kwa muda kupisha kalenda ya Shirikisho la Soka Duniani (FIFA), imeshuhudiwa tamu na chungu kwa baadhi ya wachezaji kufanya ‘maajabu’ ya kuzibeba na kuziangusha timu zao.

Ligi Kuu inatarajiwa kuendelea Juni 12 kwa mechi tatu kupigwa katika viwanja tofauti, ambapo Fountain Gate itakuwa mwenyeji wa Azam FC, KMC ikiialika TRA United na Coastal Union ikimpokea Namungo jijini Tanga.

Hadi sasa, Yanga ndiyo vinara wa Ligi Kuu wakitetea taji lao la tano mfululizo kwa pointi 61, wakimtangulia mtani wao Simba kwa pointi mbili, huku Azam FC iking’ang’ania nafasi ya tatu kwa pointi 52.

Vita ya nafasi nne ni nzito zaidi, ambapo timu za Singida Black Stars (41), JKT Tanzania (38) na TRA United (37) zinapigana vikali kumaliza katika nafasi hiyo ili kuwakilisha nchi kwenye mashindano ya kimataifa.

Mbali na presha ya kumaliza ndani ya ‘Top Four’, hekaheka nyingine ni kwenye kupambana kutoshuka daraja, ambapo KMC inayoburuza mkia ni kama hesabu zinakataa huku ikisubiri muujiza wa kunusurika. Timu za Mashujaa iliyo nafasi ya 11 kwa pointi 27, sawa na Mtibwa Sugar, Namungo (25), Mbeya City (22) na Tanzania Prisons (20) zinawindana vikali kukwepa kushuka daraja na kucheza mechi za mchujo (play-off).

Utamu mwingine katika ligi hiyo msimu huu ni katika mbio za kuwania tuzo ya mfungaji bora, ambapo hadi sasa kiungo wa Azam FC, Feisal Salum, ndiye kinara akiwa na mabao 14, akifuatiwa na nyota wa Yanga, Allan Okello, mwenye mabao 11.

Hata hivyo, katika uhondo wa Ligi Kuu, wapo wachezaji walioonyesha ubora na kuzisaidia timu zao kupata matokeo mazuri, lakini pia wapo baadhi waliozikaanga timu zao kwa kujifunga. Mwanaspoti linakuletea orodha ya wachezaji waliojifunga katika timu zao na kuzinufaisha timu pinzani, jambo lililowatia katika presha kubwa ndani na nje ya uwanja kutokana na hisia za wadau na mashabiki wa soka.


JAMES MWASHINGA (PAMBA JIJI)

Beki huyo tegemeo wa Pamba Jiji alijikuta akiizamisha timu yake wakati wa mchezo dhidi ya Mtibwa Sugar uliopigwa Januari 25 mwaka huu na kumalizika kwa Pamba Jiji kufungwa bao 1-0. Bao hilo lilipatikana katika dakika za nyongeza kupitia shuti la Twalib Muhenga lililombabatiza Mwashinga wakati akijaribu kuokoa hatari na mpira kuishia wavuni.


KENNY ALLY, HANCE MASOUD (KMC)

Pamoja na kuwa mkiani mwa msimamo wa ligi hadi sasa, KMC haitasahau kipigo cha mabao 3-0 dhidi ya TRA United walipokutana katika Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mjini Tabora, mchezo ambao ulionekana kuwa wa upande mmoja.

Katika mechi hiyo, moja ya mabao hayo lilikuwa la kujifunga kupitia kwa nahodha wa KMC, Kenny Ally, aliyejifunga kwa mpira wa kichwa uliomalizia wavuni. Mbali na nyota huyo, beki Hance Masoud naye ni miongoni mwa wachezaji waliojifunga wakati KMC ikifungwa bao 1-0 dhidi ya JKT Tanzania alipokuwa akijaribu kuokoa hatari iliyokuwa ikielekea langoni. Pia, mchezaji mwingine ni Ibrahim Nindi aliyejifunga katika mchezo dhidi ya Dodoma Jiji, sawa na mwenzake Ismail Gumbo aliyejifunga mbele ya wapinzani hao. Hadi sasa, KMC inayoburuza mkia na kusubiri muujiza wa kunusurika kushuka daraja ndiyo inaongoza kwa kuwa na wachezaji wanne waliojifunga katika harakati za kuokoa hatari langoni mwao.


