Joto kali Kombe la Dunia 2026 na hatari kiafya
Muktasari:
- Katika mechi mbalimbali zilizokuwa zimechezwa ikiwamo za hapo jana, tumeshuhudia kukiwa na mapumziko ya unywaji maji kila baada ya dakika 22. Mbinu hiyo si ya mara ya kwanza, kwani hata Kombe la Dunia lililofanyika nchini Qatar 2022 mapumziko hayo yalikuwepo. Ikumbukwe kuwa joto kali linaweza kumweka mchezaji katika hatari kiafya.
KOMBE la Dunia 2026 limenoga kule nchini Marekani, Canada na Mexico katika hatua ya makundi. Mechi hizo zinachezwa katika kipindi cha msimu wa kiangazi ambapo kiwango cha juu cha joto ni nyuzijoto 32.
Katika mechi mbalimbali zilizokuwa zimechezwa ikiwamo za hapo jana, tumeshuhudia kukiwa na mapumziko ya unywaji maji kila baada ya dakika 22. Mbinu hiyo si ya mara ya kwanza, kwani hata Kombe la Dunia lililofanyika nchini Qatar 2022 mapumziko hayo yalikuwepo. Ikumbukwe kuwa joto kali linaweza kumweka mchezaji katika hatari kiafya.
Sababu kubwa ya hatari hiyo ni kutokana na mwili kupoteza maji na madini mwilini kwa kiwango kikubwa kuliko kawaida kwa njia ya jasho, ambapo kiwango ni kikubwa katika joto kali. Endapo upotevu wa maji mwilini hautadhibitiwa, ndivyo hatari ya kupata madhara huwa juu.
Joto kali linaweza kuwa na athari kwa wachezaji na mashabiki ikiwamo kupoteza maji mwilini, kuumwa kichwa, kiharusi kitokanacho na joto kali na mshtuko wa mwili. Ndio maana hata mashabiki wamevaa mavazi rafiki, huku pia wengine wakiwa na vipepeo na vijifeni vidogo vya kielektroniki ili kupoza mwili. Kucheza katika mazingira ya joto kali kulifanya Shirikisho la Soka Duniani kuja na mwongozo wa mapumziko ya dakika 3 kila baada ya dakika 22 ili kutoa nafasi ya kuongeza kiwango cha maji mwilini.
FAIDA YA MAPUMZIKO YA UNYWAJI MAJI
FIFA ilianzisha mapumziko ya lazima ya dakika tatu ya unywaji maji ili kuwalinda wachezaji kutokana na joto kali la kiangazi na kuhakikisha hali zao ni salama. Tofauti na mashindano ya awali ambapo mapumziko yalikuwa ya hiari kulingana na halijoto, sasa ni lazima.
Utekelezaji wa mapumziko haya umezua mjadala kwa wadau wa soka kwani huwa na faida nyingine ukiacha zile za kiafya. Itakumbukwa hivi sasa nafasi hii pia hutumika na makocha kutoa maelekezo mbalimbali ikiwamo kusahihisha makosa.
Wachezaji hunywa maji maalum ambayo huwa na maji, chumvi nyingi. Vilevile hupewa vinywaji vya kimichezo vyenye virutubisho, nguvu, madini na maji. Pia pale uwanjani huweza kujimwagia maji mwilini na kujifunika na mataulo yenye maji maji ili kuupoza mwili ambao joto huwa juu.
MWILI UNAVYOATHIRIKA NA JOTO KALI
Upungufu wa maji mwilini ni jambo ambalo linaweza kujitokeza kipindi cha joto kali na huku ikiwa hewa ni kavu isiyo na unyevu. Kwa kawaida mwili huhitaji maji na madini kwa ajili ya kazi mbalimbali za mwili ikiwamo msukumo wa damu na kazi za seli mbalimbali.
Wachezaji wanapokuwa katika mazingira ya joto huku wakifanya mazoezi makali au kucheza mechi zenye ushindani hutokwa na jasho sana hivyo kupoteza maji mengi na chumvi mwilini.
Ikumbukwe kuwa kadiri joto linavyozidi kuwa kali ndivyo mwili unavyotoa jasho zaidi, lengo ni kupunguza joto la ndani ya mwili lisizidi kiwango chake cha mwisho. Kuvuja jasho sana huwa zaidi wakati wa kucheza katika joto kali, wakati huo huo kadiri jasho linavyotoka kwa wingi ndivyo pia mwili unavyopoteza maji kupita kiasi. Matatizo mbalimbali ya kiafya yanaweza kujitokeza endapo mchezaji atapata upungufu mkali wa maji mwilini na chumvi kutokana na kuvuja jasho sana.
