Jose Mourinho anajua kuzicheza mechi za fainali
Muktasari:
Straika huyo wa Stoke City bao lake alilofunga kwa kichwa dhidi ya Hull City wikiendi iliyopita kwenye ushindi wa 1-0, lilikuwa la 46 kulifunga kwa staili hiyo na kufikia rekodi ya gwiji wa zamani wa Newcastle United, Alan Shearer.
PETER Crouch ana sifa moja kubwa usimsogeze kwenye goli lako kisha timu yake ikawa inapiga mipira mirefu kwenda eneo hilo, atakuumiza tu. Ni hodari kweli kweli kwenye kuichezea mipira ya juu. Tena anaicheza kwa uhodari mkubwa kwa kutumia kichwa chake. Ushahidi huo unaojionyesha kwenye idadi ya mabao ya kichwa aliyofunga kwenye Ligi Kuu England hadi sasa.
Straika huyo wa Stoke City bao lake alilofunga kwa kichwa dhidi ya Hull City wikiendi iliyopita kwenye ushindi wa 1-0, lilikuwa la 46 kulifunga kwa staili hiyo na kufikia rekodi ya gwiji wa zamani wa Newcastle United, Alan Shearer.
Arsene Wenger amewahi kusema kama unapenda mpira basi utampenda Tomas Rosicky. Wenger amesema hilo kutokana na uhodari wa staa huyo wa Czech pindi mpira unapokuwa kwenye miguu yake. Anaweza kuufanyia chochote mpira unapokuwa kwenye miguu yake kwa uhodari huo huo.
Kila mmoja ana kimoja anachoweza kukifanya kwa uhodari mkubwa. Kama kutakuwa na mchakato wa kumsaka mtu aliyehodari kwa mechi za fainali, Jose Mourinho, jina lake litakaa juu kwenye orodha hiyo. Mreno huyo anafahamu vizuri tena kwa uhodari mkubwa namna ya kushinda mechi za fainali. Miaka yake 12 katika ukocha, amefika fainali makombe 12 na ameshinda mara 10 kati yao. Huu ni uhodari.
Sawa, alisubiri kwa miaka mitatu kubeba taji lake jingine tangu alipotwaa mara ya mwisho, lakini kipindi hicho pengine ndicho kirefu zaidi kutoka kapa katika maisha yake ya ukocha.
Karibu asilimia 50 ya fainali hizo zimechezwa kwa dakika za ziada, ikiwamo taji lake la kwanza la Kombe la Uefa alipocheza dhidi ya Celtic. Hii ni rekodi ya kipekee pengine kuliko makocha wengine maarufu barani Ulaya. Mourinho anafahamu namna ya kushinda mechi hizi za fainali.
Akienda kuwavaa Tottenham Hotspur uwanjani Wembley Jumapili na kushinda 2-0, Mourinho alitambua anakosa huduma ya kiungo wake makini, Nemanja Matic.Hata hivyo, unajua Mourinho alichokifanya? Hakumtumia Juan Cuadrado wala Oscar kuziba pengo hilo kwenye kiungo. Badala yake, akamchukua kinda ambaye ni beki wa kati, Kurt Zouma na kumchezesha kama kiungo mkabaji.
Kwa uamuzi huo tayari aliwavuruga Spurs kwenye sehemu ya kiungo kwa sababu Zouma anatumia nguvu kama ambavyo angefanya Matic kama angekuwa uwanjani.
Kwenye safu ya ulinzi, Mourinho alimtumia John Terry na Gary Cahill, ambao waliweza kumfunika kabisa Harry Kane, ambaye kwenye mechi ya Ligi Kuu iliyofanyika Mwaka Mpya uwanjani White Hart Lane aliwasumbua sana Spurs iliposhinda 5-3. Lakini, mechi hiyo haikuwa fainali, pengine hadithi ingekuwa nyingine.
Mourinho alimtumia pia Ramires kwa shughuli moja tu ya kukaba, huku akimsogeza mbele Cesc Fabregas ili kuhakikisha anawachezesha Willian na Diego Costa. Mourinho hakutaka kushindana kwa mpira na Spurs na alichokifanya ni kufanya uamuzi sahihi kitu ambacho aliweza kukifanya kwenye mchezo huo na kuvuna matokeo ya ushindi na kupata taji lake la kwanza tangu aliporejea Stamford Bridge katika awamu yake ya pili.
Takwimu zinaonyesha kwamba, taji la kwanza Mourinho kutwaa akiwa kocha wa Chelsea lilikuwa Kombe la Ligi wakati alipofanya hivyo msimu wa 2004-2005 ilipokuwa awamu yake ya kwanza klabuni hapo na sasa katika awamu ya pili taji hilo hilo limekuwa la kwanza tena kwa upande wake. Tumsubiri Mourinho ataleta mataji gani mengine mbele yake kuna mataji mawili, Ligi Kuu na Ligi ya Mabingwa Ulaya.