BAKARI MWAMNYETO (YANGA)

Mei 13, Yanga kwa mara ya kwanza ilionja kipigo kwenye Ligi Kuu ilipolala mabao 3-2 dhidi ya Dodoma Jiji, huku nahodha wake, Bakari Mwaamnyeto, akiingia kwenye lawama katika mchezo huo.

Yanga, licha ya kutangulia kuongoza kwa mabao mawili, ilijikuta ikiambulia kichapo hicho huku Mwaamnyeto akihusika katika mabao mawili ya kujifunga na kuinufaisha Dodoma Jiji kuondoka na pointi tatu.


FRANCIS CHAUDA (MTIBWA SUGAR)

Nyota huyo aliyepandishwa kutoka timu ya vijana (U-20) ya Mtibwa Sugar, Francis Chauda, alijikuta akiikaanga timu yake walipocheza dhidi ya TRA United na kupoteza kwa mabao 2-1. Chauda alijifunga katika dakika ya 90. Kabla ya kosa hilo, matokeo yalikuwa 1-1, lakini hadi kipyenga cha mwisho Mtibwa Sugar iliambulia maumivu na kukosa hata pointi moja. Kinda huyo alibabatizwa na mpira uliopigwa na nyota wa TRA United, Shaban Chilunda, aliyepokea pasi safi ya Ramadhan Chobwedo, na mpira kuishia kambani na kuwakatisha tamaa wakata miwa hao.


SHABAN MGUNDA (FOUNTAIN GATE)

Wakati Fountain Gate ikifungwa mabao 2-0 na Mtibwa Sugar, moja ya mabao yaliyoipa ushindi Mtibwa lilikuwa la kujifunga kupitia kwa Shaban Mgunda wakati wa piga-nikupige langoni mwao. Mchezo huo ulikuwa wa raundi ya pili uliochezwa Septemba 28, 2025, ambapo Mtibwa Sugar ikiwa mwenyeji iliisambaratisha Fountain Gate na kujihakikishia pointi tatu.


ANDY BIKOKO (DODOMA JIJI)

Pamoja na kiwango bora alichoonyesha hadi sasa na kuibeba Dodoma Jiji katika safu ya ulinzi, Andy Bikoko ni miongoni mwa wachezaji waliohusika kujifunga katika Ligi Kuu msimu huu.  Nyota huyo raia wa DR Congo alihusika kwenye bao la kujifunga wakati Dodoma Jiji ikilala kwa mabao 3-1 dhidi ya Coastal Union katika mchezo uliopigwa Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga, ambapo mpira wa Maabad Maabad ulimbabatiza na kujaa wavuni.


MARCO MHILU (TANZANIA PRISONS)

Nyota huyo mwenye uwezo mkubwa akiwa na mpira atakumbukwa kwa bao la kujifunga wakati Tanzania Prisons ilipocheza dhidi ya ndugu zao, Mbeya City, katika mchezo uliopigwa kwenye Uwanja wa Sokoine.

Katika mchezo huo ambao kila timu ilihitaji ushindi ili kujiweka katika nafasi nzuri, mabao ya Mbeya City yalifungwa na Eliud Ambokile kabla ya Mhilu kujifunga kwa pasi iliyomshinda kipa Edward Mwakyusa. Bao pekee la maafande lilifungwa na Emanuel Martin aliyepiga shuti kali lililojaa wavuni na kumwacha kipa wa Mbeya City, Hashim Mussa, akiwa hana la kufanya. Matokeo hayo yaliipa Mbeya City pointi tatu na kulipa kisasi.

Hata hivyo, hadi sasa ni mabao 10 ya kujifunga yaliyofungwa na wachezaji, idadi ambayo ni ndogo ikilinganishwa na misimu mitatu iliyopita. Msimu wa 2024/25 kulifungwa mabao 19 ya kujifunga, 2023/24 yalikuwa 20 na 2022/23 yalikuwa 12.

Hadi sasa zimebaki mechi tano kabla ya msimu kumalizika. Kutokana na presha iliyopo kwa kila timu kufikia malengo yake, huenda tukashuhudia maajabu zaidi au idadi hiyo kubaki ilivyo kutokana na utulivu na nidhamu itakayotumika viwanjani.