Hali hii inaweza kuambatana na madhara mbalimbali ya kiafya ikiwamo kuuma na kubana kwa makundi ya misuli ikiwamo ya nyuma ya paja ambayo ni muhimu kwa mchezaji.
Upungufu wa maji na chumvi mwilini usipokabiliwa kwa kuupoza mwili na kurudisha kiwango cha maji kilichopungua unaweza kuleta madhara makubwa kiafya. Matatizo hayo ni pamoja na kupata mchoko mkali na kiharusi kitokanacho na joto kali na kupoteza fahamu, mambo haya yanaweza hata kusababisha kifo.
Madhara mengine yanayoweza kutokana na hali ya kutokwa sana na jasho na kupungukiwa maji mwilini ni pamoja na kichwa kuuma, kuona mawimbi, mwili kuwa dhaifu, kushindwa kutulia, kukosa umakini, kuchanganyikiwa, kichwa kuuma na mwili kuuma.
Tatizo hilo la upungufu wa maji kutokana na joto kali linaweza kumfanya mchezaji akashindwa kucheza kwa kiwango au akacheza lakini akachoka mapema.
Hali ikiwatokea wachezaji wanaweza wakadhaniwa kuwa wanafanya makusudi, kumbe tu wana upungufu wa maji mwilini kutokana na kutoka jasho sana. Mara nyingi wachezaji ambao wanapata madhara haya kirahisi ni wale ambao hawanywi maji ya kutosha kabla ya mechi, na vilevile kutokula vyakula vyenye maji na madini ikiwamo matunda na mboga.
JINSI WANAVYOKABILIANA NA ATHARI YA JOTO
Kwa wachezaji hutakiwa kunywa maji mengi siku mbili kabla ya mechi angalau lita 3–5 za maji kwa siku. Unywaji maji huwa ni lazima wakati wote kwa wachezaji si tu wakati wa joto pekee. Ikumbukwe upungufu wa maji ni kihatarishi cha mchezaji kupata majeraha ya misuli kirahisi.
Hawasubiri kiu ije ili wanywe maji, bali nyakati za mapumziko ya kambini hunywa mara kwa mara au kunywa kidogo mpaka wafikie lengo linalotakiwa kwa masaa waliopangiwa. Vilevile hushauriwa kula matunda kwa wingi kila baada ya mechi na katika mlo wao kutumia mboga mboga kwa wingi. Matunda na mboga huwa na maji mengi na madini.
Hunywa maji ya kutosha kabla ya kuingia mazoezini au katika mechi, na vilevile hunywa maji kila baada ya dakika 30 au wakati wa mapumziko na baada ya kumaliza mazoezi au mechi. Kabla ya mechi wakiwa kambini hutumia vinywaji maalum kwa ajili ya wanamichezo ambapo ndani yake huwa na wanga na chumvi, hujulikana kama sports drinks.
Hawatakiwi kutumia vinywaji vya kuongeza nguvu na kusisimua au kuchangamsha mwili maarufu kama energy drinks kwani si sahihi kutumia kuongeza maji mwilini. Pombe, soda na kahawa ni marufuku kwani si mbadala wa maji yaliyopotea kwa njia ya jasho.
Katika kambi zao hutakiwa kutotembelea maeneo yenye joto na msongamano, hujiachia zaidi maeneo ya wazi yenye kivuli au ndani kwenye viyoyozi.
Hushauriwa kuvaa mavazi mepesi ya wazi kiasi ili kuupa mwili nafasi ya kupumua na kutopoteza maji kwa njia ya jasho.
Hutakiwa kuupumzisha mwili kwa kulala angalau masaa 8–10 kwa usiku mmoja katika chumba tulivu chenye kiyoyozi.
Huduma za mazoezi lainishi ya viungo ya uponaji misuli na huduma ya usingaji yaani masaji hufanyika sana kwani joto huchangia majeraha ya misuli kirahisi.
CHUKUA HII
Kipindi cha mapumziko mafupi ya unywaji maji ya kila baada ya dakika 22 katika hali ya joto kali mchezaji hunywa kiasi cha glasi 4–6 sawa na mililita 115–295.